26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

TUNAYOPASWA KUYAFAHAMU KUHUSU SHULE ZA MSINGI ZA BWENI

Na CHRISTIAN BWAYA


MAKALA Iliyopita, tuliangazia mambo mawili ya kuzingatia unapoamua kumpeleka mwanao mwenye umri mdogo kwenda shule za bweni. Tulitazama namna ilivyo muhimu kujiridhisha na ubora wa malezi na huduma kwa ujumla.

Malezi yanakuwa bora pale mtoto anapopata mlezi mwenye upendo unaomfanya ajisikie wajibu wa kufuatilia maendeleo yake kwa karibu. Shule inalazimika kuwa na walezi wa kutosha ili waweze kuwa na nafasi ya kuwaangalia watoto wachache.

Makala haya yanaendelea kujadili mambo mengine mawili ya kuzingatiwa unapofanya uamuzi wa kumpeleka mwanao kwenye shule za bweni.

 

Mawasialiano na mtoto

Mtoto anahitaji mawasiliano ya karibu na mzazi wake. Ukaribu unamhakikishia usalama wake na hivyo anakuwa na utulivu wa nafsi. Unapompeleka mtoto mbali na mazingira ya nyumbani anaweza kuumia kihisia hata kama hatakuwa na ujasiri wa kusema.

Umbali wa kimwili hutengeneza umbali wa kihisia (upweke) unaoweza kuathiri kwa kiasi kikubwa namna anavyojiona na anavyowachukulia wengine. Kwa mfano unapowauliza watoto wa darasa la pili kama wanahitaji kuoanana na wazazi wao, wengi wanakwambia, ‘kukaa na wazazi huo ni utoto.’

Majibu kama hayo yanaonesha kuwa mtoto anakuwa amejenga mtazamo hasi na uhusiano ya karibu na wazazi wake ili tu kulinda furaha yake. Mtoto wa namna hii anajaribu kumpotezea mzazi hata kama ni kweli anamhitaji. Hali hii inaweza kuzaa matatizo ya kitabia kadri anavyokua.

Ili kukabiliana na hali hii, usimtelekeze mtoto shuleni. Tengeneza utaratibu wa kuwasiliana naye mara kwa mara ili kumhakikishia kuwa bado mtoto ana nafasi muhimu kwenye maisha yako. Mpigie simu kwa utaratibu uliowekwa shuleni kumjulia hali yake. Anajisikia kuwa karibu na wewe.

Sambamba na hilo, jiwekee utaratibu wa kumtembelea mara kwa mara kadri nafasi yako inavyoruhusu. Unapomtembelea jaribu kuwasiliana na moyo wake. Mfanye akuamini na ajue unaaminika. Ukifanya hivyo, atakuwa tayari kukushirikisha mambo anayokutana nayo.

 

Kushiriki kazi za mikono

Shule nyingi za bweni zinamnyima mtoto fursa ya kushiriki kazi za mikono. Watoto hawafanyi kazi zozote zaidi ya kusoma na kujihusisha na shughuli nyingine za kitaaluma. Tumeona kuwa utaratibu huu hauna tija kwa maendeleo ya jumla ya mtoto.

Upo ukweli kuwa matarajio ya wazazi yanaweza kuwa chanzo cha utaratibu huu. Wazazi wanatarajia kuona mtoto anafanya vizuri kitaaluma hata ikibidi kwa gharama ya maeneo mengine ya kimakuzi. Hata katika mazingira ya nyumbani wazazi wengi hawapendi kuona watoto wao wakishiriki kazi za mikono. Mtazamo huu unapalilia changamoto mpya ya watoto kushindwa kujifunza stadi za maisha.

Unahitaji kubadilisha mtazamo wako. Mruhusu mwanao kushiriki kazi za mikono ajifunze stadi ndogo ndogo za maisha. Omba mtoto afundishwe kazi za mikono kama kufua nguo nyepesi soksi, kuoga, kutandika kitanda, kufanya usafi wa mahali anapoishi, kuosha vyombo anavyovitumia na shughuli kama hizi. Hakikisha mtoto anachukulia kazi za mikono kama sehemu muhimu ya maisha yake ya kila siku.

Epuka shule zinazomwondolea mtoto wajibu wa kushiriki kazi za mikono hata kama zinamfanya achangamke kitaaluma. Usifurahie shule bora zinazohakikisha mtoto ametandikiwa kitanda, amefuliwa nguo, amesafishiwa vyombo alivyovitumia kwa chakula na hata kumsafishia maeneo anayoishi. Shule za namna hii hazimfai mwanao.

Itaendelea…

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles