31.2 C
Dar es Salaam
Saturday, May 18, 2024

Contact us: [email protected]

PONDA AHOJIWA POLISI KWA SAA SITA

AGATHA CHARLES Na LEONARD MANG’OHA, DAR ES SALAAM

KATIBU wa Jumuiya ya Kiislamu na Msemaji wa Shura ya Maimamu, Sheikh Ponda Issa Ponda, amehojiwa kwa takribani saa sita na Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, baada ya kujisalimisha mwenyewe asubuhi ya jana.

Akizungumza Dar es Salaam juzi, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, alisema Ponda alitakiwa kujisalimisha polisi ndani ya siku tatu, baada ya kudaiwa kutoa lugha za uchochezi, kukejeli shughuli za Serikali na makosa mengine ya jinai, alipofanya mkutano na waandishi wa habari Jumatano wiki hii na kuelezea mazungumzo aliyofanya na Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, baada ya kumtembelea katika Hospitali ya Nairobi, nchini Kenya, anakotibiwa kutokana na kupata majeraha ya risasi alizopigwa Septemba 7, mwaka huu nyumbani kwake, mjini Dodoma.

Polisi walivamia mkutano wake katika hoteli moja iliyopo Kariakoo kwa nia ya kumkamata, lakini hawakufanikiwa, badala yake wakaondoka na baadhi ya waandishi baada ya kuwakataza kutoka ndani ya ukumbi huo hadi watakapompata Ponda.

Akizungumza ofisini kwake jana, mmoja wa mawakili wanaomtetea, ambaye pia alishiriki mahojiano hayo, yaliyofanyika kuanzia saa tano asubuhi hadi saa 6:55 mchana na saa 8:30 mchana hadi 12:30 jioni, Profesa Abdallah Saffari alisema alifika Ofisi ya Upelelezi ya Kanda Maalumu Dar es Salaam akiwa na Ponda na walitakiwa kusubiri.

Profesa Saffari alisema walisubiri na kuomba kufanya haraka mahojiano au kusubiri hadi Jumatatu ili kutoa nafasi ya wao kwenda kuswali, kwa kuwa mawakili wote wanne wa Ponda ni Waislamu.

Alisema walisubiri hadi saa sita na robo mchana, ndipo alifika ofisa upelelezi huyo akiambatana na wenzake na kutakiwa kuingia ndani na kuanza mahojiano ya mdomo (oral).

Pia alisema katika mahojiano hayo, Ponda alisimamiwa na mawakili wanne, akiwamo yeye, huku Ofisi ya Upelelezi Kanda wakiwa watano.

Profesa Saffari, aliyedai kupigiwa simu juzi usiku na Wakili mwingine wa Ponda, Nassoro Juma, ili kuongozana naye katika mahojiano hayo, alisema akiwa hapo, mteja wao alihojiwa maswali mengi kuhusu alichokizungumza Jumatano wiki hii na waandishi wa habari.

“Walimwonyesha Ponda taarifa yake kwa vyombo vya habari na video fupi waliicheza kusikia alichozungumza, ndiyo wakaanza kuuliza maswali mengi tu. Baada ya hapo tukawaambia tunakwenda kuswali, sisi tukaondoka, Ponda wakamtia nguvuni sasa, wakamkamata, bado wanaye, baada ya kuswali saa 8:30 mchana tutaendelea ili aandike maelezo yake kwa maandishi.  Tutajua kama watamwachia kwa dhamana, watampeleka mahakamani au kama kawaida ya maaskari. Ukiwa sheikh au kiongozi wa upinzani, utawekwa au utalala ndani hadi Jumatatu kumpeleka mahakamani,” alisema Profesa Saffari.

Kuhusu alichosikia katika sehemu ya video hiyo, Profesa Saffari alisema Ponda alizungumzia vitendo vya mauaji na makosa yanayoendelea nchini, huku akidai vyombo husika havichukui hatua, pamoja na safari yake aliyokwenda kumwona Lissu nchini Kenya.

“Mimi kama profesa wa sheria na Wakili wa kujitegemea sijaona kosa hapo, lakini wao ndio wapelelezi. Safari hii akipelekwa mahakamani, mimi nitaongoza kumtetea mwanaharakati mwenzangu. Mzee mwenyewe atatinga, siku nyingi sijatinga huko,” alisema Profesa Saffari.

Naye Wakili Yahya Njema alisema ilipofika saa 12 jioni ya jana, Ponda aliondoka na maaskari kwenda katika hoteli alikofanyia mkutano na waandishi wa habari, ili kupata vielelezo na kulikuwa na uwezekano wa kwenda kukagua nyumbani kwake.

“Sisi tunatawanyika, wakirudi ndiyo tutajua kuhusu dhamana, ila kwa jinsi hali nilivyoiona, hakuna dhamana muda huu labda Jumatatu,” alisema Yahya.

Katika hatua nyingine, gazeti hili lilimtafuta Mambosasa kupitia simu yake ya mkononi ambayo awali iliita, lakini haikupokelewa na baadaye haikupatikana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles