Na JUSTIN DAMIAN
KWA mara ya kwanza katika historia, uchimbaji madini ya dhahabu na shaba unatarajia kufanyika kwenye kina kirefu chini ya bahari ifikapo mwaka 2019.
Kwa mujibu wa Kampuni ya Nautilus Minerals Inc ya nchini Canada, uchimbaji huo utakaofanyika kwenye pwani ya nchi ya Papua New Guine ambayo inaelezewa kuwa na utajiri mkubwa wa madini hayo, utafanywa kwa kutumia roboti ambaye anaendeshwa na rimoti.
Roboti hao ambao mdogo ana uzito wa tani 200, watakuwa na uwezo wa kuvunja miamba iliyopo chini ya bahari na kutoa madini.
Watu wengi hawafahamu kuwa chini ya bahari kuna madini mengi kuliko hata ardhini. Tatizo limekuwa ni namna ya kuyachimba, tunashukuru teknalojia kwa kutuwezesha kufanya uchimbaji huu wa aina yake,” anasema Michael Johnston ambaye ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Nautilus.
Mikataba mingi imetolewa kufanya utafiti wa madini yaliyopo baharini sehemu ambazo bahari haipo kwenye eneo la nchi yoyote imetolewa na shirika la linalojulikana kama International Seabed Authority (ISA), ambalo lipo chini ya Umoja wa Mataifa
Chini ya bahati, kuna utajiri mkubwa wa madini ambayo yana ubora wa hali ya juu na ni mengi mno,” anasema Michael Lodge ambaye ni Katibu Mkuu wa shirika hilo.
Kampuni ya Nautilus inasema majaribio tayari yameshafanyika na upatikanaji wa madini ya shaba katika eneo hilo chini ya bahari ni mara kumi zaidi ya yale yanayopatikana ardhini huku ubora wa midini hayo ukiwa mara saba zaidi ya yanayopatikana ardhini.
Roboti watakaofanya kazi ya uchimbaji wametengenezwa kuweza kufanya kazi kwenye mazingira ya baridi ambayo inakadiriwa ni baridi inayoweza kugandisha huku presha ikiwa mara 150 zaidi ya iliyopo kwenye usawa wa bahari.
Roboti wa kwanza atakuwa akifanya kazi ya kuvunja vunja miamba ili kuwezesha roboti wa poili ambaye ni maalumu kwa ajili ya kusaga na kuchambua madini yatakayokuwapo kwenye miamba hiyo.
Roboti wa tatu, ambaye kazi yake ni kama mashine ya kukusanya atakuwa nyuma ya watangulizi wawili ambapo kazi yake itakuwa kuchukua madini ambayo yamechanganyikana na udongo kidogo wa miamba na kupeleka juu ya bahari ambako kuna meli.
Meli hiyo itakuwa na mitambo maalumu ya kuchambua na kupata madini safi. Mabaki ya udongo yanarudishwa baharini huku madini safi yakisafirishwa moja kwa moja kwenda sokoni nchini China.
Hata hivyo, uchimbaji huo unakabiliwa na vikwazo kutoka kwa wanamazingira ambao wanasema bado hujafanyika utafiti wa kutosha kuonyesha kama hautakuwa na athari kwa mazingira ya bahari pamoja na viumbe wake.
Kuna mambo mengi ambayo hayafahamiki juu ya uchimbaji wa madini chini ya bahari,” anasema Natalie Lowrey ambaye ni mwanamazingira wa nchni Australia anayependekeza zoezi la uchimbaji madini baharini usitishwe.
“Tumeharibu kiasi kikubwa cha ardhi kwa sababu ya uchimbaji madini si jambo jema kuharibu na mazingira ya baharini,” anasema
Lowrey anasema miamba itakayokuwa inavunjwa na roboti wakati wa uchimbaji inaweza kusafiri na mawimbi na kuharibu ekolojia ya baharini ikiwa ni pamoja na keleta madhara kwa viumbe waishio majini.
“Kuna tishio kubwa pia uchimbaji huo unaweza kusababisha madhara kwa binadamu wanaotegemea vitoweo kama samaki kutoka baharini kwa ajili ya chakula kwa jamii zinanazoishi katika pwani ya Papua New Guinea,” anasema.
Hata hivyo, Kampuni ya Nautilus inachukulia suala la mabaki ya miamba kwa umakini mkubwa na kuongeza kuwa mashine za uchimbaji zimetengenezwa kwa kuzingatia suala hilo.
Wakati Nautilus ikijiandaa kwa ajili ya uchimbaji huo wa aina yake, kampuni nyingine za madini zimekuwa zikifuatilia kwa ukaribu maendeleo ya mradi huo na kama itafanikiwa inatarajiwa makampuni mengine yatafuata.
“Kama Nautilus ikiendelea vyema na zoezi lake hili, itakuwa imefungua dirisha jipya katika sekta hii,” anasema Lowrey.