24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali kujenga matenki sita mapya ya mafuta Kigamboni na kufufua tenki namba Nane

Na Faraja Masinde, Mtanzania Digital

Serikali imeazimia kujenga matenki mapya sita ya mafuta na kufufua tenki namba nane katika eneo la Kigamboni, Dar es Salaam, ili kuhakikisha nchi inakuwa na akiba ya kutosha ya mafuta wakati wote.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Balozi Ombeni Sefue, amebainisha hayo leo Ijumaa, Juni 7, 2024, wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya ziara ya kuangalia hali ilivyo hivi sasa.

“Leo Bodi ya TPDC imefanya ziara hapa Kigamboni kuona maeneo ambayo huko nyuma tulikuwa tunafanya biashara ya kusafisha na kuuza mafuta, lakini biashara hiyo ikawa imesimama,” alisema Balozi Sefue.

“Hapa kuna miundombinu ambayo ni muhimu sana kwetu sisi TPDC kutekeleza jukumu letu tulilopewa kitaifa la kuhakikisha kwamba kuna hifadhi ya kutosha ya mafuta kwenye nchi yetu,” amesema Balozi Sefue.

Balozi Sefue ameeleza kuwa tenki namba nane lilijengwa na kukamilika mwaka 1993 na lilifanya kazi kwa miaka sita kabla ya kufungwa mwaka 2000 kutokana na mabadiliko ya soko huria na faida kutotosheleza. Hata hivyo, kutokana na mwelekeo mpya wa kitaifa na kiserikali chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, TPDC inarudi kwenye jukumu lake la kuhakikisha kuwa taifa linakuwa na akiba ya mafuta wakati wote.

“Katika eneo hili la Kigamboni, TPDC itafufua tenki namba nane na kujenga mengine sita mapya, lengo likiwa ni kuhifadhi tani 162,000 za mafuta kwa Dar es Salaam,” amesema Balozi Sefue na kuongeza: “Kando na Dar es Salaam, pia tutajenga matenki mengine ya mafuta kwenye kanda zote ikiwamo kanda ya kati, kanda ya ziwa na nyingine ili kuhakikisha kwamba wakati wote nchi inamafuta ya kutosha na haipitii kipindi kigumu.”

Balozi Sefue alibainisha kuwa mchakato wa kufufua tenki namba nane unaweza kuchukua miezi 20, na wanatarajia kuwa kazi hiyo itakamilika kufikia mwaka 2026.

Meneja wa Biashara ya Mafuta kutoka TPDC, Baraka Nyakutonya, ameongeza kuwa tayari wameshatangaza utaratibu wa ujenzi wa matenki sita katika eneo hilo, ikiwemo zabuni ya tathmini ya mazingira. “Kuna kampuni kadhaa zimeonyesha nia ya kufanya kazi hii, na Juni 17, mwaka huu tutatangaza tenda ya zabuni hii. Pia tunategemea ndani ya mwezi huu kutangaza zabuni nyingine kwa ajili ya kupata mshauri wa mradi,” amesema Nyakutonya.

Nyakutonya alifafanua kuwa uwezo wa tenki namba nane ni tani 46,000 za mafuta, lakini opareshenary ni tani 45,000. Baada ya kupata taarifa ya mshauri, TPDC itakuwa na taarifa kamili juu ya lini mradi utakamilika na utagharimu kiasi gani.

Serikali inatumai kuwa juhudi hizi za kuongeza hifadhi ya mafuta zitasaidia kuivusha nchi katika vipindi vya mabadiliko ya bei ya mafuta katika soko la dunia, hivyo kuhakikisha kuwa uchumi wa taifa unakuwa imara na usiokuwa na misukosuko ya upatikanaji wa nishati hiyo muhimu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles