MOSCOW, URUSI
WAZIRI wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo amefanya mazungumzo na Rais Vladimir Putin pamoja na Waziri wake wa Mambo ya Nje, Sergei Lavrov, akijaribu kutuliza wasiwasi wa kimataifa kuhusu kuongezeka kwa mvutano ambao unahofiwa kuweza kuzidisha mzozo kati ya Marekani na Iran.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana mjini hapa, viongozi hao walikutana juzi katika mji wa Sochi uliopo pwani ya Bahari Nyeusi.
Taarifa hizo zinaeleza kuwa katika mkutano huo, Pompeo alisema kwamba kimsingi Marekani haitafuti vita na Iran, na kuongeza kwamba lakini nchi yake imekwishabainisha kuwa ikiwa taifa hilo litatishia masilahi yao, kitisho hicho kitajibiwa kwa njia inayoeleweka.
Viongozi hao wa Marekani na Urusi wamezungumzia pia masuala mengine ambayo yanazusha tofauti kubwa baina yao, ikiwemo mizozo ya Venezuela, Iran, Ukraine na Syria.
Pompeo vile vile ameionya Urusi dhidi ya kuingilia uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2020 nchini Marekani.
Hata hivyo, kila upande umeelezea nia ya kuboresha uhusiano baina yao ambao unachechemea na kusaka njia za kushirikiana.