31.2 C
Dar es Salaam
Monday, July 22, 2024

Contact us: [email protected]

POLISI WATOE UFAFANUZI KWA KIFO HIKI

JESHI la polisi mkoani Mbeya kwa mra nyingine limekumbwa na kashfa ya mauaji ya mfanyabiashara katika mazingira ya kutatanisha.

Jeshi hilo linatuhumiwa kumuua mfanyabiashara ya machungwa, Allen Mapunda mkazi wa Uwanja wa Ndege, Kata ya Iyela baada ya kumkamata na baadaye kufariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa Mbeya.

Jeshi hilo, linadaiwa kumkamata Mapunda akiwa katika shughuli za kijamii, lakini  kwa siku moja aliyoshinda mahabusu imebadili historia au kuondoa kabisa uhai wake hapa duniani.

Kama kawaida polisi hufanya shughuli zao za doria katika maeneo mbalimbali, lakini katika tukio hili kijana huyo alikamatwa saa tano usiku katika kibanda cha kulia chakula.

Hatupingi polisi kutimiza wajibu wa kisheria, lakini tunapata maswali mengi namna ambavyo watuhumiwa wakitua mikononi mwao muda mfupi wanapoteza maisha.

Jambo hili limekuwa likijitokeza mara ka mara mno katika maeneo mbalimbali. Hivi inakuwaje unyama huu unatendeka kiasi hiki?

Tunaamini siku zote polisi hufanya kazi kwa sheria, sasa hawa watuhumiwa wanapoteza uhai kwa njia hizi? Mosi kama ilivyo desturi yao wamekuwa wakitumia nguvu kubwa pasipo na sababu.

Lakini pili, polisi wanatembeza kipigo kizito hata pale pasipostahili jambo ambalo tunaamini si sahihi.

Katika tukio hili, mama mdogo wa marehemu, Aris Mapunda anasema hata walipokwenda kumtolea dhamana mwanawe walimkuta akiwa dhaifu, anatetemeka, huku akilalamika kupigwa na askari.

Hata baada ya kufikishwa hospitali ya Hospitali ya mkoa kwa matibabu na baadaye walimhamishia Hospitali ya Rufaa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini ambako alifariki dunia kutokana na kipigo kikali.

Si nia yetu kuelezea mlolongo wa matukio ya polisi, lakini katika hili tunataka kuona Jeshi la Polisi mkoani Mbeya, linatoa taarifa za uchunguzi wa tukio hili.

Kwa kufanya hivo, kutasaidia kurejesha imani kwa wananchi kwa sababu wapo waliohusika kwa namna moja au nyingine kumshughulikia kijana  huyo hadi kupoteza uhai.

Tunaamini siku zote kwamba, polisi wamepewa dhamana ya kusimamia usalama wa raia na mali zao, sasa inakuwaje wamshikilie mtu kisha apoteza uhai baada ya kutoka mikononi mwao?

Hatuzuii polisi kutumia nguvu pale inapohitajika, lakini mazingira ya kumkamata kijana huyo yanaonesha wazi hayakuwa hatarishi kiasi cha kumfanya atoke mikononi mwao anachechemea.

Siku zote mtu mtukutu hutambuliwa vizuri na jamii inayomzunguka kama ilivyokuwa kwa kijana huyo, baada ya wananchi kuandamana  kupinga kilichotokea.

Tunaamini  Kamanda  aa Polisi Mkoa wa Mbeya, Mohammed Mpinga kama alivyoahidi atakuja na majibu ya msingi ya kifo ili kuondoa manung’uniko ambayo yametawala kwa wakazi wa mkoa huo.

Sisi MTANZANIA tunasitiza kuwa wapo polisi wachache ambao wanataka kulichafua jeshi hili katika wajibu wake, hawapaswi kupewa nafasi hiyo.

Maana hao ndiyo wanakuwa chanzo cha kulipaka matope jeshi hilo na wakati mwingine kutaka kulichonganisha na wananchi.

Kwa msingi huo, tunataka kuona hatua  za kinidhamu zinachukuliwa dhidi ya wale wote waliohusika na tabia ya kulindana iwekwe kanda ili haki itendeke.

Kupoteza kijana mdogo kama huyo ni hasara kwa familia na taifa zima ambalo lilikuwa linamtegemea kwa namna moja au nyingine.

Tunamalizia kwa kusema, ukweli wa tukio hili utakuwa kioo mbele ya jamii inayowazunguka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles