Ramadhan Hassan, Dodoma
Serikali imevunja mkataba na Kampuni ya Rom Solution Ltd. ya nchini Romania ulioingiwa baina yake na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.
Mkataba huo ni ule ulioshtukiwa na Rais John Magufuli kabla hajaingilia kati na kuwatumbua aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola na aliyekuwa Kamishna wa Jeshi la Zimamoto, Thobias Andengenye.
Akitangaza uamuzi huo jijini Dodoma leo Ijumaa, Machi 13, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene amesema mkataba huo ulivunjwa rasmi Februari 12, mwaka huu.
Amesema Januari 27, mwaka huu wakati wa sherehe za kuapishwa kwake kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Rais alimuagiza kushughulikia suala la mkataba huo tata baina ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na Kampuni ya Rom Solutions.
“Na katika kushughulikia suala hili, nilibaini kuwepo kwa hati ya makubaliano iliyoingiwa Agosti 22, mwaka jana kati ya aliyekuwa Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na kampuni hiyo.
“Hata hivyo makubaliano yalikuwa ni kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya jeshi la zimamoto vyenye thamani ya Euro milioni 408,416,238.16 ambayo kwa fedha za Tanzania ni zadi ya Sh trilioni moja,” amesema Simbachawene.
Amesema serikali baada ya kupitia hati ya makubaliano baina ya aliyekuwa kamishna, iliona mkataba huo ulikuwa na mapungufu mengi na haikuwa na haja ya kuendelea na makubaliano hayo kwani hayakuwa na tija na hivyo serikali ikaamua kuuvunja Februari 12, mwaka huu.
“Aidha, baada ya kuvunjwa kwa makubaliano hayo hakuna hasara wala madai yoyote ambayo serikali inadaiwa kwa sababu mkataba umevunjika na pande zote mbili zimekubaliana,” amesema Simbachawene.