27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

MAOMBI YOTE KWA LISSU

Na WAANDISHI WETU -DODOMA/DAR

NI taharuki. Ndivyo unavyoweza kusema, baada ya watu wasiojulikana kumpiga kwa risasi Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema).

Tukio hilo lilitokea jana mchana mjini Dodoma wakati mbunge huyo alipokuwa anarejea nyumbani kwake, ambapo watu hao walimvizia akiwa ndani ya gari na kuanza kummiminia risasi zaidi ya 20 ambazo zimemjeruhi vibaya.

Baada ya tukio hilo ambalo lilizua taharuki kwa wabaunge na wananchi, Lissu alikimbizwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma kwa matibabu.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana na Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, walisema Lissu alipigwa risasi jana saa saba mchana, akiwa nje nyumbani kwake, eneo la Area D, mjini Dodoma, alipokuwa akitoka kuhudhuria vikao vya Bunge.

Kwa mujibu wa viongozi hao, vyombo vya ulinzi la usalama vilianza kufuatilia tukio hilo, muda mfupi baada ya kutokea.

Naye mmoja wa viongozi waandamizi wa Chadema makao makuu, alisema kabla ya Lissu kupigwa risasi, dereva aliona gari aina ya Nissan likiwafuatilia kwa nyuma na kulitilia shaka.

“Dereva alisema wakati wanatoka bungeni, kuna gari moja aina ya Nissan nyeupe ilikuwa ikiwafuatilia kwa nyuma, hivyo akaitilia shaka kwa sababu Lissu amekuwa akilalamika, kwamba kuna watu wanamfuatilia.

“Kwa hiyo, alichokifanya ni kwamba, baada ya kukaribia kuingia nyumbani kwake, dereva alimshauri asiteremke kwenye gari ili ajiridhishe na usalama wa gari hilo.

“Wakati wanasubiri kuona mwisho wa hilo gari, mfyatuaji wa risasi alishuka kwenye gari hilo lililokuwa nyuma yao na kumimina risasi kwa kutumia bunduki aliyokuwa nayo na kisha akarudi kwenye gari na kuondoka,” alisema kiongozi huyo kwa kifupi.

MWIGULU

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, alilaani tukio hilo na kusema lazima waliohusika wakamatwe na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

“Hili ni kati ya matukio mabaya sana kuwahi kutokea hapa nchini na linachafua heshima ya nchi yetu kimataifa. Kwa hiyo, Serikali haiko tayari kuwavumilia wahusika na tutawasaka kwa namna yoyote hadi watakapopatikana.

“Hata kama tukio hilo ni la kisiasa, hata kama ni la hujuma, hata kama ni ujambazi au ugomvi, hatuko tayari kulivumilia na tayari nimeshawaelekeza polisi wadhibiti njia nzote za kuingia na kutoka Dodoma ili kuwabaini wahalifu hao.

“Ninachokisema hapa, ni kwamba Watanzania wamwombee Lissu ingawa najua yeye ni ‘radical’, kwa sababu yoyote ile, alichofanyiwa hakikubaliki.

“Yaani hata ukiona picha za kwenye tukio, zinaonyesha watu hao walikuwa na nia mbaya na walitaka kumuua ila ni Mungu tu kamwokoa,” alisema Mwigulu na kuongeza.

“Kuhusu afya yake kwa sasa ni kwamba taarifa za hivi punde nilizopewa zinasema madaktari wameshafanikiwa kudhibiti damu zisivujie tumboni na kinachofuata sasa ni kuimarisha afya ili afanyiwe upasuaji.

“Kwa upande wa idadi ya risasi alizopigwa, siwezi kusema kwa sababu katika taarifa niliyopewa hilo hawakulisema,” alisema Mwigulu.

WAZIRI WA AFYA

Kwa upande wake, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alisema matibabu ya kwanza yalifanyika vizuri na kwamba miongoni mwa madaktari waliomhudumia mgonjwa ni pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk. Mpoki Ulisumbisya.

“Hatua ya kwanza tayari, hatua ya pili ya matibabu ambayo itahusisha upasuaji ikikamilika, ndipo ataweza kuhamishiwa katika Hospitali yetu ya Taifa Muhimbili kama kutakuwa na sababu ya kufanya hivyo.

“Nawaomba wananchi na Bunge waamini mgonjwa yuko katika mikono salama, yaani tunao uwezo wa kumtibu, madaktari wapo na miongoni mwao ni katibu wa wizara ambaye anashiriki kwa kuwa yeye ni daktari bingwa,” alisema..

SPIKA WA BUNGE

Kwa upande wake, Spika wa Bunge, Job Ndugai, alisema alipata taarifa za tukio hilo akiwa njiani kutoka Dar es Salaam alikokuwa amekwenda kikazi.

“Nimepata taarifa za tukio hilo nikiwa njiani kutoka Dar es salaam ndiyo maana nilipofika hapa na wabunge wenzangu, tulikuja moja kwa moja hapa hospitalini.

“Kwa kifupi, mgonjwa yuko kwenye mikono salama na tutahakikisha tunafanya kila linalonalowezekana apone,” alisema Spika.

MKUU WA MKOA

Wakati hayo yakisemwa, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana, aliwataka wakazi wa Mkoa wa Dodoma wasiendelee kuja hospitalini hapo kwa wingi kwa sababu hawataweza kumwona Lissu kutokana na matibabu aliyokuwa akiendelea kupata.

“Hata Naibu Spika amefika hapa, amezuiwa asimwone, kwa hiyo, wananchi wawe watulivu juu ya tukio hilo,”alisema Rugimbana.

MBOWE

Akizungumzia tukio hilo, Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, alisema hawezi kuhusisha suala hilo na shughuli za Lissu kwa kuwa ni mapema mno kufanya hivyo.

Hata hivyo, alisema anaamini vyombo vya ulinzi na usalama, vitalifanyia kazi suala hilo na wahusika kupatikana kwa haraka.

Kwa mujibu wa Mbowe, washambuliaji hao walitumia bunduki aina ya SMG, kumimina risasi kwenye gari alilokuwamo mbunge  huyo.

KAULI YA POLISI

Naye Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto, aliwataka wananchi watoe ushirikiano wa kuwakatama wahalifu hao kwani bila wao polisi hawataweza kufanikiwa katika kazi zao.

MGANGA MKUU

Naye Mganga Mkuu, Mkoa wa Dodoma, Dk. James Kiolongwe, alisema hali ya Lissu ilikuwa ikiendelea kuimarika kutokana na matibabu aliyokuwa akiendelea kupata.

“Hali yake inaendelea kuimarishwa kwa sababu uwezo wa kumtibu tunao na tuna huduma nzuri za dharura ila kama kuna taarifa za kutoa, tutaendelea kuzitoa.

“Kuhusu idadi ya risasi zilizoko mwilini, sijaelezwa ingawa nimeambiwa amepigwa tumboni na miguuni,” alisema Dk. Kiolongwe.

Wakati hayo yakiendelea, baadhi ya wabunge waliokuwa hospitalini hapo, walikuwa wakiangua vilio baada ya kupata taarifa za tukio hilo.

Miongoni mwa wabunge hao ni wabunge wa Viti Maalum wa Chadema, Zubeda Sakuru na Kunti Majala ambao walikuwa wakinyamazishwa na wenzao.

Pia mamia ya wananchi wa Mkoa wa Dodoma, walikuwa wamejazana hospitalini hapo kushuhudia kilichokuwa kikiendelea licha viongozi wa hospitali hiyo kuwafukuza ili kupisha huduma nyingine.

MWANDOSYA, PONDA

Tukio la kupigwa risasi kwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) mjini Dodoma limeshtua wengi akiwemo Waziri wa zamani wa Nchi Ofisi ya Rais, Profesa Mark Mwandosya.

“Leo ni siku ambayo Watanzania hatukutaraji yaliyotokea yangetokea, jaribio la kumuua mheshimiwa Tundu Antipas Lissu kwa risasi mjini Dodoma.

“Sala zetu na maombi yetu kwa Mwenyezi Mungu yawe na mheshimiwa Tundu Lissu ili amwokoe maisha yake na kumpa unafuu katika maumivu ya majeraha yake.

“Sala zetu pia ziikumbuke familia yake na wananchi wa jimbo lake la uchaguzi,” alisema Prof Mwandosya kupitia ukurasa wake wa Facebook.

Naye Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda, alisema kuwa amesikitishwa tukio la kupigwa risasi kwa Lissu.

“Nimesikitishwa na tukio la kupigwa risasi mheshimiwa Tundu Lissu. Ni tukio linalopingana na misingi ya sheria za nchi.

“Bila shaka wakati wa ukombozi ukifika hata jiwe litapiga kelele, ninaamini wakati wenyewe haupo mbali. Ni ujinga na upuuzi kudhani kwamba matumizi ya silaha yanaweza kuzuia ukombozi. Wanaodhani hivyo wanakinzana na akili zao,” alisema Sheikh Ponda

MATUKIO YA LISSU

Katika siku za hivi karibuni Lissu alizungumza na vyombo vya habari na kusema kuwa moja kati ya ndege aina ya ‘Bombadier Dash Q400’ mali ya shirika la ndege la Tanzania ATCL imeshikiliwa nchini Canada na kampuni moja ya Ujenzi ijulikanayo kama Stirling Civil Engineering Ltd.

Lissu alidai kuwa sababu za kushikiliwa ndege hiyo ni kutokana na serikali ya Tanzania kudaiwa kiasi cha dola za Marekani milioni 38 ambazo ni zaidi ya Sh bilioni 87 na kwamba Kampuni hiyo imetishia kuipiga ‘mnada’ ndege hiyo ili kufidia deni hilo.

Lissu ambaye pia ni Mwansheria Mkuu wa Chadema, alisema kuwa mwaka 2009 kampuni hiyo ya Stirling Civil Engineering Ltd, ilipewa kandarasi ya kutengeneza Barabara ya Wazo Hill – Bagamoyo.

Hata hivyo siku moja baadaye Serikali kupitia Kaimu Msemaji wake, Zamaradi Kawawa ilijibu tuhuma hizo na kudai kuwa suala hilo limekuwa likichochewa na wanasiasa ambao si wazalendo kwa nchi.

Pamoja na hali hiyo mara kadhaa Lissu alitoa tahadhari ya na kudai anawindwa na vyombo vya ulinzi na usalama kila anakokwenda.

Alisema wamekuwa wakimfuata kwa kutumia gari dogo kila anapokwenda hivyo aliwaambia wasimfuate yeye wawafuate majambazi.

“Hapa kwenye huu mkutano Polisi mpo muwapelekee ujumbe mabosi zenu, muache kutufuata tunaofanya kazi ya kuwawajibisha serikali mkakamate majambazi,’’alisema Lissu.

Licha ya hali hiyo Lissu amefungulia kesi kadhaa kwa mwaka huu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ikiwemo za uchochezi huku akipinga hatua ya kutaka kupimwa mkojo wake.

Pamoja na hali hiyo hata alipotoka kwa dhamana alisema kuwa hatanyamaza ila atafanya hivyo akiwa mfu kaburini.

Lissu ambaye anasifika kwa kuwa na misimamo dhidi ya Serikali pia alikaririwa akisema kuwa ataendelea kuikosoa Serikali hadi pale atakapokufa.

“Hakuna gereza litakalotunyamazisha, watu wakipelekwa mahabusu watazungumza wakiwa mahabusu, wakifungwa watazungumza wakiwa kifungoni, hivyo ili wanyamaze itabidi kwanza wafe… tutanyamaza tukiwa wafu kwa sababu wafu hawasemi,” alisema.

Alisema katika sheria ya uchochezi ya mwaka 1953, kutoa kauli yoyote yenye lengo la kukosoa matendo ya Serikali, sera si kosa na wala kumkosoa rais na Serikali yake si kosa.

“Sasa ukisema wanakukamata, wanakushtaki kwa uchochezi, wanakupiga, wanakupeleka central (kituo kikuu cha polisi) au Oysterbay wakikupeleka sio kosa, bali unatumia akili zako kuikosoa Serikali.

“Niliwaambia nyie maaskari mimi nimeshtakiwa kwa uchochezi, unathibitishaje uchochezi kwa kupima mkojo?” alisema Lissu.

JPM agiza msako

Kwa upande wake Rais Dk. John Magufuli jana kupitia akaunti yake ya mtandao wa Tweet alisema amepokea kwa kwa masikitiko tukio la kupigwa risasi Tundu Lissu, ambapo alimwombea kwa Mwenyezimungu aweze kupona haraka.

“Vyombo vya dola viwasake wale wote waliohusika na tukio hili la kinyama na kuwafikisha ktk mikono ya sheria,” alisema Rais Magufuli.

Naye Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, alisema kuwa amepokea kwa mshtuko mkubwa taarifa za kupigwa risasi kwa Lissu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles