Na Mwandishi Wetu, RUKWA
MKUU wa Mkoa wa Rukwa, Zelote Stephen amekutana na wadhibiti ubora wa shule wa halmashauri nne za mkoa huo kujua changamoto wanazokumbana nazo na mambo yanayosababisha kushuka kiwango cha elimu.
Stephen alifikia uamuzi huo baada ya mkoa wake kushuka katika elimu kutoka nafasi ya 6 mwaka 2015 hadi nafasi ya 12 kati ya mikoa 31 mwaka 2016 katika mtihani wa kidato cha nne.
Pia mkoa huo umeshuka katika mitihani ya kidato cha pili kutoka nafasi ya 20 kwa mwaka 2015 hadi nafasi ya 21 mwaka 2016.
Wadhibiti hao walielezea sababu nyingi zilizosababisha kushuka kiwango cha elimu, mojawapo ikiwa ni kutopewa mrejesho wa taarifa za kila wiki wanazoziandika na kukabidhi kwa wakurugenzi wa halmashauri na wakuu wa wilaya.
“Tangu Julai, mwaka jana tumeshaandika ripoti nyingi tu zinazoelezea upungufu kama vile walimu kwa baadhi ya masomo, matundu ya vyoo na vitabu vya kusomea,”alisema Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Goreth Ntulo.
Alisema sababu nyingine zinazokwamisha ufanisi wa kazi za wadhibiti hao ni kutopewa motisha na mwajiri wao na kusababisha waishi katika maisha magumu.
“Mimi sijawahi kwenda likizo kwa fedha ya Serikali tangu nianze kufanya kazi, na madaraja hatupandishwi…hata ukipandishwa linabaki jina tu… mshahara upo pale pale,”alisema mmoja wa wadhibiti hao.
Akijibu hoja hizo, RC Stephen aliwaagiza wakurugenzi wote kuhakikisha wadhibiti hao wanapatiwa mrejesho juu ya kasoro walizozibaini baada ya kufanya ukaguzi katika shule zao.
Mmoja wa wadhibiti hao, Pracida Rwegasira alisema amefurahishwa na uamuzi wa kuitwa kutoa mchango wao utakaosaidia kuinua kiwango cha elimu mkoani humo.