LAS VEGAS, MAREKANI
BINGWA wa mchezo wa judo na ngumi nchini Marekani kwa upande wa wanawake, Ronda Rousey, amedai kuwa siku za hivi karibuni anaweza kuweka wazi kama ataendelea kuutumikia mchezo huo au kustaafu.
Mwanamichezo huyo mwenye umri wa miaka 29, alichezea kichapo na mpinzani wake, Amanda Nunes, Desemba 31 mwaka jana na kumaliza mwaka kwa kichapo.
Nyota huyo alikuwa na wakati mgumu katika mchezo huo baada ya kukaa nje kwa miezi 13 kutokana na utovu wa nidhamu ambao aliuonesha na kufungiwa kwa muda.
Katika pambano hilo alijikuta akitumia sekunde 48 kumaliza mchezo huo baada ya kuchezea kichapo na mpinzani wake na kuweka historia mpya ya pambano ambalo lilifunga mwaka kwa kutumia muda mfupi sana.
Kutokana na hali hiyo, Ronda amedai kuwa anafikiria kutaka kutangaza mwelekeo wa maisha yake ya ngumi, kama atakuwa tayari kuendelea au kutangaza kustaafu.
“Naanza kwa kuwashukuru mashabiki wangu wote ambao walijitokeza katika pambano langu la funga mwaka ambalo lilikuwa ngumu katika historia ya maisha yangu ndani ya mchezo huo.
“Siwezi kusema jinsi gani nimejisikia kutokana na uwepo wenu katika pambano langu, napenda kusema nawashukuru sana.
“Nilivyopanga kurudi ulingoni nilikuwa na maana ya kushinda pambano na si kupoteza kama ilivyotokea, ni kweli unaweza kujiandaa kwa kiasi kikubwa lakini ukajikuta unapoteza pambano lenyewe ikawa tofauti na vile ambavyo umepanga.
“Lakini nimekuwa na furaha kubwa ya kuwa msichana ambaye naweza kuwakilisha katika mchezo huu, ila nachukua nafasi hii kusema kwamba natarajia kufanya maamuzi juu ya uwezo wangu katika mchezo huu, naweza kutangaza kustaafu au kuendelea, asanteni kwa kunielewa,” alisema Ronda.