25.7 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 20, 2024

Contact us: [email protected]

RONALDO, MESSI KUMSAFISHIA NYOTA HAZARD URUSI

MOSCOW, URUSI

 

WINGA wa timu ya taifa ya Ubelgiji, Eden Hazard, ameahidi kuwa nyota wa michuano ya Kombe la Dunia inayoendelea nchini Urusi baada ya nyota wa Argentina, Lionel Messi na Ureno, Cristiano Ronaldo kuondolewa Jumamosi katika hatua ya 16.

Timu ya Argentina iliondolewa katika michuano hiyo na Ufaransa, baada ya kufungwa mabao 4-3 huku Ureno ikifungwa mabao 2-1 na Uruguay.

Ubelgiji jana ilitarajia kuvaana na Japan katika Uwanja wa Rostov, Urusi  kutafuta tiketi ya kufuzu hatua ya robo fainali ya michuano hiyo na Hazard anaamini timu hiyo inayo nafasi ya kutwaa ubingwa.

Kikosi cha Ubelgiji ambacho kinatambulika kama kizazi cha dhahabu, hakikufanya vizuri katika michuano ya Euro mwaka 2016, baada ya kupoteza dhidi ya Wales, pia kilionyesha kiwango cha chini katika michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2014 nchini Brazil.

Lakini kikosi hicho ambacho kiliongoza kufumania nyavu hatua ya makundi, kimepewa nafasi kubwa ya kupenya hatua inayofuata  na huenda ikavaana na Brazil endapo itapenya dhidi ya Colombia katika mchezo ambao ulitarajia kuchezwa jana mapema.

“Ndio, nina matumaini ya kuwa nyota  katika michuano hii, Messi na Ronaldo hawapo hivyo ni wakati wangu wa  kung’aa. Nahitaji kufuzu hatua inayofuata, pia nusu fainali na pengine hata hatua ya fainali,” alisema Hazard.

“Mimi sipo peke yangu. Messi na Ronaldo hawapo sasa, lakini wapo wachezaji wengine wazuri katika michuano hii. Tutaona hadi mwisho itakuwaje.”

Hazard anahisi kuondoka kwa nyota hao atakuwa katika nafasi nzuri ya kuonyesha uwezo wake ndani ya uwanja.

“Nipo imara zaidi ya miaka miwili iliyopita au miaka minne  wakati tunacheza michuano ya Kombe la Dunia nchini Brazil,” alisema Hazard na kuongeza kwamba kwa sasa ana uzoefu wa kutosha.

“Miaka minne iliyopita wachezaji wote wa Ubelgiji ilikuwa mara ya kwanza kucheza michuano mikubwa kama hii. Kuondolewa ilikuwa funzo kubwa kwetu,” alisema Hazard.

“Ukiwa na kikosi kilichosheheni vijana ni jambo linalosumbua hata kama wakiwa na vipaji. Kwa sasa miongoni mwetu tuna miaka kati ya 25 na 30, hivyo tupo katika nafasi nzuri na jambo hili linaweza kuleta utofauti.”

Hazard amefunga mabao mawili katika michuano hiyo nchini Urusi, lakini mchezaji mwenzake anayekipiga katika timu ya Manchester United, Romelu Lukaku, amefunga mabao manne na muunganiko wake na Dries Mertens  umekuwa na mafanikio katika kikosi cha Ubelgiji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles