MWANDISHI WETU– DAR ES SALAAM
SERIKALI imesema kupanda kwa bei ya sukari kumesababishwa na waagizaji kushindwa kuagiza bidhaa hiyo kutokana na ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona (Covid-19).
Ilisema kuwa ilitoa vibali kwa viwanda vinne vya ndani kuagiza tani 40,000 za sukari kukabili upungufu uliopo na tayari zimeanza kuingizwa nchini.
Akizungumza jana, Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa, alisema sukari iliyokwishaingia bandarini kupitia Kampuni ya Kagera Sugar ni tani 9,990 na imeanza kutolewa tangu juzi jioni.
Alisema Aprili 24, 28 na 30 Kampuni ya Mtibwa Sugar itaingiza tani 10,000, Kilombero Sugar tani 1,624 kutoka Malawi na Msumbiji huku tani 1,800 zikiagizwa kutoka Afrika Kusini.
Bashungwa alisema wiki ya kwanza ya Mei, Kilombero Sugar itaingiza tani 7,276 na kwamba Mei 15 Kampuni ya TPC itaingiza tani 5,000 na Mei 30 tani 4,500 zitaingia nchini.
Alisema pia wizara inatarajia kuomba nyongeza ya tani 58,000 ili kukidhi mahitaji ya sukari kufikia Juni 2020.
“Kila mwaka Serikali imekuwa makini katika kutathmini mahitaji ya sukari kwa wananchi, kadhalika uwezo wa viwanda vya ndani katika uzalishaji, hivyo wananchi hawapaswi kuwa na wasiwasi,” alisema Bashungwa.
WAZIRI WA KILIMO
Naye Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga, akizungumza na MTANZANIA, alisema huenda sukari inayozalishwa ndani ikapungua kwa sababu ya changamoto ya mvua iliyosababisha baadhi ya viwanda kusimamisha uzalishaji. “Uwezo wa viwanda vya ndani ni kuzalisha tani 350,000 lakini mwaka huu huenda wasifikie kiwango hicho, tulikuwa na changamoto, mvua zimekuwa nyingi sana kwenye mashamba, zimezuia uzalishaji wa sukari kwa sababu imekuwa ni kazi kutoa miwa kwenye mashamba.
“Kwahiyo viwanda vingi vimesimamisha uzalishaji kabla ya ule muda, kimebakia tu Kagera Sugar ndiyo kinaendelea na uzalishaji mpaka muda huu,” alisema Hasunga.
Alisema wafanyabiashara hawapaswi kupandisha bei kwa sababu wameshaagiza sukari ya kutosha na kuonya kuwa watakaobainika kupandisha bei watachukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kufungiwa biashara na kunyang’anywa leseni.
BEI YA SUKARI MTAANI
Uchunguzi wa MTANZANIA ulibaini bei ya sukari katika baadhi ya maeneo imeongezeka kwa kati ya Sh 200 na 2,500 kulingana na eneo husika.
Mkazi wa Mtaa wa Amani uliopo Kata ya Buza, Manispaa ya Temeke, Najma Fadhili, alisema bei imepanda kutoka Sh 2,600 hadi Sh 3,200 kwa kilo.
Mkazi wa Mbezi kwa Msuguri, Ramadhani Juma, alisema awali alikuwa akinunua kilo moja kwa Sh 2,500 lakini hivi sasa imepanda hadi Sh 4,500.
“Kuna baadhi ya maduka ukienda wanakuambia ile ambayo iko kwenye mifuko ya Kilombero kilo Sh 3,500 na ile ya kupima kawaida Sh 4,500 hadi Sh 5,000,” alisema Juma.
Katika duka la Godfrey Tarimo lililopo Sinza, sukari haikuwapo kwa siku mbili na ilipopatikana iliuzwa Sh 4,000 kwa kilo moja.
Muuzaji wa jumla katika Mtaa wa Aggrey, Mussa Hassan, alisema kupata sukari imekuwa ni mtihani mkubwa na kwamba inawalazimu kuamka mapema kwenda kupanga foleni.
“Foleni ya kupata sukari ni kubwa pale kwa Zacharia (Wakala), bila kuamka mapema hupati, ndiyo maana hapa umekuta sukari leo,” alisema Hassan.
Mkoani Morogoro, mmoja wa wafanyabiashara wa vyakula, Hosiana Ngowo, alisema awali alikuwa akinunua mfuko wa kilo 25 kwa Sh 64,000 lakini hivi sasa umepanda hadi Sh 68,000.
WAKALA
Gazeti hili pia lilifika katika duka la Wakala wa Sukari, Haroun Zacharia, lililopo mtaa Aggrey na kukuta foleni kubwa ya watu wanaosubiri kulipia ili wakachukue stoo.
Watu waliokuwapo walisukumana kwa nguvu geti la kwanza la duka hilo kutokana na kuhisi kucheleweshewa huduma na kuingia, lakini walizuiwa katika geti la pili na la tatu.
Mmoja wa wanunuzi, Mohamed Khatibu, alisema kwa sasa wananunua sukari kwa Sh 135,000 kwa mfuko wa kilo 50, huku mfuko wa kilo 25 ukinunuliwa hadi Sh 73,000.
“Hadi sasa hatujui sababu ya kupanda kwa bei ya sukari kiasi hiki japo wenyewe wanasema viwanda vinafanyiwa ukarabati,” alisema Khatibu.
VIWANDA VYA SUKARI
Meneja wa Kiwanda cha Sukari cha TPC, Jafari Ali, alisema wamesitisha uzalishaji tangu Machi 13 mwaka huu na kwamba mauzo walimaliza Machi 30.
“Kifupi ni kwamba sukari tumesimama uzalishaji na bei ya mwisho kwa mfuko wa kilo 50 ilikuwa Sh 109,408 ikijumuishwa na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT),” alisema Ali.
Alisema vibali vya kuagiza sukari vilitoka Machi 17 mwaka huu, tani 10,000 kwa kila mzalishaji sawa na tani 40,000 kwa wote na kwamba tayari imeanza kuingia bandarini.
“Msimu ujao tunatarajia kuanza uzalishaji Juni 17, mwaka huu na hakuna sababu za wafanyabiashara kupandisha bei kwa walaji kwani wameuziwa sukari na wazalishaji kwa bei ile ile waliyouziwa toka Desemba hadi mwishoni mwa Machi 2020,” alisema Ali.
Alisema ni utaratibu wa kawaida kusimama uzalishaji wakati wa masika kwani hawawezi kuvuna miwa shambani, matrekta huwa yanazama.
“Hivyo huwa tunachukua muda huo kufanya matengenezo ya kiwanda hadi masika yapite,” alisema Ali.
HABARI HII IMEANDALIWA NA NORA DAMIAN, CHRISTINA GAULUHANGA NA TUNU NASSOR (DAR ES SALAAM)