26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 20, 2024

Contact us: [email protected]

RAIS MAGUFULI: KILA MTU ATABEBA MSALABA WAKE

Rais Dk John Magufuli, akizungumza na mkazi wa Bukoba, Charles Masinde jana aliyeamua kujenga nyumba yake mwenyewe baada ya kubomoka kutokana na tetemeko la ardhi lilitokea mwaka jana.
Rais Dk John Magufuli, akizungumza na mkazi wa Bukoba, Charles Masinde jana aliyeamua kujenga
nyumba yake mwenyewe baada ya kubomoka kutokana na tetemeko la ardhi lilitokea mwaka jana.

Na ASHA BANI Dar na Renatha Kipaka,

HATIMAYE Rais Dk. John Magufuli, amepigilia msumari wa mwisho kwa wakazi zaidi ya 200 wa Mkoa wa Kagera waliokumbwa na tetemeko la ardhi Septemba  mwaka jana, baada ya kusema kila mtu atabeba msalaba wake.

Amesema kutokana na hali hiyo, Serikali haitamjengea nyumba mtu yeyote aliyeathirika na tetemeko hilo kwa sababu si jukumu lake.

Rais Dk. Magufuli, aliyasema hayo jana wakati akizungumza na wananchi katika Shule ya Sekondari Ihungo mjini Bukoba, ikiwa ni mara ya kwanza tangu kutokea maafa ya tetemeko la ardhi lililosababisha vifo vya watu 17, kubomoa nyumba na  kuharibiwa miundombinu.

Rais Dk. Magufuli, alisema watu wote ambao nyumba zao ziliharibika, wanatakiwa kujenga wenyewe kwa sababu hakuna sehemu yoyote duniani ambako Serikali inabeba jukumu la kuwajengea nyumba waathirika wa maafa kama hayo.

“Kuna nchi kama Japan na Italia, zimekuwa zikikumbwa na matetemeko mengi, haijawahi kutokea Serikali yao ikawajengea nyumba upya ispokuwa inarejesha miundombinu ya taasisi za umma kama vituo vya afya, shule na barabara.

“Mwaka jana nilipokuwa naomba kura kwenu, sikuomba tetemeko la ardhi litokee hapa, hili ni jambo  ambalo liko nje ya uwezo wangu, tunaomba kila mmoja aweze kutumia msaada uliotolewa ili kurejesha miundombinu ya makazi yenu.

“Wapo wanasiasa ambao watainuka  na kuanza kuwadanganya eti Serikali  itawajengea nyumba, hilo halipo kama wanaona wanajiweza  wawejengee wenyewe,”alisema.

Rais Magufuli, alisema anashangazwa na kitendo cha baadhi ya wananchi wa Kagera kudai tetemeko limesababisha njaa ambapo aliwahoji kama mazao yao yakiwamo migomba ilipandwa kwenye nyumba.

Alisema  muda huu, ni wakati wa kufanya kazi kwa bidii ikiwa ni pamoja na  kulima mazao ya biashara kama maharage, nyanya, mchicha na matikiti maji.

“Serikali na wananchi kila mmoja abebe msalaba wake mwenyewe,’’ alisema Rais Dk. Magufuli.

Alisema anawashangaa wengine baada ya kusikia serikali inakuja kuwajengea nyumba zao zilizokuwa zimebomoka kidogo wakaongezea kuzivunja zote , hivyo wasitarajie fadhila hiyo.

Baada ya wakazi hao kukumbwa na tetemeko la ardhi, wahisani, balozi na taasisi za serikali na zisizo za kiserikali walijitokeza kuchanga zaidi ya Sh bilioni 5.4 kwa ajili kusaidia waathirika hao.

Katika hatua nyingine, Rais Dk. Magufuli alisema  pasitokee mtu akasema Serikali itagawa chakula cha msaada kwa kuwa ardhi ya Kagera ni kija kibichi, hivyo watu wanapaswa kulima.

Huku akitoa maelekezo kwa Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Deodatus Kinawilo kuwa hakuna chakula na Serikali haina chakula wala hawana shamba la Serikali kwa sababu mvua imenyesha kila mtu anatakiwa kulima.

‘’Lazima niwaeleze ukweli kwa kuwa msema kweli ni mpenzi wa Mungu, mvua zimenyesha watu tufanye kazi ,Serikali tusimamie yale mahitaji muhimu kwa Watanzania,tutengeneze reli, tujenge hospitali ,tununue dawa ,tununue ndege ,tulete umeme,’’alisema rais Magufuli.

SHULE

Katika hatua nyingine, Rais Dk. Magufuli ameinyang’anya Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Shule ya Sekondari ya Omumwani  na kuirudisha serikalini.

Ilielezwa shule hiyo, iliyonzishwa mwaka 1966   hadi mwaka jana, ilikuwa na wanafunzi 85 pekee,baada ya wanafunzi 35 kuhitimu kidato cha nne mwaka jana, imebaki na  wananfunzi 50 na walimu wanne.

‘’Waziri wa Elimu Profesa Ndalichako yupo hapa, ahakikishe  masuala yote pamoja na madai ambayo shule wanadaiwa na jumuiya ya wazazi yalipwe na shule irudi mikononi mwa serikali,’’ alisema Rais Magufuli.

Alisema  walimu na wanafunzi watabakia hapo hapo na watakuwa ni wa Serikali, wawe wameshindwa  au kushinda mitihani yao.

“Hapa ukarabati unaendelea katika shule hii, taarifa nilizozipata ni kwamba  majengo ya Shule ya Omumwani yametumia Sh milioni 172, nyinyi  mnaniletea taarifa  mmetumia Sh  milioni 116 jambo ambalo sikubaliani nalo.

“Naagiza Kamati ya Maafa Ofisi ya Waziri  Mkuu na Kamati ya Maafa Mkoa wa Kagera, kufuatilia hatua kwa hatua ili kujua kila shilingi imefanya nini,”alisema Rais Dk.  Magufuli.

Pia aliiagiza Kamati ya Maafa ya Mkoa huo na  wadau mbalimbali waliokuwa wameahidi kutoa msaada wa waathirika wa tetemeko hilo kutoa misaada yao ili kufikia mwisho wa jambo hilo.

Alitoa wito kwa mtu au mfadhili ambaye anataka kutoa msaada wake,  anatakiwa kupeleka moja kwa moja katika jamii husika  kupitia kwa watendaji, huku akimtaka Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali mstaafu Salimu Kijuu kuendelea kusimamia shughuli za maendeleo.

Baadae  Rais Dk. Maguful, alitembelea maeneo mbalimbali  kujionea athari za tetemeko hilo.

Tetemeko la ardhi lilitokea Septemba 10,mwaka jana na kusababisha  vifo vya watu 17, nyumba 840 kuanguka na nyingine 1,264 kupata nyufa, yakiwamo majengo 44 ya taasisi mbalimbali za umma.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles