25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

NJOMBE MJI KUTUMIA ‘UCHAWI’ WA MALAWI KUIUA YANGA

Na THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM

KOCHA Mkuu wa Njombe Mji, Hassan Banyai, amesema anaamini kambi ya siku saba waliyoweka nchini Malawi, itawasaidia kuwakalisha wapinzani wao Yanga.

Njombe Mji itakuwa mwenyeji wa Yanga katika pambano la Ligi Kuu Tanzania Bara litakalopigwa Jumapili  kwenye Uwanja wa Sabasaba mjini Njombe.

Timu hiyo ambayo ni miongoni mwa timu tatu zilizopanda daraja msimu huu ikiwa pamoja na Lipuli na Singida United, ipo nchini Malawi ikijifua kwa mchezo dhidi ya Yanga.

Timu hiyo ilianza vibaya msimu mpya wa Ligi Kuu baada ya kunyukwa mabao 2-1 na Tanzania Prisons kwenye uwanja wao wa Sabasaba.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Banyai alisema baada ya kuanza ligi vibaya, safari hii hawatakubali kupoteza tena zaidi ya kuvuna pointi tatu dhidi ya Yanga.

“Tunakutana na Yanga ambao mchezo wao wa kwanza walitoka sare ya bao 1-1, hivyo nafahamu watakuwa na hasira ya kutaka kupata ushindi mbele yetu, lakini hatutawapa nafasi ya kuchomoka mbele yetu,” alisema.

Alisema kikosi chake kipo fiti kikiendelea na mazoezi nchini humo, huku morali ya wachezaji wake ikiwa ya kiwango cha juu.

“Nina majeruhi watatu kwenye kikosi changu ambao ni Hussein Akilimali, Mark Mwambunguru na Shaban Kondo, vinginevyo wengine wako fiti.”

Banyai aliwataka mashabiki wa timu hiyo wajitokeze kwa wingi kwenye mchezo huo ili kuwapa sapoti wachezaji wao ili waweze kujituma na kupata matokeo mazuri.

“Tunatarajia kurudi Jumamosi asubuhi Njombe tukiwa fiti kabisa kuwavaa Yanga, kwani tunaamini pointi tatu muhimu zitabaki kwetu,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles