22.3 C
Dar es Salaam
Saturday, July 13, 2024

Contact us: [email protected]

NI MABOMU TU

MABOMU* Polisi wawasambaratisha Chadema, wapiga ‘Stop’ mikutano ya vyama vya siasa

Na Fredrick Katulanda, Kahama

JESHI la Polisi Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, limewasambaratisha viongozi, wafuasi na wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) waliokuwa wakitaka kufanya mkutano wa hadhara wa uzinduzi wa ‘Operesheni okoa demokrasia nchini’, jana.

Mkutano huo ambao ulitarajiwa kufanyika katika viwanja vya CDT mjini Kahama, ulianza kusambaratishwa kwa maji ya kuwasha saa 9:00 alasiri wakati viongozi wa Chadema Taifa wakiwa njiani kuingia Kahama kuanza mkutano huo.

Kabla ya kusambaratishwa kwa mkutano huo, msafara wa Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Freeman Mbowe, Katibu Mkuu Dk. Vicent Mashinji pamoja na wabunge ulipokewa katika Mji wa Kagongwa kwa pikipiki, baiskeli na magari zaidi ya 10 kabla ya kuingia Kahama mjini kuelekea viwanja vya mkutano.

Katika mkutano huo, Chadema walipanga kuzindua Operesheni okoa demokrasia kwa lengo la kuelezea uamuzi wa Bunge kuwafungia wabunge wa kambi ya upinzani bungeni kuendelea kuhudhuria vikao vya Bunge, kuzuiwa Bunge kurushwa ‘Live’ pamoja na kasoro za Serikali ya awamu ya tano ya Rais Dk. John Magufuli na baadaye wangekwenda mikoa ya Mwanza, Kagera na Mara.

 

MSAFARA WANUSURIKA AJALI

Majira ya saa 9:08 wakati msafara wa viongozi wa kitaifa wa Chadema ukielekea Kahama mjini, ghafla gari la kubeba wagonjwa lenye namba DFP 1334 Land Cruiser linalodaiwa kuwa liliwabeba maofisa wa polisi, liliingilia msafara huo na kuyagonga magari matatu ya wabunge, Godbless Lema lenye namba T 875 AKS, Halima Mdee namba T 374 BEK na John Heche namba T 309 DGG.

Hata hivyo magari hayo hayakupata madhara zaidi ya kuyumba barabarani na kuendelea na safari.

Msafara huo ukiongozwa na Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema Taifa (Bavicha), Patrobas Katambi uliingia katika viwanja vya mkutano saa 9:30 alasiri na kukutana na makundi ya wafuasi wao wakikimbia mabomu ya machozi na maji ya kuwasha.

Wakati mabomu ya machozi yanaendelea kurindima, baadhi ya wananchi walijihami kwa kuwarushia mawe polisi katika vurugu hizo zilizodumu kwa saa moja huku maduka yakifungwa na shughuli mbalimbali zikisimama katika mji wa Kahama.

Hata hivyo msafara wa viongozi hao ambao ulilakiwa na wafuasi wao kwa wingi, nao ulisambaratishwa mara moja na polisi waliotumia maji ya kuwasha na mabomu ya machozi, hivyo viongozi hao walishindwa kuteremka katika magari na kulazimika kugeuza na kuelekea katika hoteli moja mjini Kahama.

 

MBOWE AELEZEA

Baada ya kutawanyika, Mbowe aliwaambia waandishi wa habari kuwa wamesikitishwa na hatua ya polisi kuzuia mikutano yao na huku wakiwasambaratisha wafuasi wao na wanachama kwa maji ya kuwasha, risasi za moto na mabomu ya machozi.

“Hizi ni siasa za kibabe na kidikteta ambazo Rais Magufuli ameanza kuzionyesha kwa kuzuia Bunge lisionekane na sasa wanazuia mikutano ya hadhara ambayo ni haki yetu ya kikatiba,” alisema Mbowe.

Mbowe alisema Serikali ya Rais John Magufuli inaogopa kukosolewa na kuumbuliwa, huku ikitaka wanyonge wasielezwe maovu yake.

Alisema juzi walipomsikia msemaji wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Christopher ole Sendeka akieleza kuwa watapita kila watakapopita kuwajibu Chadema, walifurahi na kuona sasa wanakwenda kupambana kwa hoja, lakini wameshangazwa polisi kuanza kutumika kuwazuia.

 

MASHINJI

Naye Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Mashinji akizungumzia hali hiyo, alisema baada ya mkutano huo kusambaratishwa viongozi watakutana na watatoa taarifa yao.

Alisema polisi iliruhusu kufanyika kwa mkutano huo kwa barua ya Juni 6, mwaka huu yenye kumbukumbu namba KAH/A.24/27/VOL.XII/346 iliyosainiwa na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kahama (OCD), George Kyando ambayo iliwataka kutofanya maandamamo, kutoa kashfa, vurugu na kuzingatia muda wa kumaliza mkutano.

“Lakini wakati tumejiandaa na kutumia gharama ambazo ni fedha za walipakodi, leo (jana) viongozi wangu walipokea barua nyingine saa 6:50 kutoka kwa OCD wa Kahama, George Kyando yenye kumbukumbu namba KAH/SO.7/2/A/VOL.IV/19 ikieleza kuwa mkutano uliopangwa kuanza saa 6:00 umezuiwa kwa sababu za kiintelijensia,” alisema Dk. Mashinji.

 

KAMANDA AMKANA OCD

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Mika Nyange, alipotakiwa kuzungumzia suala hilo, alisema hajatoa ruhusa ya kuzuia mkutano huo na kuwa hatua hiyo imefikiwa na Kamanda wa Wilaya ya Kahama ambaye ana mamlaka ya kufanya hivyo iwapo ataona kuna sababu.

 

MABOMU YAATHIRI WAGONJWA

Mabomu ya machozi yaliyokuwa yakivurumishwa na polisi yaliathiri wagonjwa waliokuwa wamelazwa katika zahanati ya Kahama Community Health, iliyopo jirani na uwanja wa mkutano na kuathiri wagonjwa waliokuwa wamelazwa.

Mmiliki wa zahanati hiyo, Issa Mvano alisema amesikitishwa na polisi kutojali wagonjwa na kupiga ovyo mabomu na kuwaathiri.

MIKUTANO YA WAPINZANI YAZUIWA

Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi limepiga marufuku mikutano yote ya hadhara, maandamano ya vyama vya siasa kuanzia Juni 7, mwaka huu hadi hapo hali ya usalama itakapotengemaa.

Taarifa ya jeshi hilo iliyosainiwa na Kamishina wa Polisi Operesheni na Mafunzo, Nsato M. Mssanzya na kusambazwa kwa vyombo vya habari jana, iliwataka wanasiasa kuacha mara moja kuwashinikiza wananchi kutotii sheria za nchi, huku likitishia kuchukua hatua kali za kisheria kwa mtu au chama chochote cha siasa kitakachokaidi agizo hilo.

“Katika siku za hivi karibuni, Jeshi la Polisi nchini limepokea taarifa kutoka kwa baadhi ya vyama vya siasa wakitaka kufanya mikutano na maandamano, hata hivyo, kupitia vyanzo vyake mbalimbali vya habari limebaini mikutano hiyo ina lengo la kuwahamasisha wananchi kutotii sheria za nchi,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

 

ZITTO AITWA POLISI

Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam imemwita Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo) kwa lengo la kumhoji leo katika Kituo Kikuu cha Polisi.

Ofisa Uhusiano wa ACT-Wazalendo, Abdallah Khamis alisema jeshi hilo halijatoa sababu za kutaka kumhoji Zitto.

 

ACT WALAANI

Wakati huo huo, Chama cha ACT-Wazalendo kimelaani uamuzi wa Jeshi la Polisi kuzuia mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa nchini kote.

Taarifa ya chama hicho kupitia Katibu wa Itikadi, Mawasiliano na Uenezi, Ado Shaibu ilisema uamuzi wa kuzuia mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa hauna mashiko kwani mikutano hiyo ni ya kisheria kama ilivyoelezwa katika sheria ya vyama vya siasa ya mwaka 1992 kifungu cha 11(1).

“Sababu iliyotolewa na Jeshi la Polisi kuwa mikutano hii inalenga kuchochea wananchi kutotii sheria ni mwendelezo wa visingizio vya Serikali vinavyolenga kuminya uhuru wa wananchi kuikosoa Serikali,” ilisema taarifa hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles