31.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 20, 2024

Contact us: [email protected]

SAKATA LA MAFUTA YA KULA: SERIKALI YACHARUKA

Na GABRIEL MUSHI


WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema kuna mpango maalumu wa kuyumbisha Watanzania kuelekea kipindi hiki cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa wafanyabiashara kusababisha ukosefu wa bidhaa za mafuta ya kula na sukari nchini.

Pia amesema jambo hilo halitaachwa lipite kwa kuwa mafuta ya kula yapo na sukari ipo ya kutosha.

Majaliwa ametoa kauli hiyo bungeni jana wakati akitoa taarifa ya Serikali kuhusu utata wa hali ya upatikanaji wa mafuta ya kula nchini.

Utata huo ulisababisha Spika wa Bunge, Job Ndugai, juzi kumwagiza Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, kutoa taarifa ya Serikali juu ya hali hiyo.

Hali hiyo ilijitokeza kutokana na mzozo ambapo wafanyabiashara wanadai mafuta yaliyozuiliwa bandarini ni ghafi, huku Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), ikidai ni mafuta safi.

Akifafanua kuhusu hali hiyo, Majaliwa alisema kwa takwimu ambazo anazo, anawahakikishia Watanzania kwamba kusingekuwa na sababu ya kukosekana kwa mafuta ya kula nchini au kupanda bei ya bidhaa hiyo.

“Zile sababu waziri alizotoa kwamba wastani wa mafuta yanayotumika nchini kwa mwezi ni lita zisizozidi tani 28,000 na kila mwezi kuanzia Januari hadi Machi si chini ya tani 30,000 zilizoingizwa nchini.

“Kwa hiyo mafuta ya Januari hadi Machi ni zaidi ya tani 30,000, yalikuwa yanaweza kabisa kutumika mwezi Aprili wote na mafuta ya mwezi Mei ambayo yamepokelewa jana, leo yanaendelea kupokelewa zaidi ya tani 46,500 kusingekuwa na sababu hiyo ya kupungua kwa mafuta,” alisema.

Alisema itakumbukwa wiki iliyopita wakati wa maswali ya Papo kwa Hapo, alijibu swali hilo na kueleza kuwa imeundwa timu ya kufanya mapitio ya kero hiyo ambayo jana imepewa maelekezo na waziri ametoa maelezo ya Serikali.

“Jana nilikuwa napokea taarifa hii ya mwenendo wa mafuta yaliyoinghizwa nchini na upungufu uliopo wa mafuta na kwanini upo. Na kile kilichokuwa kinazungumzwa kwamba kuna mgongano wa taasisi zinazohakiki ubora, TBS (Shirika la Viwango), TFDA (Mamlaka ya Chakula na Dawa), Mkemia Mkuu wa Serikali na kwamba TRA anakataa takwimu zilizotolewa na taasisi hizo.

“Ni kweli kwamba taasisi hizo mzigo wote unapofika huwa wanajiridhisha baada ya kupokea nyaraka za nchi ulipotoka na ubora wake. Ndipo TRA wanapoendelea na taratibu za tozo na kadiri ya ubora na kuruhusu,” alisema na kuongeza;

“Jambo hili hatuwezi kukubaliana nalo tukaliacha hivi hivi kama lilivyo, kwa sababu upo mpango unaoonekana wa kutaka kuyumbisha Watanzania na hasa kipindi hiki ambacho Waislamu wanaelekea kwenye mfungo wa Ramadhan,” alisema.

Aidha, alitoa maelekezo kwa wafanyabiashara wanaohusika na mafuta ya kula na sukari, anahitaji sukari ya kutosha kwa kuwa Serikali imeweka utaratibu mzuri.

“Mafuta yapo, sukari pia ipo. Kama serikali tunatoa siku tatu, kuanzia kesho (leo) Alhamis, Ijumaa na Jumamosi, mafuta yote yaliyopo kwenye bohari yaondolewe ili yaendelee kupatikana nchini kote kwa sababu tunao uhakika yapo ili wananchi wasihangaike, yaliyopo bandarini tunaendelea na taratibu zake.

“Wenye matatizo tutaendelea kuzungumza nao. Kuanzia Jumapili tutalazimika kuingia kwenye maghala ili kuhakiki mafuta yapo au laa. kwa sababu shida tunawapa wananchi wetu bila sababu yoyote na kwa namna hiyo hatuwezi kuvumilia.

“Watanzania waelewe kuwa jambo hili halipo kwa bahati mbaya, nieleze kuwa mafuta tunayo na taratibu za kusambaza  tunatarajia kama kawaida kila eneo nchi litakuwa na mafuta kama kawaida, “ alisema.

 

Kwa habari zaidi jipatie nakala ya gazeti la MTANZANIA.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles