Na ASHA BANI -DAR ES SALAAM
MWENYEKITI wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP), Abdul Nondo, amesema anahitaji kupumzika kwa sababu hayupo vizuri kiakili.
Akizungumza jana baada ya kuwasili jijini Dar es Salaam akitokea mkoani Iringa baada ya kupata dhamana juzi dhidi ya kesi inayomkabili mahakamani, Nondo alisema anahitaji kupumzika lakini muda si mrefu atawaelezea Watanzania yaliyomkuta hadi alipopata dhamana.
Alisema akiwa katika mapumziko atakuwa anaandaa waraka ambao unaweza kuwa tayari ndani ya siku mbili ambao utaelekeza kwa kina yaliyomsibu hadi kufikishwa mahakamani.
“Kwa sasa ‘mentally’ (akili) siko vizuri lakini nikitulia nitaweza kuzungumza, ndani ya siku 20 zikiwemo tatu za kukaa mahabusu Iringa hadi kupata dhamana,’’ alisema Nondo.
Alipoulizwa kuhusu kusimamishwa chuo na uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema hajui lolote na hata barua ya kusimamishwa hajakabidhiwa hadi sasa .
Pamoja na mambo mengine, mwanafunzi huyo amewashukuru Watanzania waliopasa sauti zao hasa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu na Jeshi la Magereza mkoani Iringa alilokaa nalo vizuri.
Kwa upande wa Mratibu wa THRDC, Onesmo ole Ngurumwa alisema watakwenda mahakamani kupinga aumuzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kumsimamisha masomo Nondo kwa ajili ya kesi inayomkabili ambayo kwa sasa ipo mahakamani.
“Na ndiyo maana hata Mahakama ya Iringa ilisema kuwa wampe dhamana kwa kuwa mwanafunzi ili aweze kuendelea na masomo lakini wao wanamsimamisha, atasoma lini?
“Na kama ikija kubainika kwamba hakufanya kosa watafanyaje wakati wenzake walikuwa wakiendelea na masomo? huu ni uonevu ambao hautakiwi kuvumiliwa,’’ alisema Olengurumwa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Hellen Kijo-Bisimba, alisema kilichofanywa na UDSM ni uonevu ikizingatiwa mazingira magumu aliyonayo na kitendo cha kumuweka ndani kwa muda mrefu.
“Hata kanuni zilizopo chuoni hapo hazifai kutumika kutokana na kwenda kinyume na sheria na haki za binadamu,” alisema.
DARUSO
Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Daruso), imeshangazwa na kitendo cha kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii barua ya kusimamishwa masomo kwa Abdul Nondo kabla hajakabidhiwa mwenyewe.
Rais wa Daruso, Jeremiah Jilili ameikosoa barua hiyo kuwa ina makosa mengi na ikiwamo kukosewa kwa kozi anayosoma Nondo
Mwisho.
Biteko aeleza madini ujenzi yanavyoingiza fedha
Na VERONICA SIMBA
-DODOMA
NAIBU Waziri wa Madini, Doto Biteko amesema madini ya ujenzi na viwanda yanaingizia Serikali kiasi kikubwa cha fedha ikilinganishwa na aina nyingine za madini yanayopatikana nchini.
Akizungumza na wafanyakazi wa Ofisi ya Madini Dodoma akiwa kwenye ziara ya kazi, Biteko alisema takwimu zinaonyesha mwaka 2016/17, tani milioni 15.6 za madini ya ujenzi zilizochimbwa, ziliingiza Sh. bilioni 230.6.
“Kati ya fedha hizo, ulipatikana mrabaha wa Sh bilioni 7.1,” alisema Biteko.
Alisema pia idadi ya wachimbaji wa dhahabu na madini mengine nchi nzima wakijumlishwa, hawawezi kufikia hata robo ya wale wanaofanya shughuli za madini ya ujenzi.
Alisema Serikali imejipanga kuhakikisha inaongeza vituo vya madini ya ujenzi na viwanda kutoka 85 vilivyopo sasa nchi nzima hadi kufikia 174.
“Nina uhakika tukiviongeza vituo kufikia idadi hiyo, tutakusanya mrabaha wa zaidi ya Sh bilioni 15 katika madini hayo pekee,” alisema Biteko.
Biteko pia aliwataka wakandarasi wanaotekeleza miradi mbalimbali hususani ya ujenzi wa barabara, watimize wajibu wao kwa kuzingatia sheria ya madini inayomtaka kila mtu aliyepewa leseni kulipa tozo na kodi stahiki.
“Kama tuna Watanzania ambao ni maskini na tunachukua mrabaha kwao, halafu kampuni kubwa yenye mtaji mkubwa inayoendesha shughuli za ujenzi iache kulipa kodi stahiki, hiyo haikubaliki,” alisema.
Biteko alisema, Wizara ya Madini itaandaa utaratibu wa kukutana na kujadiliana na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), ambao ndiyo hupewa leseni kwa mujibu wa sheria kuhusu namna bora ya kusimamia suala husika ili madeni yaliyopo yalipwe.
Maagizo hayo ya Naibu Waziri Biteko yalikuja baada ya Ofisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Dodoma, Silimu Mtigile kumsomea ripoti iliyoeleza kuwa ofisi yake inakabiliwa na changamoto ya ukusanyaji mirabaha inayotokana na wakandarasi wa barabara.
“Katika miradi mikubwa ya barabara iliyopo Dodoma, ulipwaji wa mirabaha ya madini ujenzi kutoka kwa wakandarasi umekuwa wa kusuasua ambapo hadi sasa kiasi cha Sh 642,632,195.00 kimekusanywa, sawa na asilimia 33.11 kati ya jumla ya Sh 1,941,177,853.23 zinazopaswa kulipwa,” alisema Mtigile.
Mwisho.
Mwasisi Chadema kuzikwa Dar kesho
Na TUNU NASSOR
-DAR ES SALAAM
MWILI wa aliyekuwa Katibu Mtendaji na Mwasisi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Victor Kimesera unatarajiwa kuzikwa kesho mchana katika makaburi ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Akizungumza jana na MTANZANIA, msemaji wa familia, Mali Kimesera alisema ibada ya mazishi itaanza saa nne asubuhi nyumbani kwa marehemu, Mtaa wa Uporoto, Victoria Mwananyamara jijini hapa.
Alisema kwa sababu kesho ni Alhamisi Kuu, mazishi yatafanyika saa saba mchana ili kutoa fursa kwa watakaokwenda katika ibada za siku hiyo.
“Tunatarajia kuanzia ibada ya mazishi saa nne asubuhi ili kutoa nafasi kwa wataokwenda katika ibada ya Alhamisi Kuu,” alisema Mali.
Kimesera alifariki Machi 24, mwaka huu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), alipokuwa akipatiwa matibabu.