23.6 C
Dar es Salaam
Wednesday, September 27, 2023

Contact us: [email protected]

WAZIRI MKUU AAGIZA UMEME WA UHAKIKA KISARAWE II

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amemwagiza Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, kuhakikisha eneo la Kisarawe II linakuwa na umeme wa uhakika ili kuwezesha viwanda na wananchi wa eneo hilo kupata nishati hiyo.

Alitoa agizo hilo juzi jioni alipotembelea kiwanda cha Milkcom kinachozalisha bidhaa za maziwa na kiwanda cha Watercom kinachozalisha maji vilivyoko katika Kata ya Kisarawe II wilayani Kigamboni akiwa katika ziara yake ya kikazi.

“Waziri wa Nishati ahakikishe eneo hili linapata umeme wa uhakika ili kuviwezesha viwanda hivi kufanyakazi vizuri jambo litakaloongeza uzalishaji. Pia wananchi wanaoishi katika maeneo haya nao watanufaika na upatikanaji wa nishati hiyo,” alisema Majaliwa.

Alisema amefarijika na jitihada za mwekezaji huyo za kuunga mkono mkakati wa Serikali ya Awamu ya Tano wa kuifanya Tanzania kujenga uchumi wa viwanda utakaoliwezesha Taifa kufikia uchumi wa kipato cha kati ifikapo mwaka 2025.

Awali, Msemaji wa viwanda hivyo, Aboubakar Faraj, alisema moja ya changamoto zinazowakabili ni pamoja na upatikanaji wa umeme wa uhakika jambo linalosababisha kupanda kwa gharama za uzalishaji.

“Punde umeme unapokatika tunalazimika kutumia majenereta kwa muda mrefu. Hii husababisha ongezeko la gharama za uzalishaji ambazo huumiza kiwanda kwa sababu haiwezekani kumtwisha mzigo huu mlaji,” alisema.

Faraji alisema changamoto nyingine ni miundombinu ya barabara ambayo husababisha wateja wengi kushindwa kufika kwenye viwanda hivyo kwa urahisi, hivyo aliiomba Serikali kuwatatulia kero hiyo.

Aliongeza kuwa kwa sasa viwanda hivyo vimeajiri watu zaidi ya 1,800, ambapo alisema endapo Serikali itawahakikishia upatikanaji wa umeme na barabara wataongeza ajira kwa asilimia 25 ifikapo mwaka 2018.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,729FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles