Na WALTER MGULUCHUMA- KATAVI
MTU mmoja aliyejulikana kwa jina la Salaganda Kipeta, mkazi wa Tarafa ya Kipeta, Wilaya ya Sumbawanga, Mkoa wa Rukwa, amejeruhiwa vibaya kwa kupigwa risasi mguuni.
Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Rukwa, George Kyando, aliwaambia waandishi wa habari jana kwamba, Kipeta alijeruhiwa na Ofisa Wanyamapori katika Pori la Akiba la Uwanda wa Kipeta, aliyetambuliwa kwa jina la Lemomo Miseyeko.
Alisema kwamba, tukio hilo lilitokea juzi saa saba mchana katika pori hilo la akiba.
“Mwananchi huyo alipigwa risasi baada ya kutuhumiwa kuingia ndani ya msitu wa hifadhi bila kuwa na kibali.
“Katika harakati za kutaka kumkamata, mtuhumiwa alikaidi amri halali iliyomtaka atulie, ndipo ofisa huyo wa wanyamapori alipoamua kumpiga risasi katika mguu wa kushoto na kumjeruhi vibaya.
“Kwa kifupi chanzo cha tukio hilo ni Salaganda kukaidi amri halali ya kumtaka asimame ili akamatwe,” alisema Kamanda Kyando.
“Kwa hiyo yule askari aliyehusika katika tukio hilo, tunamshikilia kwa mahojiano zaidi kwani alitumia nguvu nyingi zaidi kumdhibiti majeruhi ambaye hakuwa na silaha,” alisema Kamanda Kyando.
Pamoja na hayo, kamanda huyo wa polisi alitoa wito kwa askari wa wanyamapori kuacha kutumia vibaya mamlaka waliyonayo pindi wanapokuwa wakitaka kuwakamata watuhumiwa.
Pia aliwataka wananchi kuacha tabia ya kuingia ndani ya hifadhi bila vibali kwa kuwa kufanya hivyo ni kukiuka sheria.