27.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Upinzani waendeleza kilio cha tume huru ya uchaguzi bungeni

Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA

KAMBI rasmi ya upinzani Bungeni, imeendeleza kilio chake cha kuwa na tume huru ya uchaguzi, safari hii wakitumia Bunge kufikisha kilio chao wakisema, kuna haja ya kuwa tume hiyo kutokana na baadhi ya wakurugenzi kufanya kampeni.

Msemaji Mkuu wa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Ruth Mollel, akiwasilisha maoni ya upinzani kwenye bajeti ya wizara ya Utumishi kwa mwaka 2020-2021 jana, alisema kambi hiyo inaona kuna haja ya uwepo wa tume huru ya uchaguzi

“Uwepo wa tume huru ni umuhimu kwa sababu tarehe 22/03/2020 huko Busokelo, Mbeya Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke Ndugu Mwakabibi akiwa kwenye harambee ya kujenga zahanati, alionekana akiwa amevaa mavazi ya Chama cha Mapinduzi na bila hofu kujitangaza kuwa ni Mbunge ajaye wa Jimbo la Busokelo, na alichangia mabati 100. 

“Huyu DED pamoja na mkewe ambaye pia ni DED wa Biharamulo, Kagera walipiga kampeni kwa uwazi na kutoa rushwa kwa wananchi wa Busokelo. Viongozi hawa ni wasimamizi wa uchaguzi (Returning Officers) katika maeneo yao. Je, watatenda haki kweli kipindi cha uchaguzi wakati inaonekana waziwazi wameegemea upande wa chama tawala? 

“Sio hivyo tu ametumia gari la ofisi ya umma kwenda kwenye harambee ya kampeni, huu si utawala bora na unatakiwa kupigwa vita kwa nguvu zote. Yu wapi Mwenyekiti wa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma? Yu wapi Waziri wa Utumishi wa Umma?

“Mheshimiwa Spika, huyu DED ndugu Mwakabibi yeye amejitokeza wazi kwamba ni mwanachama wa CCM, wapo wakurugenzi watendaji wengi ambao ni wanachama wa CCM. Hivyo basi, kauli ya Rais kwamba uchaguzi utakuwa huru na wa haki itakuwa mashakani,”alisema.

Wasiorudisha matamko

Katika hatua nyingine, Serikali imesema viongozi 592 sawa na asilimia 4 ya viongozi wote wa umma, hawajarejesha fomu za tamko la rasilimali na madeni  kwa mwaka 2019.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, George Mkuchika, akiwasilisha bajeti yake bungeni alisema viongozi wa umma 14,878 ambao ni sawa na asilimia 96 ya viongozi 15,470 wamerejesha fomu za tamko la rasilimali na madeni kwa kipindi kilichoishia  Desemba 31 mwaka  2019 ikilinganishwa na viongozi 15,391 waliorejesha kipindi kama hicho mwaka 2018. 

Alisema viongozi 592 sawa na asilimia 4 ya bado hawajarejesha fomu za tamko la rasilimali na madeni  kwa mwaka 2019.

Mkuchika alisema Wakala wa Ndege  umeingia mkataba wa ununuzi wa ndege tatu ambapo moja ni aina ya De – Havilland (Bombardier) Dash 8 – Q400 ambayo inatarajiwa kuwasili nchini mwaka 2020 na mbili ni aina ya Airbus A220 – 300 zinazotarajiwa kuwasili nchini mwaka 2021.

Pia alisema huduma za usafiri wa anga zimetolewa kwa viongozi wakuu wa kitaifa ambapo safari 117 za ndani na tano za nje ya nchi zilifanyika.

Alisema wanahewa 34 wamepatiwa mafunzo ya kisheria ya uhuishaji wa leseni zao ambapo  matengenezo madogo ya ndege tatu zinazowahudumia viongozi Wakuu wa Kitaifa yalifanyika. 

Aidha, mafuta ya ndege na vipuri vilinunuliwa kadri ya mahitaji huku gharama za bima za ndege na bima za Wanahewa zililipwa.

Vilevile ukarabati na upanuzi wa karakana za ndege za Serikali umeanza kufanyika

“Ndege mbili mpya zilipokelewa ambapo moja ni aina ya Boeing 787- 8 (Dreamliner) na nyingine aina ya De – Havilland (Bombardier) Dash 8 – Q400,”alisema.

Mkuchika alisema Wakala ya Ndege za Serikali imeingia mikataba miwili ya ukodishaji ndege na Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) na kufanya mikataba iliyosainiwa kufikia nane.

Waziri Mkuchika alisema katika kipindi cha Julai, 2019 hadi Machi, 2020, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ilitekeleza malalamiko 113 ya ukiukwaji wa maadili dhidi ya viongozi wa umma yalipokelewa na kuchambuliwa. 

“Kati ya malalamiko hayo, malalamiko 58 yalihusu Sheria ya Maadili ya Viongozi na malalamiko 55 hayakuhusu Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma. Uchunguzi kwa malalamiko 15 yanayohusu ukiukwaji wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma umekamilika na uchunguzi wa malalamiko 43 unaendelea. 

Aidha, malalamiko 55 ambayo hayakuhusu ukiukwaji wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma walalamikaji walipewa 37 ushauri na mengine yalielekezwa kwenye mamlaka zinazohusika.

Alisema  viongozi 203 (Wanaume 120 na wanawake 83) walihojiwa ikiwa ni sawa na asilimia 89 ya viongozi waliotarajiwa. 

“Kati ya viongozi 203 waliohojiwa, asilimia 14 walionekana kuwa na viashiria vya mgongano wa maslahi,”alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles