23.5 C
Dar es Salaam
Monday, June 24, 2024

Contact us: [email protected]

MAGUFULI ALIVYOWANG’OA MAWAZIRI

Na ELIZABETH HOMBO -DAR ES SALAAM

WAKATI ripoti za kamati za uchunguzi wa makinikia ya dhahabu zikiondoka na Profesa Sospeter Muhongo, aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, zile za Bunge zilizochunguza almasi na tanzanite, zimeondoka na mawaziri wawili, baada ya Rais Dk. John Magufuli, kuwaambia waliotajwa na kamati hizo wakae pembeni kupisha uchunguzi.

Mawaziri waliotajwa kwenye ripoti hizo ambao jana kwa nyakati tofauti walisema wameshajiuzulu nyadhifa zao baada ya kauli ya Rais ni Waziri  wa Nchi Ofisi ya Rais (TAMISEMI), George Simbachawene na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Edwin Ngonyani.

Baada ya kujiuzulu kwa mawaziri hao jana, sasa nafasi za uwaziri zilizo wazi ni nne, ikiwamo ile ya Profesa Muhongo na Dk. Abdallah Possi aliyekuwa Naibu Waziri (Ofisi ya Waziri Mkuu), Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, ambaye aliteuliwa kuwa balozi.

Kali ya Magufuli

Jana baada Rais Magufuli kukabidhiwa ripoti za kamati za Bunge na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alisema. “Kwenye taarifa hii wako watu wametajwatajwa na wengine mimi ndiye nilihusika kuwateua, sasa ukishatajwa inawezekana uko so much clean (msafi sana) lakini umetajwa.

“Inawezekana wewe ni mchapakazi, mpole na handsome (mtanashati) lakini umetajwa na mimi naamini Zungu (Mwenyekiti wa Kamati ya Almasi, Mussa Zungu) au Doto (Mwenyekiti wa Kamati ya Tanzanite, Doto Biteko) hawezi akamwonea mtu, lakini wewe Spika (Job Ndugai) uliyepokea huwezi kumwonea mtu na mimi sitaki kuamini kwamba kuna wabunge watamwonea mtu.

“Sasa kwa sababu mimi ndiye niliwateua na wako kwenye position (nafasi) fulani lakini nilikuteua na umetajwa, kwanza naagiza vyombo vya ulinzi na usalama vifuatilie yote haya, vifanye haraka.

“Lakini la pili wale ambao wametajwatajwa ambao ni wateule wangu uwe waziri, naibu waziri, katibu mkuu, RAS, DC, mkurugenzi na inawezakana ulifanya kule na sasa ni mkurugenzi wa wilaya, lakini ulitajwa na hivi vyombo haviwezi kufanya kazi kama bado uko serikalini, ni matumaini yangu watazingatia hili, ni matumaini yangu watakaa pembeni.

“Najua mmenielewa, ninayazungumza haya si kwa sababu nachukia watu lakini tukienda kwa utaratibu huu tutakuwa watumwa, tunaibiwa mno, ni maajabu wengine wanaohusika ni watendaji wetu, unaposaini mkataba mkubwa kama huo na kuna ofisi ya AG (Mwanasheria Mkuu wa Serikali) na wasaidizi wake unaweza kujiuliza maswali mengi,” alisema Rais Magufuli.

Wanaotajwa

Kusu watu ambao wametajwa na ripoti zaidi ya moja, alisema. “Kuna watu saa nyingine kila mahali anatajwa, ukigeuka kwenye hili yupo, mahali pengine yupo kila mahali yupo… na kwa sababu wakati mwingine wabunge wana immunity (kinga) atakuwa yupo humo humo bungeni.

“Na saa nyingine anachangia hoja na anapochangia mpaka mishipa saa nyingine inasimama, lakini watu wanajua ukweli.

“Hili pia linaaibisha Bunge kwa sababu wapo wabunge ni wazuri sana. Nakubaliana na wewe kuwa mna ile kamati yenu ya adhabu, sifahamu kama inaweza kuzungumza.

“Sitaki kuingilia kwa sababu ni mhimili unaojitegemea, kama inawezekana kubadili kanuni mengine muwe mnapeana adhabu huko huko.

“Pia nakubaliana na wewe kuwaandikia barua vyama maana na mimi ni mwenyekiti chama (CCM), hao wabunge ambao kila mahali wanatajwatajwa, usisite kuwaandikia na matatizo yao huko, sisi huwa tuna taratibu zetu, tunaweza tukawaonya, tunaweza kuwajadili wakajitetea chama kitazingatia miiko yake.

“Lakini nashukuru kwenye ripoti yenu mmesema suala la mfumo ni tatizo, nataka ifike mahali kama tuanze upya, tufunge mgodi kuliko kukaa hapa, watakuja watu wenye akili, watoto au wajukuu zetu waje wafanye hii kazi,”alisema.

Viongozi waliotajwa kwenye ripoti za almasi na tanzanite na ambao pia walitajwa kwenye zile za dhahabu ni Profesa Muhongo, Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mstaafu, Frederick Werema.

Awashangaa BoT

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli alieleza kushangazwa kwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kushindwa kuwa na kituo ambacho kitahifadhi madini ya tanzanite yanayopatikana Tanzania pekee.

“Niwaombe viongozi wenzagu serikalini kama Tanzanite inatoka Wilaya moja tu ya Simanjiro, BoT ambayo inasimamia rasilimali na fedha za nchi hii, wameshindwa kuwa na kituo chao pale kukusanya Tanzanite halafu wananunua na kuweka kwenye reserve (hifadhi) ya nchi? Nani alituloga sisi?”Alihoji.

Alimtaka Waziri Mkuu, Majaliwa, kuita wataalamu wanahosika na kukaa na wajumbe hao wa kamati za Almasi na Tanzanite kwa maandalizi ya kubadilisha sheria mbalimbali zinazohusu rasilimali hizo.

“Hatujachelewa huu ndio wakati, lazima tubadilishe kwa manufaa ya nchi yetu.  Wabunge hawa wangepewa Tanzanite mbili mbili si wangekuja na ripoti yenye page mbili wasema hakuna tatizo kabisa? Lakini mmetanguliza uzalendo mbele, ”alisema Rais Magufuli.

Amsafisha profesa Mruma

Pamoja na kwamba ripoti hiyo ilimtaja Profesa Abdulkarim Mruma ambaye alikuwa mwenyekiti wa bodi ya ukaguzi wa madini na kutuhumiwa kusaini mkataba bila kuusoma na hivyo kuruhusu madini yapotee kizembe, Rais Magufuli alimsifisha msomi huyo.

Alisema kwa sehemu kubwa, Profesa Mrema ndiye aliyetoa taarifa zilizosaidia kujulikana namna nchi inavyoibiwa kwenye madini.

“Kujua kwenye kilo hizi tulizoibiwa ni kilo ngapi na zimesafirishwa ngapi, aliyefanya hiyo kazi ni Profesa Mruma, aliyevumbua hayo mabaya ni Profesa Mruma, aliyekuwa anatupa information (taarifa) zote za huko kuwa tunaibiwa ni Profesa Mruma.

“Wakati nimeanza kuzungumza haya masuala ya uwizi, wako watu waliona nazungumza tu kutoka hewani, nataka niwaeleze tulifanya research (utafiti) ya kutosha tulitumia baadhi ya wafanyakazi, tuna information (taarifa) zote ,tulifyonza data (taarifa) zao zote kwenye migodi yote.

“Na waliposhtuka wakabadilisha kompyuta zao ‘it was too late (wamechelewa) tunamawasiliano yao ya email (barua pepe) yote, waliyokuwa wana-communicate na jinsi walivyokuwa wanapanga mikakati ya kuiba,”alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles