Na Elizabeth Kilindi, Njombe.
MKOA wa Njombe,umezindua soko la uuzaji wa madini ya dhahabu na vito kwa nia ya kudhibiti wimbi la utoroshaji wa madini uliokuwa unafanywa na wachimbaji waliokuwa wakikwepa kulipa mapato ya serikali.
Akizungumza juzi, wakati wa uzinduzi huo, Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher Ole Sendeka alisema kuwapo soko hilo, litasaidia wachimbaji kutumia fursa na njia zilizosahihi kulipa mapato kwa Serikali.
“Kuanzisha soko la madini katika mkoa wetu, inakuwa fursa ya Serikali kukusanya mapato yake yanayotokana na madini, eneo letu hili la soko la madini litakalokuwa linalotoa elimu ya uchimbaji kwa njia ya kisasa na kueleza kuwaunganisha wananchi na wawekezaji wengine wenye nia ya kuwekeza mkoani kwetu,”alisema.
Alisema mkoa huo,una rasilimali nyingi za madini mbalimbali, ikiwamo aina tofauti ya vito,ni vema wachimbaji wakaendelea kuhamasisha wawekezaji mbalimbali kuwekeza kwa maslahi mapana ya taifa.
“Nampongeza Rais Dk. Magufuli kwa kuhakikisha rasilimali na utajiri wa nchi yetu unatumika kwa manufaa na maslahi mapana ya nchi yetu, sasa namna bora ya kumuunga mkono rais ni kuhakikisha madini yetu yanazalishwa bila kujali madini ya kiwandani madini ya vito yanapitwa katika mfumo na yanauzwa katika utaratibu rasmi uliowekwa na serikali”alisema Ole Sendeka.
Kamishina wa Madini Mkoa wa Njombe, Wilfred Machumu alisema changamoto iliyopo sasa ni utoroshaji wa madini kwenye baadhi ya maeneo.
“Utoroshaji wa madini upo mkubwa,hasa maeneo ya Uwemba,Lola Lupembe na Mfumbi Makete, yale maeneo ndiyo yanayotusumbua,”alisema Machumu.
Mwenyekiti Chama cha Wachimbaji Madini Mkoa wa Njombe, Alfred Luvanda alisema soko hilo litajenga imani ya uwekezaji sekta ya madini kwa wakazi wa mkoa huo kinyume na awali.