Na THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM
BENCHI la ufundi la Simba linafahamu kwamba safu ya ulinzi ya Azam FC inaundwa na mabeki wenye roho mbaya wanapotekeleza majukumu yao uwanjani wakiongozwa na watu wawili wanaocheza kati, Aggrey Morris na Yakubu Mohamed, hivyo limeamua kuwapa mazoezi maalumu wachezaji wao kwa lengo la kuwaepusha wasiumizwe.
Simba na Azam zitashuka dimbani kesho kuumana katika pambano la Ligi Kuu Tanzania Bara litakalopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam.
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limeiruhusu Azam kutumia uwanja huo ambao ni mali ya klabu hiyo kwa ajili ya mechi zake zote za Ligi Kuu msimu huu ikiwemo dhidi ya timu za Simba na Yanga.
Kabla uamuzi huu wa sasa, TFF iliipa Azam idhini ya kuutumia uwanja huo kwa mechi zake zisizohusu Simba na Yanga kutokana na kuhofia usalama, kwa vile timu hizo zina idadi kubwa ya mashabiki wakati una uwezo wa kuingia watu 7,000 pekee.
Kuelekea mchezo huo, Kocha Mkuu wa Simba, Joseph Omog, juzi kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam aliwapa wachezaji wake mazoezi ya kuruka sarakasi kama njia itakayowasaidia kuwaepusha na majeraha pale wanapochezewa rafu mbaya kama kukatwa kwa nyuma.
Omog pia aliendelea kuinoa safu yake ya ushambuliaji ili kuhakikisha inafunga mabao ya kutosha.
Katika mazoezi hayo, kocha huyo wa zamani wa Azam aliwapa kazi maalumu ya kupiga krosi, kisha washambuliaji wa timu hiyo; John Bocco, Nicholous Gyan, Laudit Mavugo na Juma Luizio, kutakiwa kuzitumia kufunga mabao.
Akizungumza baada ya mazoezi hayo, Kocha Msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja, alisema wanakabiliwa na mchezo mgumu mbele yao hivyo lazima wajihami kuhakikisha wanapata ushindi kwenye mchezo wa kesho.
“Tunakutana na timu ambayo baadhi ya wachezaji kama Aishi Manula, John Bocco, Erasto Nyoni na Shomari Kapombe waliichezea, hivyo lazima watakuwa wameukamia mchezo huo, lakini tutahakikisha tunatoka kifua mbele,” alisema.
Naye mshambuliaji, John Bocco, sasa anakipiga Simba baada ya kusajiliwa wakati wa dirisha la usajili akitokea Azam, alisema wapinzani wao wako vizuri, lakini wamejipanga kupambana nao na kupata pointi tatu muhimu.
“Nafahamu mchezo huo utakuwa ni mgumu sana, kwani kila mtu amejiandaa kadiri ya uwezo wake kuhakikisha anashinda, kwa upande wetu tutatumia mbinu tulizofundishwa na kocha kusaka ushindi,” alisema.
Mara ya mwisho timu hizo zilikutana katika pambano la Kombe la FA, ambapo Simba iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Azam.