26.2 C
Dar es Salaam
Sunday, April 2, 2023

Contact us: [email protected]

RC Kunenge atoa mwezi mmoja kwa wavamizi wa shamba la mitiamba kulipa gharama

Na Gustafu Haule, Pwani

MKUU wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge, ametoa muda wa mwezi mmoja kwa wananchi waliovamia shamba la Wizara ya Mifugo na Uvuvi lililopo katika Halmashauri ya Mji wa Kibaha kuhakikisha wanalipa fedha kwa haraka kwa ajili ya kupimiwa maeneo hayo ili waweze kumiliki kisheria.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge,akisoma taarifa ya msimamo wa Serikali kwa wananchi waliovamia shamba la Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mitamba) lililopo Kibaha Mjini.

Kunenge ametoa agizo hilo Februari 2, 2023 katika mkutano wake na wananchi wa eneo la Lumumba, Mkombozi na Kidimu ambapo kwa pamoja yanaunda Kata ya Pangani ambapo lengo lake ni kutoa msimamo wa Serikali kuhusu wavamizi hao.

Kunenge amesema shamba hilo linalojulikana kwa jina maarufu la Mitamba linamilikiwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi likiwa na ukubwa wa hekta 4000 lakini wananchi hao walilivamia na kuanza kujenga bila kufuata sheria.

Aidha , Kunenge amesema kuwa shamba la Mitamba lilianza miaka ya 1982 na 1983 likiwa chini ya Wizara ya Mifugo na lengo lake lilikuwa ni kutoa mafunzo na uzalishaji wa Mitamba lakini wakati linaanzishwa kulikuwa na wakazi 1,557 ambao walilipwa fidia yenye thamani ya Sh milioni 20.

Amesema baada ya kulipa fidia hizo hukajitokeza uvamizi wa watu kujenga na wengine kufanya maendeleo bila ya kufuata sheria na hivyo kufanya uvamizi  mkubwa na ndipo Serikali ngazi ya Wilaya na Mkoa kuiomba ridhaa Wizara husika ili waweze kupewa eneo hilo.

Kunenge, ameongeza kuwa kutokana na hali hiyo Wizara kupitia Katibu Mkuu aliandika barua ya kuridhia kutoa eneo la ukubwa wa hekta 2,963 na kulikabidhi katika Halmashauri ya Mji wa Kibaha kwa ajili ya makazi na mipango mingine ya maendeleo.

Amesema kuwa baada ya Wizara kutoa eneo hilo na kulikabidhi katika Halmashauri ya Mji wa Kibaha kwasasa Wizara imebakiwa na eneo lenye ukubwa wa hekta 1,037 Kitalu namba 34 ambalo halitakiwa kuguswa na mtu yeyote na kwamba wanaohusika na maamuzi ya kulipa gharama ni wale waliokuwa katika ndani ya eneo la 2,963 lililotolewa na Wizara.

“Machi 7,2012 Wizara ilikabidhi hekta 2,963 kwa Halmashauri na sio kwa mtu mwingine na nyinyi mlivamia tu lakini Serikali imekaa na kuona kunahitaji la kuwasaidia wananchi wake lakini mnatakiwa kulipa gharama ili muweze kumilikishwa kisheria,” amesema Kunenge.

Kunenge amesema kuwa kisheria wananchi hao walitakiwa kulipa kulingana na bei ya soko lililopo hivi sasa lakini kutokana na huruma ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan kiwango hicho kimeshuka kutoka mita ya mraba 6,000 mpaka 1,500 na kila mwananchi atapewa mita za mraba 2,500 kwa ajili ya makazi.

Amesema fedha hizo zinatakiwa kulipwa katika kipindi cha mwezi mmoja na anayemaliza anapewa hati miliki yake na kwa yule ambaye atashindwa kufuata maelekezo hayo ataondolewa na kiwanja chake atapewa mtu mwingine.

“Rais Samia amekuwa na huruma kwa wananchi wake ndio maana hata bei mliotakiwa kulipa imeshuka ili kuwasaidia watu wachini na wale wasiojiweza kabisa watasaidiwa kupitia mpango wa Tasaf,”amesema Kunenge

Amesema kuwa,kwa wale ambao watahitaji eneo kubwa zaidi watapaswa kununua kwa bei ya soko ambayo ni Sh 6,000 kwakuwa mahitaji yao ni zaidi ya makazi huku akiwashauri Wananchi hao kutumia fursa hiyo kikamilifu.

Amesema kuwa ,hasitokee mtu wa kuwadanganya kuacha kulipa viwango vilivyopangwa na Serikali kwakuwa watakuwa wanapoteza muda na kusema hasiyetaka kulipa aondoke mwenyewe.

Hatahivyo, Kunenge amesema pamoja na hayo lakini bado ataendelea kufanya oparesheni ya kuwakamata wale wote waliowatapeli wananchi kwa kuwauzia maeneo kinyume na utaratibu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,405FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles