27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 20, 2024

Contact us: [email protected]

Ndugai: Sheria inayobana wanaoenda Z’bar ipitiwe

Na RAMADHAN HASSAN

-DODOMA

SPIKA wa Bunge, Job Ndugai ameitaka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, kuangalia namna ya kuongeza uzito wa mizigo ambayo abiria wanaotumia boti kwenda Zanzibar wanaruhusiwa kubeba bila kulipia kutoka kilo 20 za sasa.

Spika Ndugai alitoa kauli hiyo jana wakati wa kipindi cha maswali na majibu mara baada ya Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Elias Kwandikwa kujibu swali lililoulizwa na Mbunge wa Viti Maalumu, Maryam Msabaha (Chadema).

 “Maana kilo 20 hata sanduku la mwanafunzi linazidi, hata baadhi ya mashirika ya ndege yanatoza zaidi ya kilo 20, sasa kwenye boti kilo 20 ni kidogo sana.

“Ipo haja ya kuangalia kama sio sheria ni kanuni tu… Mtu akibeba mihogo mitatu kilo 20 tu anakuwa ameshavuka, kwa hiyo tuliangalie, hawa wenzetu wanaotoka Zanzibar wapate raha kidogo na imekuwa kero kwa wananchi, Serikali iliangalie hili,” alisema.

Katika swali lake, Msabaha alidai kwamba kumekuwa na kero kubwa kwa abiria wanaotumia bandari kwenda Zanzibar kwa boti, ambao hulipishwa ushuru wa bandari kwa mizigo hata boksi la kilo 10 au mchele kilo 20 kwa malipo ya Sh 9,750.

“Je, ni mizigo gani ambayo abiria anapaswa kulipia ushuru huo wa bandari (Wharfage),” alihoji.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri Kwandikwa alisema vigezo vipo katika mwongozo wa tozo TPA na kwamba tatizo linaonekana ni uelewa.

Alisema TPA huikusanyi tozo yoyote kwa abiria  ambao wana vifurushi binafsi vyenye uzito au ujazo mdogo wanaotumia bandari kwenda Zanzibar kwa boti eneo la ‘Baggage room’.

Aidha, alisema abiria wanaotozwa ushuru wa bandari katika eneo la ‘Bagage room’ ni wale tu wanaokuwa na mizigo mikubwa tena kwa madhumuni ya kibiashara.

 “Niwaelekeze bandari watoe elimu ya kutosha kwa wananchi wanaotumia bandari kwenda Zanzibar, ikiwemo hili la uzito wa kilo 21 na kuendelea ndio unatakiwa kutozwa, sio nia ya Serikali kuona wananchi wake wanalalamika,” alisema. 

Alitoa wito kwa wateja wote wanaotumia bandari kwenda Zanzibar kwa boti wahakikishe kuwa mizigo yao inapimwa kabla ya kupakiwa ili wajue uzito wake unaostahiki kutozwa ushuru.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles