27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, July 24, 2024

Contact us: [email protected]

Tume ya Uchaguzi yarejesha serikalini Sh bilioni 12  

LUBUVANa Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imekabidhi Sh bilioni 12 kwa Rais   Dk. John Pombe Magufuli, zilizobaki baada ya uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na rais uliofanyika mwaka jana

Mwenyekiti wa NEC, Jaji Mstaafu Damian Lubuva alikabidhi hundi hiyo kwa Rais Magufuli   Dar es Salaam jana, taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, ilisema.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Jaji Lubuva alisema bakaa ya fedha hizo haikuathiri kwa namna yoyote uchaguzi mkuu wa mwaka jana.

“Mheshimiwa Rais fedha ambazo tunakukabidhi, tulijibanabana sana, ingawa muda wenyewe ulikuwa mfupi lakini tulijibanabana sana bila kuathiri utendaji wa shughuli za uchaguzi.

“Isije ikawa inatoa sura kwamba iliathiri, haikuathiri, na katika hali hiyo kama ambavyo wengi ni mashahidi, hatujisifii, lakini uchaguzi ulienda vizuri,” alisema.

Akizungumza baada ya kupokea mfano wa hundi hiyo, Rais   Magufuli aliipongeza NEC kwa kuokoa fedha hizo na kuzirejesha serikalini ili zipangiwe majukumu mengine.

Taarifa hiyoilisema Rais Magufulu alitaka taasisi nyingine za serikali ziige mfano huo wa uzalendo na kutanguliza maslahi ya taifa.

“Kitendo hiki ambacho mmekionyesha leo, kinaonyesha ni kwa namna gani Tume ya Taifa ya Uchaguzi chini ya uongozi wako Mheshimiwa Mwenyekiti ilivyo na watu makini na waadilifu sana.

“Kwa sababu hizi fedha ambazo kwa lugha uliyotumia ni bakaa, kutokana na zile ambazo mlipewa zaidi ya Sh bilioni 270, mkatumia Sh bilioni 261.6, mkabakiza Sh bilioni 12.

“Mngeweza kuamua kusema hamkubakiza na hakuna mtu yeyote ambaye angewauliza, na saa nyingine pengine hakuna mtu yeyote ambaye angejua.

“Mngeweza pia kusema kiasi mlichotupa hakijatosha, tunaomba mtuongezee ama mngetengeneza maneno mazuri mazuri ya matumizi, bado nina uhakika serikalini wasingejua,” alisema Rais Magufuli.

Jaji  Lubuva pia alimuomba Rais Magufuli aisaidie tume hiyo kupata jengo lake la ofisi kwa kuwa hivi sasa  inatumia majengo ya kupanga ambayo yanaigharimu   takribani Sh bilioni 1.4   kila mwaka kwa kulipia kodi ya pango, usafiri na gharama nyingine za uendeshaji.

Rais   Magufuli amelikubali ombi hilo na kuamua kuwa fedha ambazo NEC imeziokoa   zitumike kujenga ofisi ya tume, na amependekeza ofisi hiyo ijengwe mkoani Dodoma.

 Rais Magufuli pia amelikubali pendekezo la tume hiyo la kuanzishwa   mfuko wa tume ya uchaguzi ambao utakuwa unakusanya fedha kila mwaka kwa ajili ya uchaguzi mkuu unaofuata.

Hatua hiyo itakuwa ni  badala ya kuendelea na utaratibu wa sasa wa kusubiri mwaka wa uchaguzi ndipo zitengwe fedha zote za kugharamia uchaguzi huo.

Uteuzi

Wakati huohuo, Rais   Magufuli   amemteua Jaji Ferdinand   Wambali kuwa Jaji Kiongozi kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Jaji Shaaban Ally Lila aliyeteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani.

Kabla ya uteuzi huo, Jaji   Wambali alikuwa mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto mkoani Tanga.

Uteuzi huu unaanza mara moja.

- Advertisement -
Previous article
Next article

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles