26.9 C
Dar es Salaam
Monday, December 9, 2024

Contact us: [email protected]

MAKOCHA WASIINGILIWE MAJUKUMU YAO

yangaMCHEZO wa soka ni moja kati ya michezo inayopendwa zaidi duniani kote na kadiri miaka inavyozidi kwenda wachezaji wengi wenye vipaji wamekuwa wakiibuliwa na kuonyesha uwezo mkubwa.

Walimu wanaowalea wachezaji tangu wakiwa wadogo katika vituo vya kukuza na kuendeleza vipaji pamoja na makocha wanaowafundisha wanapocheza katika timu mbalimbali wanatakiwa kupewa pongezi kutokana na kazi kubwa wanayoifanya.

Kwa hapa nchini tumeshuhudia klabu nyingi ambazo zinashiriki katika michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara zikiajiri makocha wa kigeni ili waweze kuimarisha vikosi vyao na kuziwezesha klabu zao kupata mafanikio.

Sisi MTANZANIA tunaamini kama makocha wa kigeni pamoja na wazawa waliopewa majukumu ya kufundisha timu mbalimbali watapewa ushirikiano na kupewa uhuru wa kufanya kazi zao bila kuingiliwa itakuwa rahisi kwao kufikia malengo.

Inafahamika kwamba kila mara baada ya kusimama au kumalizika kwa ligi, makocha huandaa ripoti zao na kutoa mapendekezo yao kulingana na maboresho wanayotaka yafanyike kwenye timu kulingana na mapungufu aliyoyaona.

Huu ni wakati wa mabadiliko katika soka hivyo tunaamini viongozi wa klabu za Ligi Kuu watabadilika na kuacha kuwaingilia makocha kwenye majukumu yao na kukubali kuyafanyia kazi mapendekezo wanayotoa.

Mara nyingi makocha hutoa mapendekezo yao kwa kupendekeza majina ya wachezaji wanaotaka wasajiliwe ili kuboresha kikosi na kukiimarisha zaidi ili kuondokana na mapungufu yaliyojitokeza.

MTANZANIA tunaamini kwa sasa viongozi wa klabu wataacha tabia ya kuwaingilia makocha na kuwaacha wafanye kazi na majukumu yao kwa uhuru kwa kuwa hiyo ni taaluma ambayo wameisomea, ndio maana wana uwezo wa kumsoma kila mchezaji na kujua anaweza kumtumia vipi kulingana na kipaji chake.

Si vizuri kwa viongozi kuingilia mambo ya kiufundi ambayo hawajasomea kwani hali hiyo inaweza kusababisha matatizo makubwa na kupelekea timu kufanya vibaya kwenye mashindano.

Mwaka uliopita tulishuhudia makocha wengi wakilalamikia tabia ya viongozi kuingilia majukumu yao kwa kuwapangia vikosi na kuwachagulia wachezaji watakaosajiliwa wakati hawana taaluma yoyote na matokeo yake ni timu kufanya vibaya.

Kocha yeyote anayeajiriwa lazima atapenda timu yake ifanye vizuri katika mashindano wanayoshiriki ili kufikia malengo, hivyo ni vyema wanavyowasilisha mapendekezo yao kulingana na mahitaji ya timu wakasikilizwa mawazo yao na kufanyiwa kazi.

Viongozi wanapofanya usajili bila kuwahusisha kocha mara nyingi timu hukutana na changamoto katikati ya ligi jambo ambalo linawapa wakati mgumu sana makocha wanaozifundisha.

Kwa sasa tunaamini viongozi wa klabu waliokuwa na tabia ya kung’ang’ania majukumu yasiyowahusu ndani ya timu bila kuwashirikisha makocha watabadilika ili kuiwezesha timu kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Viongozi wakifanya kazi za kuendesha klabu na kuzipatia mafanikio na makocha wakiachwa waendelee na majukumu yao, tatizo hili linaweza kupungua au kuisha kabisa hapa nchini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles