24.3 C
Dar es Salaam
Monday, September 16, 2024

Contact us: [email protected]

Nderiananga azindua nyaraka za miongozo ya usimamizi wa maafa kwa Wilaya ya Kibiti 

Na Gustaphu Haule, Mtanzania Digital 

NAIBU Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Ummy Hamis Nderiananga, amezindua nyaraka za miongozo ya usimamizi wa masuala ya maafa kwa Wilaya ya Kibiti mkoani Pwani na kuwataka watendaji wa Wilaya hiyo  kuiweka ajenda ya maafa katika vikao vya ushauri vya Wilaya (DCC).

Nderiananga amezindua nyaraka hizo juzi Wilayani humo hafla ambayo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama na Serikali  ambapo pamoja na mambo mengine amesema huu uandaaji wa nyaraka za usimamizi wa maafa ni hatua moja wapo katika kuelekea ujenzi wa jamii iliyostahimilivu dhidi ya majanga katika Wilaya hiyo.

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu, Ummy Nderiananga (katikati)akizindua nyaraka ya usimamizi wa maafa ya Wilaya Kibiti mkoani Pwani.

Amesema ni vyema Wakuu wa Wilaya katika vikao vyao vya ushauri wakawa na ajenda ya maafa badala ya kusubiri majanga na kwa kufanya hivyo itasaidia kuepuka athari zinazoweza kutokea na pia kujipanga namna ya kukabiliana nazo.

Nderiananga,amesema  nyaraka hizo zilizoandaliwa zinatakiwa kuwa chachu ya kuongeza ushirikishwaji wa jamii na wadau sambamba na kujenga uelewa kuhusiana na masuala ya usimamizi wa maafa na kuimarisha mfumo wa utoaji tahadhari ya awali katika kukabiliana na maafa.

Amesema Ofisi ya Waziri mkuu ambayo ndio yenye jukumu la kuratibu na kusimamia maafa itaendelea kutafuta rasilimali kwa ajili ya kuimarisha na kujenga uwezo wa kamati za usimamizi wa maafa ngazi ya Mkoa na Wilaya ambapo pia alisisitiza ngazi ya Wilaya kufanya jitihada kama hizo ngazi ya kata na Vijiji.

Aidha, amesema kazi ya uandaaji wa mpango wa kujiandaa na kukabiliana na maafa na mkakati wa kupunguza vihatarishi vya Maafa kwa Wilaya ya Kibiti ni muendelezo wa utekelezaji wa jukumu la msingi la Ofisi ya Waziri Mkuu ambalo limelenga kuimarisha usimamizi na uratibu wa Maafa katika ngazi za Mikoa na Wilaya.

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera,Bunge na Uratibu, Ummy Nderiananga akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa nyaraka ya usimamizi wa maafa ya Wilaya ya Kibiti iliyofanyika juzi wilayani humo.

Awali, mkurugenzi idara ya menejimenti ya maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Brigedia Jenerali Hosea Ndagala amesema Ofisi yake  kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) ilianza utekelezaji wa kazi hiyo kwa Kutoa mafunzo ya kujengea uwezo kamati elekezi na kamati ya wataalamu ya usimamizi wa maafa kwa Wilaya ya Rufiji na Kibiti.

Ndagala amesema mafunzo hayo yalilenga kuimarisha zaidi kamati za usimamizi wa maafa kwa kufahamu majukumu yao kisheria, mfumo wa usimamizi wa maafa nchini pamoja na utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maafa kwa vipindi tofauti ikiwa ni kabla, wakati na baada ya maafa kutokea kwa kufuata mpango wa usimamizi wa maafa.

“Uandaaji wa nyaraka hizi umezingatia ushirikishwaji wa jamii, wataalamu wa Halmashauri na Taasisi za kiserikali katika utaratibu wa ukusanyaji wa taarifa za msingi na ushirikiano ulikuwa mzuri na mchakato wa uandaaji ulianza Juni 24, 2024 hadi leo unapoenda kuzindua rasmi nyaraka hizi,” amesema Brigedia Jenerali Ndagala.

Hata hivyo, Ndagala amewashukuru  wadau wa maendeleo UNDP kwa ufadhili ambao umechangia jitihada za Serikali katika kutekeleza kazi hiyo pamoja na uongozi wa Wilaya ya Kibiti kamati elekezi ya usimamizi wa maafa.

Naibu Waziri,Ofisi ya Waziri Mkuu Sera,Bunge na Uratibu, Ummy Nderiananga, akiwa katika picha ya pamoja na Wataalamu waliotekeleza kazi ya kutoa mafunzo kwa kamati pamoja na maandalizi ya usimamizi wa nyaraka za maafa katika Wilaya ya Kibiti Mkoani Pwani.

Mwakilishi wa UNDP, Abbas Kitogo ambaye pia ni mtaalamu wa miradi amesema wataendelea kushirikiana na Serikali katika masuala mbalimbali kuondoa vikwazo vya maendeleo na kuhakikisha elimu ya maafa inaifikia jamii kupitia kamati husika ili waweze kuepuka majanga yanayoweza kuwakumba.

Mkuu wa Wilaya ya Kibiti, Kanal Joseph Kolombo ameishukuru Ofisi ya Waziri mkuu kwa kufika katika Wilaya hiyo na kutoa elimu ya maafa na kwamba muongozo wa nyaraka za usimamizi ambao umezinduliwa utakwenda kusaidia kuchukua tahadhari ya mafuriko na namna ya kukabiliana nayo.

Mratibu wa masuala ya kutoka Shirika la mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Abbasi Kitogo, akizungumza katika uzinduzi wa nyaraka za usimamizi wa maafa kwa Wilaya ya Kibiti,hafla hiyo imefanyika mwisho wa wiki hii Wilayani humo
- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles