Na Waandishi Wetu-Dar/Mwanza
Sakata la tuhuma za rushwa ya ngono Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), limeendelea kuwasha moto baada ya Kamati ya Maadili ya chuo hicho (CKD), kukutana na Mhadhiri Mwandamizi Dk. Vicensia Shule aliyeibua tuhuma hizo mapema wiki hii.
Hatua hiyo ni kama imechochea moto mwingine baada ya jana Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Mwanza kukiri kumuhoji Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT) (jina tunalihifadhi kwa sababu za maadili) kwa tuhuma za kuhusika na rushwa ya ngono kwa wanafunzi wake.
Taarifa za Dk. Shule kukutana na Kamati hiyo ya maadili zilithibitishwa jana jioni na Mwenyekiti wake, Profesa Evelyne Mbede.
Akizungumza na MTANZANIA Jumamosi, Profesa Mbede alisema wao kama Kamati inayojishughulisha na masuala yote yanayohusu maadili walikutana na Dk. Shule kwa nia ya kutaka awapatie taarifa juu ya tuhuma alizoziibua za kuwako kwa rushwa ya ngono UDSM.
Profesa Mbede alisema Dk. Shule amewaeleza kuwa suala hilo amekwishalifikisha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
“Tumekutana naye …amesema kesi zote amezituma Takukuru, sasa tukawa hatuna cha kufanya, tunajua watazifanyia kazi”.
Kabla Profesa Mbede hajazungumza na gazeti hili, Dk. Shule tayari alikuwa ametafutwa na alieleza kuwa kamati hiyo haikumwita kumuhoji bali kujadiliana naye jinsi ya kudhibiti suala hilo.
Alisema aliombwa na kamati hiyo kutoa mtazamo wake wa namna ya kudhibiti suala hilo.
Alipoulizwa iwapo aliombwa ushahidi wowote juu ya tuhuma alizoziibua, Dk. Shule alisema hakuombwa.
MTANZANIA Jumamosi liliwasiliana na Takukuru kupitia kwa Msemaji wake, Doreen Kapwani ambaye alisema hadi anaondoka jioni suala hilo lililikuwa bado halijawafikia na kwamba atalifuatilia.
Hatua zote hizo zimekuja ikiwa ni siku moja imepita tangu serikali ilipotangaza kuingilia kati ili kupata ukweli wa suala hilo.
Awali jana kabla kamati haijaketi, Dk. Shule aliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa Twitter kuwa; juzi jioni alipigiwa simu kujulishwa kuitwa kwenye kamati ya hiyo.
“My good people, a quick update. Leo (juzi) Alhamisi 29 Nov jioni nimepigiwa simu kuitwa kwenye kamati ya maadili siku ya Ijumaa 30 Nov mchana. Nasubiri mwaliko rasmi kwa maandishi. For our deal sexual violence survivor, we are almost there, we will win, big time.”
Andiko hilo la Dk. Shule lilitanguliwa na barua ya wito huo iliyosainiwa na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Profesa Mbede ambayo ilianza kusambaa mapema jana asubuhi.
Barua hiyo ilieleza kuwa dhumuni la wito huo kwa Dk. Shule ni kupata ushirikiano zaidi kuhusu sakata hilo.
Barua hiyo yenye kichwa cha habari, ‘Taarifa ya rushwa ya ngono Chuo Kikuu cha Dar es Salaam’ yenye kumbukumbu Na. GY//MBD/2018-23 iliandikwa juzi Alhamisi.
“Rejea kichwa cha barua hapo juu. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kupitia akaunti yako ya kijamii ya Twitter kimepokea taarifa kama ulivyoandika kuwa rushwa ya ngono imekithiri mno hapa chuoni.”
“Kwa barua hii Kamati ya Maadili ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam inakuagiza ufike kwenye kikao cha kamati kitakachofanyika kesho (jana) Novemba 30, 2018 saa tisa mchana ili kamati iweze kulifanyia kazi suala hili kwa haraka,” inasomeka barua hiyo
Kutokana na mwenendo huo, kabla kamati hiyo haijaketi jana saa tisa alasili MTANZANIA Jumamosi liliwasiliana na Profesa Mbede ambaye alisema kamati hiyo inataka kuzungumza na mhadhiri huyo ili awasadie kupatikana kwa wahusika waliotenda au kutendewa vitendo hivyo vya rushwa ya ngono kabla ya kuchukua zaidi.
“Sisi hatumhoji kwa sababu hii si kamati ya nidhamu, ni kamati ya maadili ya chuo… huwa tunapokea malalamiko yoyote yenye ‘element’ za rushwa, tumeunda mkakati wa kudhibiti rushwa.
“Tukiyapokea malalamiko hayo tunashughulikia, tukikuta yana ‘element’ za nidhamu tunapeleka kamati ya nidhamu, kama ya rushwa tunapeleka kwenye vyombo husika.
“Kwa hiyo sisi hatumhoji kuhusu rushwa, tunataka atusaidie, kwa sababu ukisema kuna rushwa ya ngono kama hujapata wahusika tunaweza kuendelea hivi tu, hatutaweza kufika mahali ambapo tutachukua hatua,” alisema.
Aidha, alisema kamati hiyo imekuwa ikipokea malalamiko mbalimbali ikiwamo ya rushwa na kuyafanyia kazi kwa mujibu wa taratibu.
Mhadhiri wa SAUT ahojiwa
Wakati hayo yakijiri UDSM, Mhadhiri wa SAUT alikamatwa na kuhojiwa na Takukuru, Mkoa wa Mwanza kwa tuhuma za kuhusika na rushwa ya ngono kwa wanafunzi wake.
Taarifa kutoka chuoni hapo ambazo zimehibitishwa na Naibu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mwanza, Emmanuel Stenga zilieleza kuwa mhadhiri huyo ambaye hufundisha somo la Project Appraisal alikamatwa Novemba 28, mwaka huu na kushikiliwa kwa saa kadhaa kwa mahojiano na kuachiwa kwa dhamana siku iliyofuata.
“Tunafanya kazi kwa sheria, hivyo hairuhusiwi kutoa taarifa zaidi kwa sasa hivyo naomba niishie hapo lakini tukakapokamilisha uchungizi huu na kuwa kwenye hatua za kulitolea taarifa tutawaeleza, lakini itoshe kusema tulimkamata mhadhiri huyo (anamtaja jina) ambaye alilamikiwa kwa kujihusisha na vitendo vya rushwa ya ngono,” alieleza.
Aidha taarifa kutoka Takukuru zimebainisha kuwa simu ya mhadhiri huyo inashikiliwa kwa ajili ya uchunguzi zaidi kutokana na kuwapo kwa tuhuma kuwa alikuwa akiitumia kuwaandikia ujumbe mfupi wanafunzi hao ambao anatuhumiwa kuwaomba ngono na kumgomea.
Taarifa kutoka chuoni hapo zilieleza kuwa hadi sasa wanafunzi wawili ndiyo waliojitokeza kueleza wazi namna ambavyo wamekuwa wakinyanyaswa na mhadhiri huyo kwa kuombwa rushwa ya ngono na wamekuwa wakifelishwa somo lake baada ya kukataa kumtimizia haja zake.
Nondo abainisha ukubwa wa tatizo
Akizungumzia suala hilo, Mwenyekiti mstaafu wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP), Abdul Nondo alisema alisema hali ni mbaya kwa wanafunzi huko vyuoni na kusisitiza kuwa amewasiliana na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako na kumshauri kuunda tume ya kuchunguza jambo hilo.
Zaidi ameshauri kuandaliwa kwa chombo ambacho kitakuwa kikisimamia maadili ya wahadhiri.
“Tunazungumzia mwanafunzi mmoja aliyepata ujasiri na kulieleza hili wazi na hata kujitokeza Takukuru na kuonyesha ushahidi wa jambo hilo, lakini hali ni mbaya wapo wanafunzi wengi wanasumbulia na mambo haya, wasichana na hata wavulana,” alisema.
Nondo alisema kwa taarifa za haraka alizonazo yeye chuo cha SAUT Mwanza wapo wanafunzi zaidi ya wawili na kubainisha katika Chuo Kikuu cha Tumaini Iringa tayari Mhadhiri mwingine naye alishtakiwa kwa kuhusika na rushwa ya ngono na kesi yake ipo mahakamani.
Alisema yupo mwanafunzi ambaye alipaswa kumaliza mwaka 2017 akiwa chini ya mhadhiri huyo wa somo la Project Appraisal lakini kutokana na kumkatalia ngono alifelishwa makusudi.
Alisema hata aliporudia tena alifelishwa hivyo atalazimika kurudia tena mwaka 2019 somo hilo.
WAJA JUU DK. SHULE KUHOJIWA
Uamuzi wa Dk Shule kuitwa na Kamati ya Maadili UDSM, umewaibua wanaharakati mbalimbali kikiwamo Chama cha ACT Wazalendo ambao walihoji dhumuni nyuma ya barua hiyo ya wito, zaidi wakiapa kusimama pamoja na Dk. Shule kukemea vitendo hivyo.
Kwa upande wao wanaharakati wameungana kupaza sauti pamoja na Dk. Shule kupinga vitendo vya ngono katika Taasisi ya Elimu ya Juu wakisema inadhalilisha, kuua na kuzalisha watendaji wasioweza kazi.
Akizungumza katika mkutano uliandaliwa kwa pamoja na Mtandao wa Jinsia (TGNP), Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Sauti ya Jamii Kipunguni, Kituo cha Taarifa na Maarifa Mabibo, Mfuko wa Wanawake Tanzania na taasisi zingine zinazopinga vitendo hivyo, Mwana Mtandao, Janeth Mawinza alisema baada ya Dk. Shule kutoa taarifa ya rushwa ya ngono UDSM amekuwa akidhalilishwa katika mitandao ya kijamii.
“Tunakemea vitendo vya udhalilishaji, usiku Novemba 29, Dk Shule aliandika katika ukurasa wake wa Twitter kuwa jana ameitwa na kamati ya maadili kuhojiwa kuhusu suala hili.
Janeth alisema katika kipindi cha kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia ikiwemo rushwa ya ngono wanaunganisha sauti zao na sauti ya Dk. shule kwa kauli mbiu ya ‘Vunja ukimya rushwa ya ngono inadhalilisha na kuua.
MWANAFUNZI WAFUNGUKA
Akichangia mwanafunzi, Neema Mbise alisema vitendo hivyo vipo na vinasababisha wanafunzi kufeli na wengine kufaulu kwa sababu ya kukubali kutoa rushwa ya ngono.
Mbise aliishauri serikali kuweka simu au barua pepe (e-mail) ambayo watafikisha taarifa hizo kwa siri ili kuwakomboa wanawake.
Mwanafunzi wa Chuo cha Utumishi ,Lilian Mhagama alisema rushwa ya ngono ifike kikomo inakwamisha juhudi za Serikali kufikia Tanzania ya viwanda kwa kupata watendaji wasioweza kazi.
A
SAKATA LILIVYOANZA
Tuhuma hizo za ngono UDSM zilibuliwa Novemba 28 mwaka huu na Dk. Shule kupitia akaunti yake ya mtandao wa Twitter na kuonekana kutikisa taasisi hiyo.
Katika akaunti yake ya Twitter, Dk. Shule alindika; “Baba MagufuliJP (Rais John Magufuli) umeingia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kufungua maktaba ya kisasa. Rushwa ya ngono imekithiri mno UDSM.
“Nilitamani nikupokee kwa bango langu ila ulinzi wako umenifanya ninyamaze. Nasubiri kusikia toka kwako maana naamini wateule wako ni waadilifu watakwambia ukweli”.
Habari hii imeandaliwa na GABRIEL MUSHI Na KULWA MZEE (DAR ES SALAAM )
FREDRICK KATULANDA (MWANZA)