MOHAMED KASSARA -DAR ES SALAAM
LICHA ya kurejea kwa Bernard Morrison, Kocha Msadizi wa Yanga, Charles Mkwasa, amsema kuwa kitendo cha hadi sasa kutofahamika kama kiungo wao, Haruna Niyonzima atacheza katika mechi yao dhidi ya Simba, kinawapasua kichwa kutokana na umuhimu wake kwenye mechi hiyo.
Wakati Morrison akirudi kwa kishindo na kuifungia Yanga bao pekee lililoipa pointi tatu katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Kagera Sugar uliochezwa juzi kwenye Uwanja wa Kaitaba, Kagera, bado Niyonzima anaendelea kuinyima usingizi kuelekea mtanange huo.
Niyonzima yuko shakani kuukosa mchezo huo nusu fainali ya Kombe la Shirikisho dhidi ya watani zao, Simba utakaochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Hofu hiyo inakuja baada ya kiungo huyo raia wa Rwanda kutolewa katika kipindi cha kwanza katika mchezo wa ligi hiyo dhidi ya Biashara United uliopigwa kwenye Uwanja Karume, Mara baada ya kupata majeraha ya goti.
Majeraha hayo yalimsababishia fundi huyo wa kuuchezea mpira kuukosa mchezo wa ligi dhidi ya Kagera Sugar uliochezwa juzi kwenye dimba la Kaitaba, Bukoba.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Mkwasa alisema pamoja na kikosi hizcho kusheheni nyota kibao, lakini uzoefu wa Niyonzima katika michezo ya aina hiyo unahitajika katika mchezo huo mkubwa uliobeba matumaini ya kushiriki michuano ya kimataifa.
“Uwepo wa Niyonzima kwenye mechi hiyo ni muhimu sana na kila na kila Mwanayanga alihitaji kumuona akifanya kitu uwanjani hasa kutokana na uzoefu wake, lakini hadi sasa hatujawa na uhakika wa kumtumia.
“Jambo hilo linatupasua kichwa na kubaki tukitafakari kama atakuwepo mchezaji wa kutimiza majukumu yake kama ambavyo angeweza kutimiza Niyonzima pindi angekuwepo uwanjani.”