23.6 C
Dar es Salaam
Saturday, May 18, 2024

Contact us: [email protected]

NYALANDU:TUSIGEUZE SIASA MATIBABU YA LISSU

NA AZIZA  MASOUD, DAR ES SALAAM


MBUNGE wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu(CCM) ameitaka jamii kuacha kulijadili kwa mtazamo wa siasa, suala la matibabu ya Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu (Chadema), anayetibiwa  Nairobi, Kenya  kwa kuwa kufanya hivyo kutachangia kuligawa Taifa.

Nyalandu  alitoa kauli hiyo jana katika kipindi cha Tuongee Asubuhi kinachorushwa na  Kituo cha Star Tv alipokuwa akizungumzia masuala mbalimbali, hasa ushiriki wake katika matibabu ya Lissu.

Alisema  kitendo cha mtu kuhusika na kumshambulia kwa risasi Lissu, lilikuwa  jambo la kushtusha  na liligusa mioyo ya watu wengi.

“Jambo la kumsaidia  Lissu limeelezwa vizuri, kwa kuangalia utashi wa familia, Serikali  na wana Chadema kila mtu anajaribu kuangalia maslahi mapana ya afya ya  Lissu.

“Kamwe tusilichukulie suala la Lissu kisiasa, matibabu ni dhamana ya chama hiki au kile, mimi nasema tuwe na fursa za kutofautiana kwa hoja, kuumwa si suala la siasa,”alisema Nyalandu.

Alisema tukio hilo  linapaswa kulaaniwa kwa kuwa  kama  limeweza kumtokea Lissu pia  linaweza kumtokea mtu  mwingine.

“Niwakumbushe tu mimi naingia hapa katika matibabu kama jirani, yule ni kaka yangu, mbunge mwenzangu wa Singida kuona jambo hili lililofanyika limetugusa kiasi gani,”alisema Nyalandu.

Nyalandu ambaye anadai alilia baada ya kupata  taarifa hizo, alisema ameamua kuungana na watu wanaomsaidia Lissu kwa kuwa anahitaji mkono wa ukombozi ili apone.

Alisema tukio hilo ambalo limefanywa na watu wabaya wa mbunge huyo, linapaswa kulaaniwa na kila Mtanzania kama alivyofanya Rais Dk.John Magufuli na viongozi wengine wa Serikali, vyama na dini.

“Ni muhimu kufahamu tundelee kulaani kwa sababu linagawa Taifa na kuleta mmomonyoko … limenisikitisha kwa sababu mimi  mbunge wa CCM napakana na Lissu,”alisema Nyalandu.

Alisema kinacholeta ustawi wa jamii ni kuwa na mijadala ya wazi, kutofautiana kwa mawazo kwa wazi na kushindana kwa hoja na si vingine.

“Naamini jambo hili la Lissu  linawaunganisha sana watanzania isipokuwa katika mazungumzo kwa kuwa huwezi kuwazuia watu kuongea.

“Wana midomo, wapo wanaotaka kulionyesha kwamba lipo tofauti, nawaona watu wachache kuliko watanzania na viongozi wengi kutoka chama cha CCM na viongozi wachache,”alisema Nyalandu.

Alisema mbunge huyo amepona kwa miujiza kwa kuwa  mara kadhaa amekwenda kumtembelea   Nairobi  na aliona hali yake haikuwa nzuri.

“Nilipoenda  mara ya kwanza ilitangazwa lakini nimeenda tena mara kadhaa ambazo sijaziripoti, nimeona ile hali lakini ninaamini kwamba Mungu amemfanya Tundu Lissu kuwa miujiza.

“Nimeona miujiza mingi lakini kilichomtokea Lissu, Mungu aliruhusu aishi kwa kuwa Mungu amemfanya aishi, hili jambo tuliamishe liwe la taifa lisitugawe,”alisema Lazaro.

Alisema watanzania waguswe na kilichompata mbunge huyo na siyo kugeuza maneno na matendo yao kwa kutumia utashi wa ndani ya mioyo yao.

Alisema  bila kujali tofauti  zozote za siasa, kabila na itikadi  watanzania wanapaswa kuungana kumuombea.

“Kwa sababu madaktari wanaomtibu ni watu, wakikosea sehemu moja anaweza akapata shida zaidi, tumuombe Mungu azidishe fahamu za wale wanaomtibu  arudi katika hali yake ya kawaida,”alisema Nyalandu.

Alisema  anaiona safari ndefu ya matibabu ya Lissu hasa kipindi hiki cha kumuweka sawa katika majeraha aliyoyapata.

“Mtu ukiumia sana sehemu za mwili hata ukiungwa kwenye mifupa,sehemu za ndani, kuna mambo mengi ambayo hatuyajui yatatokea hivyo atahitaji muendelezo wa mazoezi ya mwili na viungo, na ushauri wa saikolojia,”alisema Nyalandu .

Alisema ushauri wa saikolojia utamsaidia kufahamu kwamba  kilichotokea kilikuwa na nia mbaya kwake lakini Mungu alikuwa na nia nzuri zaidi.

Nyalandu alisema amekuwa akisaidiana na Chadema kuhakikisha unafanyika utaratibu wa kumpeleka nje ya nchi kuhakikisha anapatiwa  matibabu zaidi.

Alisema ili kukamilisha mpango huo anaendelea kufanya mazungumzo na marafiki zake walioko Ulaya na Marekani.

Mbunge huyo alisema  amekwisha kufanya mazungumzo na hospitali ambayo itakuwa tayari kumsaidia  pamoja na madakatari wake.

Alisema kinachoendelea sasa ni kufuata ushauri wa madaktari wa Nairobi ambao walimzuia kutokana na hali yake.

Kuhusu  uvumi  wa kufukuzwa   CCM, Nyalandu  alisema  kitu hicho hakipo wala hajawahi  kupatiwa barua ya onyo tangu alipojiunga na chama hicho.

“Saa nyingine siyo kila lisemwalo lazima ujibu, tangu niwe mwanachama sijawahi hata kupatiwa barua ya onyo.

“Nilichaguliwa awali  mwaka 2005  nikiwa mbunge mdogo zaidi, sasa nipo mara ya nne.  Naamini katika kujadiliana masuala ya wazi na ukweli  ni kwamba maswali magumu katika jamii hayana majibu rahisi,” alisema Nyalandu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles