YERUSALEM, ISRAEL
WAZIRI Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu yuko mjini Moscow kuanzia jana kuonana na Rais wa Urusi Vladimir Putin kujadili wasiwasi wake kuhusu kujiimarisha kijeshi kwa Iran nchini Syria.
“Nitajadiliana na Rais Putin kuhusu harakati za  Iran kuweka kambi ya kijeshi Syria, ambayo kwa nguvu zote tunaipinga na tutachukua hatua kali kuzuia,” alionya Netanyahu, bila kufafanua, kabla ya kupanda ndege kwa ziara hiyo iliyotarajia kudumu kwa saa kadhaa jana.
Jeshi la anga la Israeli mwaka jana liliripoti kushambulia shehena za silaha za mshirika wa Iran, kundi la Hezbollah la Lebanon mara 100.
Netanyahu alisema yeye na Putin hukutana mara kwa mara kuhakikisha uwapo wa uratibu mzuri baina ya Jeshi la Israel na Urusi katika eneo hilo.
Urusi iliingilia kati vita ya wenyewe kwa wenyewe kwa niaba ya Rais wa Syria, Bashar al-Assad mwaka 2015.
Majeshi ya Iran, wapiganaji wa Hezbollah na wanamgambo wengine wa Kiislamu wa madhehebu ya Shia pia wanamuunga mkno Assad.
Israel inahofia Iran ikiachwa ijiimarishe itazidisha tisho linalosababishwa na Hezbollah nchini Lebanon, ambako lina makombora makali na ilipigana vita na jeshi la Israeli mwaka 2006.
Netanyahu pia amepanga kujadili na Putin harakati za Iran kuigeuza Lebanon kuwa kituo kikubwa cha makombora dhidi ya Taifa la Israel, kitu ambacho alisema hatokivumilia.