26 C
Dar es Salaam
Monday, March 4, 2024

Contact us: [email protected]

UMEME WAWAIBUA WASOMI, WANASIASA

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Felichesmi Mramba.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Felichesmi Mramba.

Na WAANDISHI WETU- DAR ES SALAAM

SIKU moja baada ya Rais Dk. John Magufuli kutengua uteuzi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Felichesmi Mramba, wasomi na wanasiasa wameibuka na kuzungumzia suala hilo.

Wadau hao kwa nyakati tofauti jana walitoa maoni yao, huku baadhi yao wakikosoa utaratibu uliotumika kutengua uteuzi wa Mramba na wengine wakisifu hatua ya Serikali kugomea uamuzi wa Mamlaka ya Nishati na Maji (Ewura) kupandisha bei ya umeme kwa asilimia 8.5 wakati huu ambao Serikali inahubiri sera ya uchumi wa viwanda.

Katika maoni hayo pia wameonyesha wasiwasi wao juu ya uimara wa Menejimenti ya Tanesco, Bodi na uhusiano wa taasisi za Serikali na wizara ambapo walishauri kuondolewa  mikanganyiko katika mabadiliko ya kisera na kuimarisha mifumo ya kisasa ya utendaji kazi.

Wachambuzi wengine waliiambia MTANZANIA kuwa sakata zima la kupanda kwa gharama za umeme na hatua zilizochukuliwa dhidi ya Mramba halijakaa sawasawa huku wengine wakisema suala hilo linahitaji mjadala wa kitaifa.

Profesa Semboja

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Haji Semboja alisema kutenguliwa kwa mkurugenzi huyo kunatia shaka kwamba hakukuwa na mawasiliano mazuri kati ya Wizara ya Nishati na Madini na taasisi yake mama (Tanesco).

Alisema jambo linaloshangaza na kuacha maswali kwa wengi ni jinsi mchakato wa kupandisha bei hiyo ulivyofanywa kwa uwazi na kushirikisha wadau wa umeme ambao walipewa nafasi ya kutoa maoni yao lakini mwisho wizara ikazuia.

“Wakati mchakato unaanza wadau walipewa nafasi ya kutoa maoni yao, yalikusanywa na kwenda kujadiliwa, sasa labda Tanesco watuambie kama Serikali haikukubali wazo hilo la kupandisha bei,” alisema.

Alisema hakuna asiyefahamu matatizo yaliyopo ndani ya shirika hilo kwani si mara ya kwanza kumekuwa na haja ya kuomba kupandisha gharama za umeme ili liweze kujiendesha kwa sababu ya mzigo mkubwa walionao.

“Tunajua serikali ya sasa imeweka malengo makubwa na madogo, imelenga kuipeleka nchi katika uchumi wa viwanda, hivyo umuhimu wa umeme wa uhakika na wa bei nafuu unahitajika ili wawekezaji waweze kumudu gharama za kuendesha viwanda.

“Kwa hiyo katika hili naweza kusema huenda Rais Magufuli aliona anapotezewa malengo yake, wakati akihamasisha wawekezaji wazawa wa ndani na wa nje kumiliki viwanda” alisema Profesa Semboja.

Profesa Mpangala

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ruaha (RUCO), Profesa Gaudence Mpangala alisema suala hilo limegawanyika katika pande mbili, uhalisia wa bei za umeme za Tanesco na mfumo mzima wa utawala.

“Bei walizopendekeza Tanesco binafsi sikuzifurahia hata kidogo kwani zilikuwa zinakwenda kuongeza ugumu wa maisha kwa wananchi, naipongeza Serikali kwa hatua yake ya kuzikataa.

“Lakini kwa upande wa kiutawala, naona kuna walakini, suala kama hilo angelimaliza waziri mwenye dhamana na Ewura kwa sababu wana mamlaka hayo kisheria lakini hatua ya Rais Dk. Magufuli kuingilia, kutimua na kuteua hapo hapo si sahihi,” alisema.

Alisema ili kujenga uchumi mzuri wa nchi ni lazima kuwepo na ushirikishwaji ambapo mamlaka ya juu inazipa uwezo wa kufanya maamuzi mamlaka za chini.

“Mamlaka za chini zinashindwa kutoa maamuzi ndipo zinalazimika kisheria kufuata ngazi za juu ili zitoe maamuzi, sasa kama Rais anatoa uamuzi yeye mwenyewe moja kwa moja, atafanya mangapi,” alihoji.

Aliongeza. “Waziri na Ewura walikuwa na uwezo wa kulimaliza suala hilo na iwapo ingeshindikana ingefuatwa ngazi ya Waziri Mkuu.

“Kama huko nako ingeshindikana ndipo wangeenda kwa Rais lakini si hivyo ilivyofanyika si jambo zuri kiutawala. Ni vema mamlaka za chini ziachwe zifanye kazi yake. Hali hii inatia wasiwasi kwamba huenda wengine wanaondolewa kwa haki na wengine si kwa haki.

“Wapo watakaotimuliwa lakini kumbe hawana hatia, mamlaka za chini zikiachwa zifanye kazi yake ni rahisi kubaini na pengine adhabu anayostahili mtumishi husika si kubwa kama inavyotolewa wakati huo na au labda angestahili onyo tu,” alisema.

Profesa Mpangala alisema ni kweli Tanesco hupanga bei kisheria na Ewura hujadili na bodi huamua kiwango baada ya kupitia maoni ya wadau.

“Lakini baada ya kuafiki bei, Ewura walipaswa kumwambia waziri husika waliyokubaliana kama hawakumwambia basi Ewura waliteleza katika hilo,” alisema Profesa Mpangala.

 Dk Onesmo

Mhadhiri Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Onesmo Kyauke alisema uamuzi huo umetolewa kisiasa.

“Suala la bei ya umeme ni siasa uchwara. Kuna wakati wanasiasa wanakuwa kama watoto, wanasema bei ya umeme haitapanda ili tuone kuwa serikali inawatetea wananchi kitu ambacho si kweli,” alisema.

Mtatiro

Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi wa Chama cha Wananchi (CUF), Julius Mtatiro alisema Tanesco inajiendesha kwa hasara kubwa kutokana na madeni na mikataba mibovu iliyolizingira shirika hilo.

Alisema Serikali haijawahi kuchukua hatua madhubuti za kuliimarisha shirika hilo ili liwe la mfano katika utendaji na uzalishaji wenye faida na tija kwa taifa.

“Kwa hiyo Tanesco imekuwa ikitegemea wateja wake ili kujikwamua kwa kila kitu jambo linaloifanya kuwa mzigo kwa watumiaji wa umeme na wala si serikali. Kila uamuzi utakaofanywa na serikali juu ya Tanesco wanaoathirika na uamuzi huo ni wananchi,” alisema.

Mtatiro alipongeza uamuzi uliofanywa na Waziri Profesa Muhongo wa kuzuia bei mpya za umeme zisianze kutumika kwani ongezeko hilo la asilimia 8.5 zilikuwa mzigo kwa wananchi wa kawaida na si serikali.

“Kinachoshangaza zuio la waziri limekuja dakika za mwisho za utekelezaji wa jambo ambalo limefanywa kwa mchakato wa wazi na ambao umeshuhudiwa na kubarikiwa na serikali yenyewe.

“Kuna mtu katumbuliwa, ametumbuliwa kosa lake nini? Je ni kufuata mchakato wa kisheria na kikanuni na kupandisha bei ya umeme?

“Kama serikali ilikuwa na nia njema kwa nini haikuizuia Ewura na Tanesco mapema, zisiendelee na hatua za namna hiyo? Kwa nini wasubiriwe wafanye uamuzi wa kisheria ndipo Mkurugenzi wa Tanesco afukuzwe? Hivi kweli tatizo la Tanesco ni mtu au ni taasisi?,” alihoji Mtatiro.

Zitto

Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo) alipinga ongezeko la gharama za umeme, uonevu na kuvunjwa sheria huku akihoji mamlaka ya Waziri wa Nishati juu ya Ewura.

“Waziri kwenye tamko lake kataja sheria ya umeme ya mwaka 2008 ( nilishiriki kuitunga neno kwa neno wakati William Mganga Ngeleja ni Waziri na William Shelukindo mkt wa Kamati). Naomba kusaidiwa kifungu cha Sheria alichotumia Waziri. Kifungu mahususi na si jumla jumla tu,” alisema.

Habari hii imeandaliwa na Christina Gauluhanga na Veronica Romwald- Dar es Salaam

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles