WALTER MGULUCHUMA-KATAVI
SERIKALI imeanza kutafuta masoko mapya ya zao la tumbaku baada ya kampuni ya ununuzi yaliyopo sasa kupunguza idadi ya kilo kila mwaka kwenye vyama vya msingi vya ushirika.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mathew Mtigumwe wakati alipokuwa akizungumza na wadau mbalimbali wa kilimo mkoani Katavi.
Alisema kutokana na kampuni hizo kushusha idadi ya kilo za tumbaku walizokuwa wakinunua kwa wakulima kupitia kwenye vyama vyao vya ushirika vya msingi Serikali imeona itafute masoko mapya ya zao la tumbaku kukabiliana na tatizo hilo.
Katibu mkuu huyo alieleza kuwa wameiagiza Bodi ya tumbaku nchini kwenda kwenye nchi zinatumia zaidi tumbaku kutafuta soko la zao hilo.
“Mpaka sasa kuna kampuni moja ambayo tayari imeonyesha nia ya kununua tumbaku na tunatarajia kuanza kununua kilo milioni moja msimu huu, hivyo jitihada za kutafuta masoko mengine mapya zinaendelea kufanywa na Serikali.
Awali baadhi ya wadau wa tumbaku Mkoa wa Katavi walionyesha wasiwasi wao kuhusu soko la zao hilo kutokana na kushuka kwa ununuzi wa kutoka kilo milioni 16 miaka mitatu iliyopita hadi kufikia kilo milioni sita kwa msimu huu wa kilimo.
Mmoja wa wadau hao, Selemani Kaitila alisema ununuzi wa tumbaku imekuwa ukishuka mwaka hadi mwaka kutokana na kampuni zinazonunua tumbaku huku mapato ya halmashauri yakizidi kuporomoka kwa kukosa ushuru unaotokana na zao hilo.