30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

 Maaskofu Katoliki wamtaka Magufuli kutumia busara

Pg 1NA BENJAMIN MASESE, MWANZA

BARAZA la Maaskofu Tanzania (TEC), limemtaka Rais Dk. John Magufuli atende haki na atumie busara na akili   anapochukua hatua mbalimbali za utendaji zikiwamo za kupambana na ufisadi.

Kauli hiyo ilitolewa   na Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Method Kilaini kwa niaba ya TEC, alipozungumza na waandishi wa habari   Mwanza jana.

Askofu Kilaini na wenzake wako jijini hapa   kuhudhuria kongamano la tatu la  taifa la Ekaristi Takatifu litakalofanyika   kuanzia Juni 10 hadi 11 mwaka huu.

Akijibu maswali  ya waandishi wa habari kuhusu  utawala wa Rais Magufuli na matukio yanayojitokeza nchini, Askofu Kilaini alisema taifa lipo katika hofu.

Alisema ni  kutokana na matukio ya mauaji yanayofanywa na watu wachache waliokosa hofu ya Mungu na akataka matukio hayo yashughulikiwe kwa uzito unaostahili.

Hata hivyo kiongozi huyo wa kiroho alisema TEC haiwezi kutoa tathmini au kutoa maoni ya uongozi wa Rais Magufuli kwa sasa kwa sababu ni mapema mno.

“Bado tunampa muda  tutathmini utawala wake kwa kuwa kazi aliyoifanya kwa   miezi saba haiwezi kutoa mwelekeo wa uongozi wake kwa vile bado kuna changamoto nyingi zinazowakabili Watanzania.

“Kazi ya Kanisa Katoliki ni kuwafundisha wananchi matendo mema yanayomfurahisha Mungu katika kutenda haki na usawa.

“Kwa hiyo  tunaungana na Rais Dk. Magufuli na tunamuombea  aweze kupambana na mafisadi kwa ukamilifu na uamuzi wake uwe unamfurahisha Mungu.

“Kazi ya kusafisha mafisadi ni ngumu na inahitaji kutenda haki, kutumia busara na akili katika uamuzi wowote.

“Ili rais wetu afanikiwe lazima tuungane   na kumuombea afanye uamuzi sahihi na wa busara.

“Wanasiasa wao wanaweza kumlalamikia, lakini sisi Wakatoliki tunaendelea kumpa muda kidogo kwa sababu  bado mambo ni mengi ya kufanya ndiyo maana tunafanya kongamano hili   kuongeza matumaini mapya.

“Pamoja na hayo, TEC tumesikitishwa na vitendo vya mauaji ya watu vinavyoendelea nchini na tunapaswa kuungana bila kujali tofauti za madhehebu yetu ili kuimarisha amani kwa sababu  bila kufanya hivyo, hatutawashinda mafisadi na wanaovuruga amani,” alisema Askofu Kilaini.

Kongamano

Awali, akizungumzia kongamano hilo, Askofu Kilaini alisema katika Kanisa Katoliki, Ekaristi Takatifu ndilo tukio kubwa kuliko yote na Wakatoliki wote wanatakiwa kuwa kitu kimoja wakati wa kongamano hilo.

Kwa mujibu wa Askofu Kilaini, wakati wa kongamano hilo, kutakuwa na mada mbalimbali juu ya ekaristi, ya matumaini ya kuleta amani kwa wote hasa waliokata tamaa na ekaristi kwa masikini  kuwaletea heshima na uwezo kutoka kwenye umasikini wao.

“Pia kutakuwa na maombi kwa viongozi wa taifa hasa hasa Rais Magufuli  aweze kuongoza nchi kwa weledi wa Mungu. Pia kutakuwa na maombi kwa familia  ziweze kuishi katika upendo na amani,” alisema.

Wliwaomba waandishi wa habari nchini  kufanya kazi kwa kuzingatia maadili na wawe makini kila wanapoandaa habari za kuwafikishia wananchi kwa lengo la kujenga Tanzania yenye amani.

 Wakati huo huo, Askofu Kilaini alitangaza kuwa Juni 12, mwaka huu, Askofu Flavian Kasala wa Jimbo la Geita atasimikwa rasmi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles