Na CLARA MATIMO- MWANZA, SIMIYU
SERIKALI imesema ipo tayari kupokea wawekezaji muda wowote katika sekta mbalimbali pamoja na kusikiliza changamoto zao ili waweze kufanya biashara katika mazingira mazuri.
Hayo yalibainishwa jana na Mkurugenzi mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Nchini (TIC), Dk. Maduhu Kazi, baada ya kupokea shule ya sekondari iliyojengwa katika Kijiji cha Bugatu Wilaya ya Magu Mkoani Mwanza na chuo cha ufundi kilichopo kijiji cha Kasori wilayani Busega mkoa wa Simiyu vilivyojengwa na kiwanda cha kuchambua pamba cha Alliance Ginnery vyenye thamani ya Sh. milioni 330.
Alisema TIC muda wote milango ipo wazi ili kuhakikisha inakuwa na taarifa za kila mwekezakaji na kujua kama anakabiliwa na changamoto
yoyote na kuitatua kwa haraka kwa kuwa Serikali inahitaji wawekezaji ambao wako tayari kuisaidia jamii kuinua uchumi.
“Katika kufanikisha hilo kwa sasa tunatumia teknolojia ya kisasa kwenye mawasiliano na wawekezaji, tunatumia ofisi za kanda zilizopo jijini Mwanza ili kuhakikisha kila mfanyabiashara anawekeza katika mazingira yasiyokuwa na usubufu ama urasimu, watu wanaotaka kuwekeza waje TIC bado kuna fursa nyingi,”alisema na kuongeza;
“Kiwanda cha Alliance Ginnery kimezingatia maagizo ya serikali ya awamu ya tano, tunahitaji wawekezaji kama hawa ambao wanaisaidia jamii inayowazunguka siyo wawekezaji wanaokwenda kuchimba mashimo mawili ya choo halafu wanasema wameisaidia jamii,” alisema.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Magu ambako shule hiyo imejengwa, Salum Kalli, alikishukuru kiwanda hicho kwa msaada huo na kubainisha kwamba kimesaidia kutatua changamoto ya watoto kutembea umbali mrefu kwenda shule.
Naye Meneja wa kiwanda cha Alliance Ginnery, Boaz Ogola, alisema wametoa msaada huo wa shule uliyogharimu Sh milioni 150 baada ya kuona watoto wa eneo hilo wanatembea umbali mrefu kwenda shule pia wamejenga chuo cha ufundi kilichogharimu Sh milioni 180 baada ya kubaini wanaomaliza elimu ya msingi wanakosa fursa ya kupata elimu ya ufundi ili iwasaidie kujiajiri.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Antony Mtaka, baada ya kukabidhiwa chuo cha ufundi aliagiza wasichana wote waliomaliza darasa la saba kuanza kusajiliwa ili waanze kupata mafunzo pia aliwasisitiza wazazi na walezi kuacha kupokea mahari kuwaozesha watoto wao wa kike waliomaliza darasa la saba.