24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Sababu Simiyu kushika namba tano matokeo kidato cha nne

Na Derick Milton – Simiyu

WENGI wanasema ni maajabu, ingawa kwa wenyeweji wanasema hilo ndilo lilikuwa lengo lao na wamelitimiza, Mkoa wa Simiyu kushika nafasi ya tano kitaifa katika matokeo ya kidato cha nne 2019.

Licha ya kutumiza lengo hilo, shauku kubwa ya viongozi wa mkoa huo ni kuona siku moja unatajwa katika nafasi tatu za juu, lengo ambalo wamejiwekea kwa mwaka huu.

Ni kama maajabu kweli, kwani kwa miaka miwili mfululizo, 2018 na 2019 mkoa umekuwa miongoni mwa mikoa 10 bora katika matokeo ya kidato cha nne na kidato cha sita.

Maajabu mengine Simiyu ni kuingia kwenye 10 bora matokeo ya darasa la saba, kidato cha nne na cha sita mwaka 2019, huku ukiwa ni miongoni mwa mikoa ambayo ufaulu wake unaongezeka kwa kasi kila mwaka.

Licha ya kuwa na changamoto kibao, ikiwamo ukosefu wa walimu wa kutosha wa masomo ya sayansi, vyumba vya madarasa, nyumba za walimu, umbali wa shule na makazi bado umeendelea kuonyesha maajabu hayo.

Maajabu mengine ni kwamba mkoa huo umeendelea kufanya vizuri kwa miaka ya hivi karibuni kuanzia mwaka 2017, ukiwa na shule nyingi za serikali (shule za kata) na shule chache binafsi tofauti na mikoa mingine.

Mkoa wa Simiyu, huwezi kuulinganisha na Mkoa wa Dar es Salaam, Mbeya, Mwanza, Kilimanjaro na Arusha kwa wingi wa shule zinazomilikiwa na watu binafsi, ambazo zimekuwa zikifaulisha kwa kiwango kikubwa.

Takwimu za mkoa huo zinaonyesha kuwa kuna jumla ya shule za msingi za serikali 529 huku binafsi zikiwa 10, na shule za sekondari za serikali (shule za kata) 144 huku binafsi (private) zikiwa 11.

Haya nayo yanatajwa kama maajabu mengine kwa mkoa huo, kwani unazo shule chache binafsi tena ambazo hazifanyi vizuri kama ilivyo kwa shule zilizoko mkoani Dar es Salaam au Mbeya, lakini umefanya vizuri zaidi ya mikoa hiyo.

Kwa mwaka 2019, matokeo ya kidato cha nne, Mkoa wa Simiyu umeshika nafasi ya tano kati ya mikoa 31, ukitanguliwa na Mkoa wa Kilimanjaro, Arusha, Iringa na Njombe.

Katika matokeo hayo, mkoa huo umepanda nafasi nne juu, kutoka nafasi ya tisa mwaka 2018, ambapo imefaulisha kwa asilimia 87.04, tofauti na Dar es Salam ulioshika nafasi ya 18 asilimia 75.29 ya ufaulishaji, Mbeya nafasi ya nane sawa na asilimia 86.18 na Kagera nafasi ya saba asilimia 84.29.

Kasi hiyo kwenye sekta ya elimu inatajwa kuwa kubwa ndani ya miaka miwili, huku ikiwa tishio kwa mikoa mikongwe na ambayo hufanya vizuri kama Kagera, Mwanza, Mbeya, Dar es Salaam, Morogoro, Kilimanjaro na Arusha.

Kwa muda mrefu kabla na baada ya kuundwa kwa mkoa huo mwaka 2012, ulikuwa miongoni mwa mikoa inayoshika nafasi za mwisho shule za msingi na sekondari.

Takwimu zinaonyesha kuwa mwaka 2013 mkoa ulishika nafasi ya 24 kati ya mikoa 25 matokeo ya darasa la saba, 2014 ulishika nafasi ya 22 kati ya mikoa 25, 2015 nafasi ya 16 kati ya 26. Mwaka 2016 nafsi ya 14 kati ya 26, 2017 nafasi ya 16; mwaka 2018 nafasi ya 22 kati ya 26 na 2019 nafasi ya 8 kati ya mikoa 26.

 Kidato cha nne mwaka 2014 mkoa huo ulishika nafasi ya 17 kati ya mikoa 30; 2015 nafasi ya 14 kati ya mikoa 30; mwaka 2016 nafasi ya 14 kati ya 31; mwaka 2017 nafasi 11; mwaka 2018 nafasi ya tisa na 2019 nafasi ya tano kati ya mikoa 31.

Kidato cha sita mwaka 2017 ulishika nafasi ya 26 kati ya mikoa 29, mwaka 2018 nafasi ya 10 na mwaka 2019 mkoa nafasi ya 10 kati ya mikoa 31.

 Baadhi ya wanafunzi waliokuwa kambi ya kidato cha nne 2019, wakijisomea mmoja mmoja na katika makundi muda wa usiku wakati wa kambi katika shule ya sekondari Simiyu (Picha na Derick Milton).

Mafanikio makubwa yalianza kuonekana mwaka 2017, baada ya wadau mbalimbali chini ya mkuu wa mkoa kutafuta njia ya kuundoa katika nafasi za mwisho ambazo ulikuwa ukishika kila mwaka.

Kambi za kitaaluma

Moja ya sababu kubwa inayotajwa na kila mtu, ambayo imefanya mkoa huo kufanya maajabu kwa miaka miwili mfulululizo ni kuanzishwa kwa kambi za kitaaluma zilizoanza rasmi Julai 2017.

Siyo tu kufanya vizuri kwa miaka hiyo, bali kambi hizo zinatajwa na kila mtu wakiwamo wanafunzi, viongozi wa serikali na kisiasa, wadau wa elimu kwamba zimeufanya mkoa huo kuongeza ufaulu kwa kasi.

Wazo la kuanzishwa kwa kambi hizo lililetwa na Mkuu wa Mkoa, Antony Mtaka (mwasisi wa kambi za kitaaluma Simiyu), ambapo mwanzoni mwa utekelezaji wake haikuweza kupokelewa kwa asilimia zote na wadau.

Kambi hizo zilianza kutumika kwa wanafunzi wa kidato cha sita pekee, kutokana na uchache wao mkoa wa mzima, ingawa zilianza na changamoto nyingi ikiwamo kukosekana kwa mahitaji muhimu hasa kwa wasichana.

Hata hivyo, kwa kipindi hicho ambapo wanafunzi hao walikaa kambi kwa muda wa wiki mbili, bado zilionekana hazina umuhimu na hazijazaa matunda kutokana na mkoa huo kushika nafasi ya 29 kati ya mikoa 31 matokeo ya kidato cha sita mwaka 2017.

Mwaka 2018 kambi hizo zilifanyika tena, kutoka wiki mbili hadi siku 30 kwa wanafunzi hao wa kidato cha sita, hapo ndipo mafanikio yakaanza kuonekana kwani mkoa ulishika nafasi ya 10 kwa mara kwanza.

Mafanikio hayo yalianza kubadilisha mawazo ya baadhi ya watu waliokuwa wakipinga kambi hizo na mwaka 2018 wanafunzi wa kidato cha nne nao walianza kambi siku 30.

Kambi hizo zilianza kuzaa matunda, ambapo mkoa uliingia 10 bora kwa mitihani yote miwili kidato cha sita na kidato cha nne na kuonekana kuwa ajenda kuu kwa kila mdau wa elimu.

Wanafunzi

Wanafunzi wamekuwa wakimpongeza mkuu wa mkoa kwa kubuni njia ya kambi, kwani zimeleta mageuzi makubwa kwao na zimesaidia zaidi kwenye vipindi vya sayansi.

Wanafunzi hao wanasema kuwa kwenye shule zao kumekuwa na tatizo kubwa la walimu wa Sayansi jambo ambalo hupata msaada mkubwa kwenye kambi hizo kutokana na kuwapo kwa walimu wengi na mahili.

“Kwenye kambi hizi walimu wamekuwa wakitupitisha kila mada na wakati mwingine unakuta shuleni kwetu mada zote tunakuwa hatujamaliza kutokana na uchache wa walimu, tukija hapa mada zote tunazisoma,” anasema Zawadi Joseph.

Kambi hizo zinatajwa kuwa msaada mkubwa na mwanafunzi Yohana Lameck, ambaye alipata ufaulu wa daraja kwanza alama saba na  masomo yote tisa akipata alama A na hivyo kushika nafasi ya kwanza kimkoa.

Yohana anasema bila ya kambi za kitaaluma, asingefanya vizuri kwa kiwango hicho, kwani alikuwa na tatizo kwenye masomo ya Sayansi upande wa mafunzo kwa vitendo (practical).

“Shuleni hatuna maabara na walimu wa Sayansi wapo wawili tu hivyo, upande wa mafunzo kwa vitendo sikuweza kujifunza kabisa, nilipokuja kwenye kambi nilipata fursa ya kusoma kwa vitendo maana maabara zilikuwapo na walimu wengi wa Sayansi walikuwapo,” anasema Lameck.

Naye Zawadi Joseph ni mmoja wa wanafunzi ambaye kwenye mtihani wa utimilifu (Mock) alipata daraja sifuri, anasema baada ya kuja kwenye kambi aliona mabadiliko makubwa kwake kwenye masomo.

“Mtihani wa kuhitimu nimefanikiwa kupata daraja la nne alama 26, (Division IV point 26) sikutegemea kabisa kama mimi naweza kupata alama hiyo, wakati nikiwa shuleni nilikuwa tayari nimekata tamaa, lakini hizi kambi zilirudisha matumaini,” anasema Joseph.

Walimu

Nao walimu wanasema kuwa mkuu wa mkoa ni mtu wa pekee kwani hakuna mwingine ambaye aliyefikiria kuhusu kuanzisha kambi za kitaaluma ikiwa ndio njia pekee ya kuinua elimu mkoani Simiyu.

Wanasema kambi hizo zimerudisha matumaini kwa baadhi ya wanafunzi waliokuwa tayari wamekata tamaa na masomo kutokana na mazingira ya shuleni kwao.

“Kuna wanafunzi walikuja kwenye hizi kambi wakiwa hawajui chochote, lakini leo wamefaulu hadi daraja la pili na tatu, huku wengi wao wakipata daraja la nne, wote hao walikuwa hawana matumaini tena ya kushinda,” anasema mwalimu Joseph Kazimoto.

Kwa upande wake Mwalimu Omari Ngusa anasema kambi hizo zilisaidia hata wanafunzi ambao walikuwa hawajawahi kutembea na kubadilisha mazingira, ambapo kwao ilikuwa faraja kubwa.

Wanafunzi wakiwa kwenye kambi za kitaaluma

“Kuna wanafunzi walikuwa hawajawahi kufika hapa Bariadi Mjini, ilikuwa mara yao ya kwanza kufika na hao wengi wao ndiyo walipata daraja sifuri kwatika mtihani wa utimilifu lakini kubadilisha mazingira peke yake ilisaidia kubadili matokeo yao,” anasema Mwalimu Ngusa.

Wananchi

Baadhi ya wananchi wanasema mwanzoni ilikuwa ngumu kuelewa lengo la kambi hizo ndiyo maana wapo waliogoma kuchangia chakula, huku wengine wakihofia watoto wao kupata mimba.

Mgema Buyugu ni mmoja wa wananchi hao kutoka kijiji cha Chinamili Wilaya ya Itilima, anasema baada ya kuona mafaniko ya kambi hizo, kwa sasa wananchi wamejitoa kuchangia.

“Tunamshukuru Mkuu wa Mkoa, mwanzoni hatukumuelewa lakini sasa hivi tunaona umuhimu wa kambi hizi, nasi tayari tumejipanga kuhakikisha tunashirikiana naye ili kambi hizi zilete mafanikio zaidi,” anasema Buyugu.

Naye Ndabagija Katani, anasema kutokana na umuhimu wa kambi hizo, wazazi wengi wanaomba kuongezwa muda na kwamba wapo tayari kuchangia ili watoto wao waweze kufaulu vema.

Ofisa Elimu Mkoa

Ofisa Elimu Mkoa huo, Erenest Hinju, anasema tangu kuanzishwa kwa kambi hizo kumekuwapo na mabadiliko ya uendeshaji wake, lengo likiwa ni kuleta tija zaidi kwa wanafunzi wenyewe na mkoa.

Anasema kambi ambazo zilifanyika mwaka 2019 zilikuwa tofauti na zile zilizofanyika mwaka 2017 na mwaka 2018, ndiyo maana mkoa ulishika nafasi ya tano kitaifa.

“Mwaka jana tumebadilisha kidogo, baada ya kufanyika mtihani wa utimilifu kidato cha nne, tuliwakusanya wanafunzi wote waliopata alama sifuri kwenye mtihani huo na kuwaweka pamoja kisha kuwatafutia walimu mahili,” anasema Hinju 

Anaongeza: “Lakini pia tuliwakusanya waliofanya vizuri zaidi nao tukawaweka eneo moja, hivyo tulikuwa na vituo viwili vya kambi, lengo la kufanya hivyo ilikuwa ni kupunguza sifuri pamoja na kuongeza ufaulu.”

Hinju anasema kuwa maboresho hayo yameleta tija zaidi kwa mkoa na kufanikisha kushika nafasi ya tano kitaifa, huku akieleza kuwa wataendelea kufanya maboresho ya kambi hizo ili kuleta tija zaidi.

Hinju anaeleza kuwa wanatafuta mfumo mzuri wa kuboresha kambi za wanafunzi wa darasa la saba kutokana na wingi wao. Anasema wamedhamiria kushika nafasi tatu za juu kidato cha nne, darasa la saba na kidato cha sita.

Mkuu wa mkoa

Mtaka anasema kuwa wakati anafikiria kuanzishwa kwa kambi hizo, alitafakari na kujiuliza kwanini madhehebu ya dini kama Wasabato wanaweza kukaa kambini kwa mwezi mzima?

Mtaka anabainisha kuwa mbali na kujiuliza hilo, alijiuliza pia kwanini wanafunzi wadogo shule za msingi na sekondari wanaweza kukaa kambi kwa ajili ya UMISETA na UMITASHUMITA?

Anasema maswali hayo yalikuja baada ya kuona kambi za kitaaluma ndiyo mwarobaini wa kuinua elimu mkoani humo, kwani changamoto zilizokuwa zikisababisha kutofanya vizuri zilikuwa nyingi.

Anasema baada ya kuleta wazo hilo, baadhi walipinga wakisema hakutakuwa na usalama hasa kwa wasichana kupata mimba, chakula, malazi na mambo mengine.

“Niliuliza mbona watu hawana wasiwasi kwenye UMISETA, UMITASHUMITA, kambi za Wasabato, lakini wamekuwa na wasiwasi kwenye kambi za kitaaluma, tulianza kufanya lakini kwa changamoto hizo na kila mwaka tuliboresha,” anasema Mtaka.

Mtaka anaeleza kuwa mbali na kuwapo kwa vikwazo hivyo na baadhi ya watu kupinga, kambi za kitaaluma mkoani Simiyu zimeanza kuigwa na mikoa mingine baada ya kuona mafanikio yaliyopatikana kwa miaka miwili.

“Watu wameona tunavyokuja kwa kasi chini ya kambi hizi, nasi tunazidi kubuni njia ya kuziboresha kwani lengo letu ni kushika nafasi tatu za juu zaidi kwa mithani yote ya taifa,” anasema Mtaka.

Mkuu huyo wa mkoa anataka kuwaonyesha Watanzania kuwa elimu bora au mwanafunzi kufaulu vizuri siyo lazima asome kwenye shule kubwa za watu binafsi, bali hata shule za serikali za kata anaweza kusoma.

“Nataka kuwaonyesha Watanzania na kurudisha thamani ya shule za kata, shule za serikali ambayo imepotea muda mrefu, watu waanze kurudisha watoto wao kwenye shule hizi, wajue hata Simiyu wanaweza kuleta watoto wao,” anasema Mtaka.

Anasema kupitia kambi hizo ikiwa pamoja na kuweka mikakati mingine kwa kushirikiana na wananchi ambao wengi wameunga mkono, mwaka 2020 mkoa wake utashika nafasi tatu za juu kwenye mitihani yote.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles