23.8 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 17, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yafanya mapitio ya Sera ya Taifa ya Biashara, yatangaza maboresho makubwa

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Serikali imefanya mapitio ya Sera ya Taifa ya Biashara ya mwaka 2003 na kutoa toleo la 2023, lenye lengo la kuweka mfumo mkakati madhubuti unaolenga kuboresha mazingira ya biashara, kuongeza ukuaji wa kiuchumi na kuboresha ustawi wa wananchi.

Sera hiyo mpya inalenga kuimarisha na kuendeleza biashara ya ndani na nje, pamoja na kuimarisha mtengamano na ushiriki wa nchi katika biashara na nchi zingine rafiki, kikanda na kimataifa.

Akizungumza leo Julai 28 na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Selemani Jafo, alisema utekelezaji wa sera hiyo utailetea nchi faida nyingi ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa mchango wa sekta ya biashara katika pato la taifa.

“Sera hii ni marejeo ya sera ya mwaka 2003 ambayo imefanyiwa marekebisho ili iweze kuendana na mabadiliko ambayo yametokea katika nyanja mbalimbali kikanda na kimataifa,” alisema Dk. Jafo.

Aliongeza kuwa sera hii itaimarisha mazingira ya ufanyaji biashara, kuvutia uwekezaji, kuongeza shughuli za biashara na ajira, kuongeza kipato cha wananchi, na kuimarika kwa uzalishaji viwandani kutokana na upatikanaji wa masoko ya uhakika hivyo kuchochea jitihada za ujenzi wa uchumi wa viwanda.

“Sera hii inaongozwa na kauli mbiu isemayo ‘Ushindani wa Biashara katika kuchochea kasi ya Mabadiliko ya Kijamii na Kiuchumi yanayoongozwa na Viwanda’. Inatarajiwa kuzinduliwa rasmi Jumanne, Julai 30 na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Mashaka Biteko,” alisema Dk. Jafo.

Dk. Jafo alieleza kuwa sera hiyo inachangia kuwepo kwa ushindani huru na haki katika biashara, kumlinda mlaji, kuimarika kwa ratibu wa biashara, na kuondokana na mgongano wa kisera, kisheria, na mgawanyo wa majukumu ya kitaasisi katika masuala ya biashara.

“Kuimarika kwa miundombinu ya masoko na biashara; kuimarika na kuongezeka kwa biashara ya nje, na kuongezeka kwa ufanisi katika utendaji wa shughuli za biashara kupitia matumizi ya mifumo ya kibiashara,” alisema Dk. Jafo.

Dk. Jafo alitaja baadhi ya mambo yaliyoainishwa katika sera hiyo ni kuimarisha, kukuza na kuendeleza biashara ya ndani na nje, kuimarisha mtengamano na ushiriki wa nchi katika biashara na nchi zingine rafiki, kikanda na kimataifa, na kuimarisha maendeleo na ujenzi wa miundombinu ya masoko na biashara.

Alisema sera hiyo pia inalenga kuimarisha usimamizi wa ushindani halali wa kibiashara na kumlinda mlaji, kuendeleza biashara ya huduma, kuwezesha na kuimarisha biashara mtandao kupitia matumizi ya teknolojia, na kuimarisha upatikanaji wa mikopo na mitaji ya biashara.

Dk. Jafo alieleza mafanikio ya sera ya mwaka 2003 kuwa ni serikali kufanikiwa kushiriki kikamilifu katika majadiliano mbalimbali ya biashara baina ya nchi na nchi, kikanda na kimataifa kwa lengo la kuongeza fursa zaidi za biashara ya bidhaa na huduma kutoka Tanzania ikijumuisha kupata masoko yenye masharti nafuu kwa ajili ya wafanyabiashara wa Tanzania.

“Fursa hizo ni pamoja na zile zinazotokana na soko la Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), AfCFTA, soko la China kwa kuuza bidhaa bila kulipa ushuru wala kikomo kwa asilimia 98 ya bidhaa zote kutoka Tanzania, India, AGOA kwa kuuza zaidi ya bidhaa 6,400 bila ushuru,” alieleza Dk. Jafo.

Faida nyingine ni kumewezesha mchango wa biashara katika pato la taifa kufikia asilimia 8.3 mwaka 2023, kupitia fursa hizo mauzo kwenda Jumuiya ya Afrika Mashariki yameongezeka kutoka shilingi trilioni 1.12 mwaka 2016 hadi Sh trilioni 3.022 kwa mwaka huo.

Vilevile, mauzo ya nje kwenye Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika yameongezeka kutoka shilingi trilioni 2.607 mwaka 2016 hadi shilingi trilioni 4.422 mwaka 2023, na mauzo nje kwenye Jumuiya ya Ulaya yameongezeka kutoka shilingi trilioni 0.605 mwaka 2016 hadi shilingi trilioni 3.835.65 mwaka 2023, huku bidhaa zilizouzwa kwa wingi ni za kilimo, hususan kahawa, chai, mahindi, ngano, mchele, mbogamboga na bidhaa za viwandani.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkazi wa kampuni ya Trade Mark Afrika, Elibariki Shami, aliipongeza Tanzania kwa kufanya maboresho hayo na kusisitiza kuwa ni vema kila taifa liige hatua hiyo ili biashara ziweze kufanyika kwa urahisi.

“Sera hii itarahisisha kufanya biashara katika maeneo mbalimbali ya kikanda kwa sababu nchi nyingi za Afrika zinashindwa kufanya kwa pamoja kwa sababu ya kukinzana katika sera za biashara,” alisema Shami.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles