WASHINGTON, MAREKANI
WAZIRI wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo, ameishambulia China kwa kutoa mikopo na kuziwekea nchi maskini mzigo mkubwa wa madeni.
Serikali ya Rais Donald Trump wa Marekani imeanzisha hatua za kupunguza ushawishi wa China barani Afrika kwa kutumia mpango wake mpya wa maendeleo ya Afrika wa uwekezaji na biashara pamoja na shirika jipya la ufadhili wa maendeleo linalojulikana kama ‘Shirika la Kimataifa la Ufadhili wa Maendeleo la Marekani’.
Wachambuzi wanasema, shirika hilo ni juhudi za Marekani za kutoa njia mbadala kwa mpango wa China wa barabara unaonuia kuiunganisha China kupitia bahari na ardhini na Kusini Mashariki na Kati mwa Asia, Mashariki ya Kati na Afrika.
Katika taarifa aliyotoa kwa viongozi wa kibiashara nchini Ethiopia, Pompeo amezitaja kampuni kama Chevron, Coca cola na Bechtel kama wawekezaji wakubwa katika bara la Afrika.
Amethibitisha pia kuwa Marekani inatafuta mkataba wa biashara huria na Kenya lakini hakutoa habari mpya kuhusu mazungumzo yalioanza mapema mwezi huu nchini Marekani baada Rais Uhuru Kenyatta na Raila Odinga kukutana na Rais Trump.
Pompeo amesema kuwa Serikali ya Rais Trump inataka ushirikiano huo wa kibiashara kuendelea na kupanuka.
“Tumejitolea kutimiza hayo, Kama kuna kitu mnapaswa kuelewa kuhusu rais wetu- mwajiri wangu – unapaswa kuelewa kuwa anapenda mikataba. Anataka mengi kufanyika . Anataka mengi kufanyika kati ya Marekani na mataifa yote barani Afrika,” alisema Pompeo.
Kwa mujibu wa Kjetil Tronvoll, mtaalamu wa masuala ya Ethiopia kutoka Chuo Kikuu cha Bjorknes mjini Oslo, ziara ya Pompeo nchini Ethiopia pia ilipangwa kuonyesha uungaji mkono wa mageuzi ya kisiasa ya Waziri Mkuu, Abiy Ahmed licha ya visa vya ghasia za kisiasa.
Ethiopia inatarajiwa kuandaa Uchaguzi, Agosti 29 na Abiy ameahidi kuandaa uchaguzi huru na haki tofauti na miongo iliyopita ya ukandamizaji.
Ethiopia ilikuwa kituo cha tatu cha ziara ya waziri Pompeo katika mataifa ya Afrika, ambayo ilimfikisha pia katika mataifa ya Senegal na Angola.
Wachambuzi wamesema mbali na ushirikiano wa kibiashara, ziara ya waziri huyo ililenga pia kupeleka ujumbe tofauti na hatua za Marekani za hivi karibuni kuhusu Afrika.
Miongoni mwa hatua hizo pamoja na mambo mengine ni vikwazo vya viza kwa raia wa nchi nje za bara hilo ambazo ni Nigeria, Sudan, Tanzania na Eritrea.
Wakati huo hoo Pompeo yuko mjini Riyadh kwa mazungumzo na viongozi wa Saudi Arabia yanayolenga kukabiliana na Iran.
Nchini Saudia ni ziara yake ya kwanza tangu tukio la kuuawa kwa jenerali wa ngazi ya juu wa Iran kusababisha ongezeko la mvutano wa kikanda.
Mwanadiplomasia huyo wa juu wa Marekani alifanya mazungumo na Mwanamfalme Mohammed bin Salman sambamba na Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudia, Faisal bin Farhan.
Ajenda zilizotawala mazungumzo yake ni pamoja masuala ya kiusalama na kitisho kutoka kwa Iran pamoja na haki za binadamu nchini Saudi Arabia.
Ziara yake ya siku tatu kwa mshirika wake wa karibu Saudi Arabia, inakuja baada ya Marekani kumuua kamanda wa ngazi ya juu wa Iran, Qassem Soleimani.