28.4 C
Dar es Salaam
Thursday, February 22, 2024

Contact us: [email protected]

TUNA WAJIBU WA KULINDA HAKI ZA WENYE ULEMAVU

NA CLARA MATIMO- MWANZA


walemavuKATIKA kuhakikisha watu wenye ulemavu wanaishi pasipo kubaguliwa ama kunyanyaswa, Serikali iliona ipo haja ya kutunga sheria ambayo itawalinda watu hawa.

Sheria ya watu wenye ulemavu namba 9 ya mwaka 2010 ilitungwa ili kusimamia  haki zao katika nyanja zote ikiwemo elimu, afya, ajira na jinsi ya kuzifikia  huduma mbalimbali kupitia mawasiliano na miundombinu.

Sheria hii inatoa mwongozo wa kisheria na kumtaka waziri mwenye dhamana ya kusimamia haki za watu wenye ulemavu  ashirikiane na waziri wa majengo ili kuhakikisha  kila jengo la  umma na majengo mengine yanayotoa huduma kwa umma yanafikika na kupitika kwa urahisi  kwa watu wote wenye ulemavu.

Lakini pamoja na kuwa na sheria hii bado nimeshuhudia baadhi ya majengo ambayo yanatoa huduma za umma kama shule, hospitali na ofisi za watendaji wa kata zikiwa hazijaweka mazingira rafiki kwa watu wenye ulemavu.

Si majengo tu ambayo hayazingatii mwongozo huo uliotolewa katika sheria hiyo, hata baadhi ya madaraja na vivuko vya watembea kwa miguu barabarani navyo havina mazingira rafiki kwa wenzetu wenye ulemavu.

Daraja la watembea kwa miguu la mabatini hapa jijini Mwanza, tangu lianze kutumika ni ukweli usiopingika kwamba limepunguza ajali ambazo zilikuwa zikitokea mara kwa mara lakini nasikitika kwa sababu halina tija kwa watu wenye ulemavu wa viungo vya miguu maana hawawezi kulitumia hasa wale ambao wanatembea kwa kutumia baiskeli.

Hivi sasa kuna ujenzi unaoendelea wa daraja la Furahisha, natarajia kuona Serikali hii ambayo ni sikivu  na isiyopenda kuvunja sheria inatekeleza mwongozo huo uliotolewa katika sheria  ya watu wenye ulemavu namba 9 ya mwaka 2010 kwa kuweka mazingira rafiki kwa watu wenye ulemavu ili litakapokamilika na wao wafurahie uwepo wake.

Mbali na madaraja lakini pia ingekuwa vyema kama Serikali ingesimamia majengo yote yanayotoa huduma za umma ambayo hayajatekeleza agizo na maelekezo ya sheria hiyo ya kuweka mazingira yanayopitika kwa watu wenye ulemavu yarekebishwe ili watu wenye ulemavu waweze kuzifikia huduma zinazotolewa kwenye majengo hayo kwa urahisi.

Hata kwenye vivuko vya watembea kwa miguu barabarani (zebra) navyo vinawanyanyapaa watu wenye ulemavu kwa sababu havimpi nafasi mtu mwenye ulemavu wa kutoona kujua kwamba wakati wa watembea kwa miguu umefika ili avuke barabara.

Nilitegemea hata kwenye zebra ingewekwa mifumo ambayo ingewawezesha watu wenye ulemavu wa kutoona kujua kwamba ishara fulani ikisikika wajue ni muda wao wa kuvuka barabara.

Naamini unyanyapaa huu ndio uliosababisha Chama cha Watu Wenye Ulemavu Tanzania (Chawata) Wilaya ya Ilemela, kutekeleza mradi wa kuelimisha watu wenye ulemavu na jamii kuhusu haki za watu wenye ulemavu katika kata tano zilizomo ndani ya wilaya hiyo  wakiamini utasaidia kuboresha maisha ya watu wenye ulemavu kwa kupatiwa haki zao za msingi.

Kutokana na hali hii, naiomba Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dk. John Magufuli ambayo ni sikivu, kupitia kwa Waziri mwenye dhamana kwa kushirikiana na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, wasimamie kikamilifu sheria hii ili ndugu zetu wenye ulemavu na wao wafurahie maisha bora kupitia uongozi wa awamu ya tano.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles