24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, November 7, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali: Hakuna Haki ya Muathirika wa Maafa ya Hanang’ itakayopotea

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Jenista Mhagama ametoa wito kwa wananchi kushirikiana na Serikali kuwahifadhi waathirika wa Maporomoko ya Mawe na Matope kutoka Mlima Hanang’ mkoani Manyara.

Kauli hiyo ameitoa wakati wa kikao na viongozi wa Serikali, Wazee na waathirika wa maporomoko hayo katika Kijiji cha Gendabi Halmashauri ya Wilaya ya Hanang’ mkoani humo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge na Uratibu), Jenista Mhagama akizungumza na Viongozi wa Serikali  na Waathirika wa maafa katika kijiji cha Gendabi Halmashauri ya Hanang mkoani Manyara alipowatembelea na kuona hali inavyoendelea katika eneo hilo.

Ametumia fursa hiyo kuwakumbusha kuwa serikali itaendelea kutoa huduma zote muhimu kwa kila aliyeathirika na maafa hayo na kipaumbele ni wale waliohifadhiwa katika Kambi za muda zilizopo na endapo kuna mazingira rafiki ya kuhifadhiwa na ndugu, jamaa na marafiki wanapaswa kufuata utaratibu zilizopo.

“Tunahitaji kupunguza mikusanyiko mikubwa kwenye makambi kiafya siyo sahihi tutahakikisha tunamhudumia kila muathirika popote atakapokuwa amehifadhiwa na ndugu au Jamaa na hakuna haki yake itakayopotea,” alibainisha.

Aidha, alishauri kuwa, wananchi wawapokee waathirika wa maporomoko ya mawe katika makazi yao na hata kama nyumba itakuwa haitoshi serikali itawezesha kujenga mahema ili waweze kujitosheleza.

Amefafanua zaidi kuwa lengo la serikali ni kuhakikisha vifaa vya msaada wa kibinadamu vinawafikia waathirika katika maeneo yao kwa kuhakikisha wanapata mahitaji muhimu ikiwemo chakula, magodoro pamoja na mablanketi.

“Sio kweli kwamba Muathirika wa maporomoko ya Mawe na Matope akienda kwa ndugu zile stahiki zake atakosa, cha msingi ni kuainisha eneo analokwenda kwa anuani, majina viongozi wake pamoja na mawasiliano yao,” amefafanua.

Kwa upande wake, Nyerere Izrael Mwenyeji wa kijiji cha Gendabi ameomba serikali kutuma wataalam kuangalia tabia za Mlima Hanang’ ili janga hilo lisije likajirudia.

“Wataalamu watasaidia kutupa taarifa za awali kama eneo ni salama au si salama kuendelea kuishi bila kuleta taharuki kwa wananchi,” amesema.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge na Uratibu), Jenista Mhagama akizungumza na Waathirika wa maafa ya maporomoko ya Mawe na Matope alipoenda kuwafariji na kuwapa pole.

Awali, Steven Sulle Mwenyekiti wa CCM Kata Gendabi, amemshaukuru, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan amesema ni rais wa kipekee kabisa ameonesha upendo na kutoa faraja katika madhila haya.

“Niipongeze serikali kwa kutukimbilia sisi tunawashukuru sana, ila nashauri wale waathirika wenye uwezo wa kwenda kwa ndugu, jamaa na marafiki watumie utaratibu uliopo na ni sahihi kuwapokea kwa upendo, tunavyoendelea kuwaacha katika eneo la Kambi, wataendelea kuwa wapweke zaidi,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles