27 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

Ripoti ya CAG yaanika udhaifu vyama vya siasa

MAREGESI PAUL -DODOMA

MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad, ameeleza jinsi alivyogundua kasoro zilizoko katika uendeshaji wa vyama vya siasa nchini.

Profesa Assad alieleza kasoro hizo mjini hapa jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari juu ya kilichomo katika ripoti ya ukaguzi wa hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha 2017/18.

Katika maelezo yake, Profesa Assad alivitaja vyama viwili vya siasa, Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kueleza kasoro za kihasibu zilizomo katika vyama hivyo.

Akizungumzia Chadema, Profesa Assad alisema kilinunua gari aina ya Nissan Patrol kwa Dola za Marekani 63,720 (Sh milioni 147.76) kwa matumizi ya chama hicho.

Badala yake, Profesa Assad alisema gari hilo lilisajiliwa kwa jina la mwanachama badala ya Bodi ya Wadhamini ya Chadema.

“Gari hilo pia lilionyeshwa kwenye taarifa za fedha za chama kama mkopo kwa mwanachama huyo bila kuwapo makubaliano ya mkopo yaliyosainiwa kati ya mwanachama na Bodi ya Wadhamini ya Chadema,” alisema Profesa Assad.

CHAMA CHA MAPINDUZI

Akizungumzia CCM, Profesa Assad alisema ukaguzi ulionesha chama hicho hakikuwasilisha michango ya kila mwezi kwenda kwenye Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).

Alisema kwamba hadi kufikia Mei 2018, chama hicho kilikuwa na deni la Sh bilioni 3.74 ambalo linajumuisha adhabu ya Sh bilioni 2.73 iliyotokana na ucheleweshaji wa uwasilishaji wa michango hiyo.

“Aidha, ukaguzi ulibaini kwamba kuna tatizo la uendelevu wa biashara katika Kampuni ya Uchapishaji ya Uhuru inayomilikiwa na CCM.

“Pia hati za ardhi za nyumba 199 zinazomilikiwa na CCM Zanzibar, zilionekana hazijasajiliwa kwa jina la Bodi ya Wadhamini bali zimesajiliwa kwa majina ya maofisa wa chama.

“Pamoja na hayo, vyama saba vya siasa vilifanya matumizi ya jumla ya shilingi milioni 777.91 bila ya kuwa na nyaraka toshelevu na hivyo nilishindwa kuthibitisha iwapo malipo hayo yalikuwa halali,” alisema Profesa Assad.

Alivitaja vyama vilivyofanya matumizi bila kuwa na nyaraka toshelevu kuwa ni CCM, Chadema, Chaumma, UMD, SAU, AAFP na CCK.

Kutokana na hali hiyo, alipendekeza vyama vya siasa vihakikishe udhibiti unaanzishwa na kuimarishwa hasa kwenye malipo ili yanapofanyika yawe na vielelezo na nyaraka toshelezi zikiwamo risiti za kielektroniki.

MASHIRIKA YENYE HALI MBAYA

Profesa Assad pia alitaja mashirika ya umma yenye hali mbaya kifedha.

 “Katika ukaguzi wangu nilibaini kuwapo kwa mashirika ya umma 14 yenye matatizo makubwa ya kifedha pamoja na kupata hasara hadi kusababisha madeni kuwa zaidi ya mitaji yao kwa zaidi ya asilimia 100.

“Kati ya mashirika hayo, mashirika 11 yana hali ukwasi hasi kwa maana ya kujiendesha kwa hasara kwa zaidi ya miaka miwili sasa.

“Kutokana na hali hiyo, ni wazi kwamba mashirika hayo hayawezi kujiendesha bila kutegemea msaada kutoka Serikali Kuu. Hivyo basi, kuna hatari mashirika hayo yakashindwa kuendelea kutoa huduma kwa jamii,” alisema Profesa Assad.

Aliyataja mashirika hayo kuwa ni Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Lindi, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Bodi ya Utalii Tanzania na Shirika la Maji na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASCO).

Mengine ni Kampuni ya Maendeleo ya Nishati na Joto Tanzania (TGDC), Baraza la Taifa la Biashara, Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mtwara, Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mwanza, Kampuni ya Usafirishaji na Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usambazaji wa Umeme, Kampuni ya Simu (TTCL Pesa), Bodi ya Maziwa Tanzania na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA).

UDHAIFU USIMAMIZI MAPATO MASHIRIKA YA UMMA

Profesa Assad alisema ukaguzi wake ulionesha uwepo wa udhaifu katika ufuatiliaji wa marejesho ya Sh trilioni 1.46 cha mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu.

Alisema kwamba Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) imeshindwa kufahamu walipo wakopaji wa mikopo ya elimu ya juu yenye thamani hiyo ya fedha, japokuwa fedha hizo ni nyingi.

“Pamoja na uwepo wa tatizo hilo, kifungu cha 4 (h) cha sheria ya bodi, kinaitaka bodi kutengeneza mtandao wa kushirikiana na taasisi na mashirika mbalimbali ili kuwatambua wadaiwa na kuwezesha kupata marejesho ya mikopo hiyo.

ONGEZEKO MADENI ELIMU YA JUU

Akizungumzia ongezeko la madeni ya wafanyakazi katika taasisi za elimu ya juu, Profesa Assad alisema kuanzia mwaka wa fedha 2016/17 hadi 2017/18, madeni yanayohusiana na malipo ya posho ya majukumu kwa wahadhiri wa vyuo vikuu vya Mzumbe na Ardhi yameongezeka.

“Katika Chuo cha Kikuu Mzumbe, madeni yameongezeka kutoka Sh bilioni 1.49 hadi Sh bilioni 3.41 na kwa Chuo Kikuu cha Ardhi madeni yameongezeka kutoka Sh bilioni 1.48 hadi Sh bilioni 2.26.

“Aidha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Mzumbe, vilikuwa na madeni ya kiinua mgongo cha Sh bilioni 5.59 na Sh milioni 525 za wafanyakazi waliomaliza mikataba yao.

“Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine kilikuwa na madeni ya Sh bilioni 6.78 ambazo ni za posho za nyumba na madeni mengineyo ya wafanyakazi kuanzia Juni 2017.

“Kwahiyo, hali hiyo inaweza kusababisha kushuka kwa kiwango cha elimu ya juu kutokana na wahadhiri kukosa moyo wa kufanya kazi,” alisema.

SERIKALI KUTOCHANGIA MIRADI

Profesa Assad pia alisema Serikali imekuwa haichangii ipasavyo kwenye miradi ya maendeleo inayotakiwa kuchangia.

Kutokana na hali hiyo, amesema baadhi ya miradi inayotekelezwa imekuwa ikichelewa kukamilika kutokana na ukosefu wa fedha.

“Ukaguzi wangu wa miradi mbalimbali kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, mwaka 2018, ulibaini kuwa miradi 10 ambayo Serikali ilitakiwa kuchangia kiasi cha Sh bilioni 118.44, ilichangia Sh bilioni 7.43 ambazo ni sawa na asilimia sita tu.

“Kwahiyo, hali hiyo ilisababisha upungufu wa kiasi cha Sh bilioni 111.01 kinyume na makubaliano na wadau wa maendeleo.

“Hivyo basi, kitendo cha Serikali kushindwa kuchangia miradi hiyo, kwa kiasi kikubwa kumeathiri utekelezaji wa miradi husika na kudhoofisha juhudi za kufikia malengo yaliyokusudiwa,” alisema.

WAKALA WA NISHATI VIJIJINI

Katika ukaguzi wa miradi ya nishati, Profesa Assad alisema walibaini Wakala wa Nishati Vijijini (REA), ilipanga kusambaza umeme katika vijiji 12,268 kuanzia mwaka 2013 hadi 2021.

“Hata hivyo, hadi kufikia Juni 2018, mradi huo ulikuwa umefikisha umeme katika vijiji 4,395, sawa na asilimia 36 kwa kipindi cha miaka mitano.

“Kwahiyo, hali hiyo inaondoa uwezekano wa kufikia lengo la kusambaza umeme kwenye vijiji 7,873 vilivyobaki katika kipindi cha miaka mitatu iliyobaki hadi kufikia 2021,” alisema.

DAMPO KIGOMA

Pamoja na hayo, Profesa Assad alizungumzia mradi wa dampo lililotengenezwa kwa thmani ya Sh bilioni 2.96 lililoko Ujiji Kigoma.

Alisema kwamba baada ya kukagua mradi huo, aligundua mradi huo licha ya kugharimu kiasi kikubwa cha fedha, bado haujaanza kutumika baada ya shule ya msingi kujengwa jirani na mradi huo.

Kwa mujibu wa Profesa Assad, dampo hilo halijaanza kutumika kutokana na kuhofia afya za wanafunzi pamoja na uwepo wa hofu ya uharibifu wa mazingira katika eneo hilo.

Akitoa ushauri katika maeneo hayo, Profesa Assad alitaka Serikali ianzishe ofisi itakayokuwa na jukumu la kuratibu utekelezaji wa miradi yote ikiwamo ya maendeleo nchini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles