27.3 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 1, 2021

CCM, Chadema wapishana Segerea

Andrew Msechu – Dar es Salaam

UONGOZI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na wa CCM, umejikuta katika mvutano kuhusu nani aliyehusika kumtoa Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema),  ambaye alitoka rasmi gerezani jana saa 10 jioni.

Ilikuwa ni tukio la aina yake, wakati Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole akiwa katika eneo la Gereza la Segerea aliita waandishi wa habari kuzungumza nao baada ya kuachiwa huru kwa Msigwa, lakini hali ilibadilika katika hatua za mwisho na kulazimika kuwatoroka waandishi.

Mchungaji Msigwa ambaye naye alitarajiwa kuzungumza na waandishi baada ya kutoka gerezani, pia aliondoka kimya kimya huku waandishi wakibaki wametahayari kuhusu nini kilichotokea hadi viongozi hao ambao waliwaita kwa kusudi maalumu kuamua kuwatelekeza eneo hilo kimya kimya, wakiwa katika magari yenye vioo vyeusi.

Awali, katika eneo la gereza hilo, majira ya saa nane mchana, Polepole ndiye aliyekuwa wa kwanza kuwasili na baadaye aliwasili wakili wa Chadema, Frank Kiwelo ambaye alikuwa akishughulikia suala la kuachiwa kwa Msigwa.

Punde baada ya wakili huyo kufika akiongozana na Mchungaji Beneth Simon Msigwa ambaye ni kaka wa Msigwa, waliendelea na utaratibu wa kumtoa mbunge huyo ambaye alikuwa akishikiliwa katika gereza hilo la Segerea pamoja na viongozi wengine wa Chadema baada ya hukumu iliyotolewa Jumanne.

Katika hukumu hiyo ya kesi ya uchochezi iliyokuwa ikiwakabili viongozi wanane wa Chadema, Msigwa alitakiwa kulipa faini Sh milioni 10 kwa kila kosa kati ya makosa manne yaliyomhusu, au kutumikia kifungo cha miezi mitano kwa kila kosa.

Tayari uongozi wa Chadema ulishatangaza kuwalipia faini ya Sh milioni 100 wabunge wao watatu, ambao ni Ester Matiko (Tarime Mjini), Ester Bulaya (Bunda Mjini) na Halima Mdee (Kawe) ambao waliruhusiwa kuwa huru jana asubuhi.

Chadema ilitangaza kuendelea na harambee kukusanya zaidi ya Sh milioni 90 zilizokuwa zimebaki kati ya Sh milioni 320 walizokuwa wakidaiwa viongozi wao saba waliokuwa mahakamani, baada ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho ambaye alijiunga na CCM, Viscent Mashinji kulipiwa Sh milioni 30 na chama chake kipya juzi.

KAULI YA CHADEMA

Akizungumzia kuachiwa kwa Mchungaji Msigwa, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema alisema kuna sintofahamu kuhusu hatua ya wanaodai kuwa wamemlipia faini hiyo kuwa ni ndugu zake, kwa kuwa yeye hata hivyo hawafahamu kwa undani.

Mrema alisema ukweli ni kwamba wao walishamlipia faini Mchungaji Msigwa tangu juzi na kwamba wanashangaa kama kuna mtu mwingine aliyemlipia na kama ni kweli basi kuna jambo lililojificha.

“Sisi tulishamlipia Msigwa na tulishapewa namba ya kulipia (control number) tangu jana (juzi, Jumatano Machi 11) na tukaendelea na utaratibu wa malipo.

“Tunavyofahamu kila mfungwa huwa ana namba moja ya kulipia, hakuna mfungwa anayeweza kuwa na namba mbili, hata sidhani kama mahakama inaweza kufanya hivyo, yaani kutoa namba mbili kwa mfungwa mmoja.

“Ni kwamba tunachofahamu Mchungaji Msigwa ametoka kutokana na malipo tuliyoyafanya kupitia kwa mawakili wetu ambao walikuwa wakiendelea kushughulikia suala hili.

“Hata baada ya kuondoka Segerea, aliondoka na wakili wetu Frank Kiwelo ambaye ndiye aliyekuwa akiwatetea na kushughulikia suala hilo,” alisema Mrema.

Alisema wakili huyo ndiye aliyekwenda mahakamani na kupewa namba ya kufanyia malipo ambayo ilitumika kufanya malipo, hivyo hata kama kuna watu wengine waliokuwa wamekwenda huenda walikwenda kwa sababu zao nyingine.

CHANZO CHA MVUTANO

Mvutano huo ulitokea muda mfupi baada ya taarifa kuwa Rais Dk. John Magufuli amemsaidia Sh milioni 38 Mchungaji Msigwa ili kumtoa gerezani, baada ya ndugu zake kumchangia Sh milioni mbili.

Taarifa hiyo ilitolewa na mmoja wa ndugu zake, ambaye alisema Rais Magufuli amemnusuru Msigwa baada ya kuombwa na familia kufanya hivyo.

Akizungumza nje ya mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana asubuhi, kaka mkubwa wa Mchungaji Msigwa, Mchungaji Beneth alisema tangu juzi wamekuwa kwenye kampeni kubwa ya kutafuta fedha, lakini hawakufanikiwa kutimiza Sh milioni 40.

“Katika familia tulipata Sh milioni mbili, Rais Magufuli na sisi ni ndugu… Kayemba, yaani mjomba wetu kaoa binti yake,” alisema Mchungaji Beneth.

Alimshukuru Rais kwa msaada wake kwa sababu kama familia walikuwa wameshakwama.

Mchungaji Msigwa alitiwa hatiani katika mashtaka manne ikiwamo kufanya mkusanyiko, kukaidi amri halali ya polisi na kushawishi wananchi wa Kinondoni kutembea na silaha mbele ya umma.

Mbali na Mchungaji Msigwa, mahakama hiyo pia iliwatia hatiani Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, aliyekuwa Katibu Mkuu, Dk. Vicent Mashinji, Halima Mdee, Esther Bulaya, Esther Matiko, Salum Mwalimu na John Mnyika.

Mdee, Bulaya na Matiko walifanikiwa kutoka baada ya kulipa faini.

Hukumu ilitoka Machi 10 mwaka huu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba baada ya pande zote mbili kufunga ushahidi ambapo Jamhuri ilikuwa na mashahidi nane na upande wa utetezi mashahidi 15.

MDEE ASIMULIA

Jana, katika ofisi za Makao Makuu ya Chadema, Kinondoni, Dar es Salaam, viongozi wa Chadema walioachiwa baada ya kulipiwa faini walitoa shukrani kwa Watanzania kwa kile walichoeleza kuwa ni kutokana na namna walivyowasitiri katika wakati huu mgumu walio nao.

Akizungumza na wanahabari baada ya kutoka gerezani jana, Mdee ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), alisema hukumu hiyo iliwaweka mahali pabaya kwa kuwa hawakuwa na fedha katika akaunti zao na kudai kuwa walitozwa faini kubwa kuliko uwezo waliokuwa nao.

Alisema kilichotokea ni kama vile hakimu aliyewapa hukumu hiyo alijua kuwa katika akaunti zao walikuwa hawana kitu na akaunti za mwenyekiti wa chama hicho, Mbowe zote zimezuiwa.

Mdee alisema kutokana na ukweli huo, hawana namna zaidi ya kurudi kwa Watanzania na wanachama wao ili kuomba michango ili kunusurika kutumikia kifungo cha miezi mitano kwa kila kosa.

“Hapa mnaweza kuona, kwa mtu mwenye makosa matatu atatumikia kifungo cha miezi 15 ambacho ni zaidi ya mwaka gerezani, kwa mwenye makosa manne atatumikia kifungo cha miezi 20 ambayo ni karibu miaka miwili, na mwenye makosa saba atatumikia miezi 35,” alisema Mdee.

Alisema wanaendelea kuomba Watanzania kwa umoja wao waendelee kutoa michango kuwatoa gerezani viongozi watano wa chama hicho ambao bado walikuwa gerezani hadi jana mchana.

ESTER MATIKO 

Kwa upande wake, Matiko alisema kipekee anatoa shukrani kwa maombi na mapambano ya pamoja kwa miaka miwili ambayo kesi hiyo ilikuwa ikiendelea na kuonyesha utayari katika kupigania demokrasia ya kweli nchini.

“Kwa namna ambavyo mmeonyesha ushirikiano katika hili, mmetuma salamu kwa CCM na tumepewa takwimu za uchangiaji kwamba Sh 200, Sh 500 na 1,000 ndizo zilizokuwa nyingi.

“Na mimi niseme sitarudi nyuma kamwe katika kupigania haki na demokrasia katika nchi hii.

“Haya yote yanatokea kwa sababu Watanzania hawa wanaamini kuwa siku Chadema ikishika dola itakwenda kuwatetea. Na mimi nasema sitanyamazishwa kwa namna yoyote, iwe kwa kifungo au vyovyote,” alisema Matiko.

Aliwashangaa wale wenye kipato cha kati na cha juu wanaoonekana kurudi nyuma katika kuchangia na kuwezesha kutolewa kwa viongozi wa Chadema jela wakati wao ndio waliojaa magerezani kwa uhujumu uchumi.

“Hawa ninawaomba wasome alama za nyakati na waamue kushirikiana nasi. Na kwa kweli ninasimama kushukuru jinsi Watanzania walivyoshirikiana nasi kwa kuwa wanajua kinachofanyika sicho.

“Chadema ni ya Watanzania na tuko tayari kuwapigania Watanzania pale tunapoona haki haitendeki. Sasa hivi nimepata ari zaidi ya kupigania haki dhidi ya uovu,” alisema Matiko.

ESTER BULAYA

Kwa upande wake, Mbunge wa Bunda Mjini, Bulaya alisema kwa michango iliyotolewa na kuwawezesha kutoka gerezani, ni salamu tosha kwa CCM kwamba Oktoba itaondoka madarakani.

Alisema safari imeshaanza, hivyo wale ambao bado wako nyuma waunge tela kwa sababu wenye kipato cha chini wameonyesha njia katika kutetea demokrasia ya kweli.

“Tunawaomba Watanzania, hasa wa kipato cha kati na wale wa kipato cha juu endeleeni kuchanga, ninaamini kama mna hofu yoyote ya kujulikana kuna namna ya kuchangia, jitokezeni tutawalinda. Ninachoamini kule gerezani nilienda kupumzika na sasa nimetoka mapambano yanashika kasi,” alisema Bulaya.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,530FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles