21.5 C
Dar es Salaam
Saturday, July 27, 2024

Contact us: [email protected]

Polisi yakamata toy zinazotumika kufanyia uhalifu

Na Winfrida Mtoi, Mtanzania Digital

Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, imemkamata Hassan Yahya ‘Kobra’ na wenzake watatu wakiwa na toy ambazo wanazitumia kama silaha katika kufanya uhalifu.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 7,2024, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amezitaja toy hizo huwa ni Pistol toy 7, AK47 toy 2, jambia toy 2, shoka toy 2, kama sehemu ya maandalizi ya kufanya kuhalifu.

Ameeleza kuwa watuhumiwa hao walikamatwa Mei 21,2024 maeneo ya Kipunguni B, Ukonga wakiwa pia na dawa za kulevya aina ya bangi huku wakipanga njama za kufanya vitendo vya kihalifu yakiwemo makosa ya unyang’anyi.

Amesema jeshi hilo limefanikiwa kukamata watu hao kutokana na mkakati uliopo wa kutokomeza uhalifu jijini.

” Kazi hii maalum ya kuzuia vitendo vya kihalifu ni muendelezo wa kazi hiyo iliyoanza mwezi Aprili 2024 na inayoedelea kulenga, kufuatilia, kuchunguza na kukamata wahalifu mbalimbali pamoja na wanaopanga njama za kuiba, kuvunja nyumba, wanaouza, kusafirisha na kutumia dawa za kulevya,”amesema Kamanda Muliro.

Aidha amewataja watuhumiwa wengine 13 waliokamatwa ambao wanahusika na kuuza, kusafirisha na kutumia dawa za kulevya ikiwemo bangi wakiwamo Hamis Seif (18) Mkazi wa Mbondole na Bosco Bosco (18) Mkazi wa Kipunguni Ilala.

“Watuhumiwa hao wamekamatwa na Puli 531 na kete 2,639 na misokoto 158 ambayo ilikuwa tayari kutumiwa wakiwa pia na viroba vinne vya bangi pia pikipiki mbili MC 673 CKM na MC 591 CUW zilizokuwa zinatumika kusambaza bangi hizo pia zimekamatwa,” ameeleza Kamanda huyo.

Kwa upande wa usalama wa barabarani, amesema Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linaendelea kuwafuatilia, kuwakamata na kuwafikishwa mahakamani madereva wasiotii sheria na kanuni za usalama barabarani wakiwemo walevi na makosa hatarishi ya wapanda pikipiki za miguu miwili na miguu mitatu.

Amesema kwa kipindi cha mwezi Aprili hadi Mei 2024 jumla ya makosa 67 ya pikipiki yalikamatwa yakihusisha kutokuwa na leseni, kuzidisha abiria na kuendesha pikipiki wakiwa wamelewa ambapo madereva 21 walifikishwa mahakamani, na wengine walitozwa faini za papo hapo.

Madereva wa magari sita walikamatwa kwa makosa ya kuendesha wakiwa wamelewa ambapo madereva wawili walifikishwa mahakamani na wengine wanne walitozwa faini papo hapo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles