PARIS, UFARANSA
MKURUGENZI wa klabu ya Paris Saint Germain, Luis Fernandez, amesisitiza kuwa uongozi wa timu hiyo haupo kwenye mipango yoyote ya kuwaacha wachezaji wao, Neymar na Kylian Mbappe waondoke katika kipindi hiki cha majira ya joto.
Neymar ambaye alishindwa kulipigania taifa lake la Brazil kwenye michuano ya Kombe la Dunia nchini Urusi, ametajwa kuwindwa na klabu ya mabingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, Real Madrid kwa madai kuwa hana furaha ndani ya PSG.
Hata hivyo, Madrid walionesha nia ya kuitaka saini ya Mbappe tangu majira ya baridi, lakini PSG wakamchukua mchezaji huyo kwa mkopo kabla ya kudaiwa PSG kumpa mkataba wa kudumu.
Madrid wanawinda saini za wachezaji hao katika kipindi hiki cha majira ya joto ili kuweza kuziba nafasi ya Cristiano Ronaldo ambaye amejiunga na Juventus.
“Neymar tayari alifanya maamuzi ya kuendelea kubaki Paris Saint-Germain, lengo lake kubwa ni kuhakikisha anapata mafanikio makubwa akiwa hapa baada ya kushindwa kufanya vizuri akiwa na Brazil kwenye michuano ya Kombe la Dunia, hivyo kwa sasa anataka kutwaa ubingwa wakiwa na PSG.
“Kwa upande mwingine, Mbappe na yeye ataendelea kuwa hapa, aliwahi kusema hivyo kwa asilimia 100 anataka kuwa hapa kwa ajili ya kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, hivyo sina wasiwasi na kitu muhimu ni wachezaji hao kuendelea kubaki,” alisema Fernandez.