PARIS, Ufaransa
RIPOTI mpya ya Waandishi Wasio na Mipaka (RSF) imeitaja China kuendelea kuwa kwenye orodha ya nchi ambazo waandishi wa habari wake wanafanya kazi kwenye mazingira magumu zaidi duniani.
Ripoti ya RSF imeiweka China katika nafasi ya 177 kati ya nchi 180, ikiwa imeachwa nafasi mbili tu na Korea ya Kaskazini.
Kwa mujibu wa ripoti ya taasisi hiyo, waandishi takribani 127 wanashikiliwa na vyombo vya usalama hadi sasa, ikiwa ni sehemu ya kampeni kabambe ya China kuikandamiza taaluma hiyo.
Ikitolea mfano Jimbo la Wuhan, ripoti imedai waandishi na wachambuzi wanaotajwa kufikia 10, akiwamo mwanasheria Zhang Zhan, wameshaingia matatizoni kwa kuripoti juu ya janga la Corona.
Zhan aliingia kwenye misukosuko baada ya kuitembelea Wuhan mwanzoni mwa mwaka jana na kisha kuanza kuripoti kwa mtindo wa makala hali mbaya aliyoiona mitaani na hospitalini wakati wa Corona.