26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 20, 2024

Contact us: [email protected]

RAIS KENYATTA KUFUNGUA KESI YA KUPITIA HUKUMU UPYA

NAIROBI, KENYA

WANASHERIA wa Rais, Uhuru Kenyatta, wamepanga kufungua kesi kutaka kupitiwa upya kwa uamuzi wa Mahakama ya Juu wa kufuta ushindi wake katika uchaguzi wa Agosti 8, gazeti la Sunday Standard limebainisha.

Vyanzo vya habari vya uhakika vilivyo karibu na Rais vimesema kwamba uamuzi huo umepitishwa na chama chake cha Jubilee, huku wanasheria wake wakijifungia kushughulikia ukataji huo wa rufaa.

Katikati ya maombi hayo ya kutaka kupitiwa upya, Jubilee inataka maboksi ya kura yafunguliwe na kuhesabiwa upya hadharani.

Hoja ya wanasheria hao pamoja na mambo mengine imeegemea katika amri ya Mahakama ya Juu kuwa masanduku ya kura yabakie yalivyo na hivyo uamuzi wa Mahakama ya Juu ulitokana na kushindwa kazi kwa mfumo wa usambazaji matokeo, kitu ambacho inaona kinatosha kufungua kesi hiyo.

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Jubilee (JP), David Murathe alisema shauri la kupitia hukumu upya litafunguliwa rasmi wiki ijayo likilenga masanduku kufunguliwa na kura kuhesabiwa upya.

“Kitu cha kwanza nitakacho kuambia ni kwamba tuko tayari kwa uchaguzi mpya. Lakini ni wazi washindani wetu hawako tayari kwa uchaguzi mwingine. Kwa sababu Mahakama ya Juu ilisema tatizo lilikuwa katika usambazaji wa matokeo, tunataka matakwa ya watu kama yalivyojieleza katika Uchaguzi wa Agosti 8 yahalalishwe na hakuna hitaji la kurudia uchaguzi,” alisema.

Mwelekeo huo mpya unaozidisha sintofahamu ya kisiasa nchini hapa unakuja huku muungano wa upinzani wa NASA ukisisitiza kutoshiriki uchaguzi wa marudio wa Oktoba 26 iwapo hakutakuwa na mabadiliko katika sekretariati ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Wakati huo huo, Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Serikali nchini Kenya, Keriako Tobiko ameiamrisha polisi na kitengo cha kukabiliana na rushwa kuichunguza IEBC kutokana na tuhuma za ukiukwaji wa taratibu katika usimamizi wa uchaguzi wa rais uliobatilishwa.

Tobiko amesema uchunguzi mpana dhidi ya IEBC unapaswa kukamilika ndani ya siku 21.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles