Na Fred Azzah, Dodoma
Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye (CCM), ameishangaa Serikali kuweka nguvu nyingi kwenye mradi wa umeme wa Stigler’s George ambao haupo kwenye ilani ya chama hicho na kuachana na umeme wa gesi ambao waliunadi wakati wa kampeni.
Akichangia hotuba ya Mapato na Matumzi ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Nape amehoji serikali kuacha mpango wa uchumi wa gesi siyo kuisaliti ilani ya CCM na wananchi wa Lindi na Mtwara?
“Tulipopiga kura mwaka 2015, tuliamini sana uchumi wa gesi ni mkombozi mkubwa na uko salama mikononi mwa Rais Magufuli (Rais John Magufuli) na Serikali ya awamu ya tano.
“Ndiyo ulikuwa mkataba wetu na si kwa maneno lakini uliwekwa kwenye ilani ya Chama Cha Mapinduzi ukurasa wa 75 hadi 77 eneo kubwa sana limezungumzwa uchumi wa gesi na imeandikwa mafuta na gesi asilia.
“Kwa hiyo, kura nyingi alizozipata Rais Magufuli ni kwasababu ya makubaliano haya yaliyopo kwenye hii Ilani ya Uchaguzi, kwamba atakwenda kuyaendeleza na kwa summary (ufupi) moja ilikuwa kuendelea kujenga miundombinu ya kuendeleza huu uchumi wa gesi kwa Lindi na Mtwara.
“La pili ilikuwa kuwaandaa wananchi wanufaike na kufaidika na gesi na mafuta kwa Lindi na Mtwara na lipo jambo mahususi la ujenzi wa LNG plant (mtambo wa kuchakata gesi) kwa mikoa ya Lindi, hili limo kwenye Ilani ya Uchaguzi.
“Lakini nasikitika sana nilipoangalia Hotuba ya Waziri Mkuu, kuanzia ukurasa wa kwanza hadi wa mwisho hakuna neno gesi kabisa,” amesema Nape.
Pamoja na mambo mengine, amesema inaonekana hata ukienda eneo lenyewe shughuli mbalimbali zinazoendana na gesi kwa Lindi na Mtwara, ni kama vile zimeanza kufungwa na shughuli imesimama kabisa.
“Sasa swali langu la kwanza, hivi ni bahati mbaya kwamba hotuba ya Waziri Mkuu imeshindwa kuliona jambo hili kuwa ni kubwa na ikaamua kuliacha au serikali imeamua kuachana nalo?
“Kwa sababu naona jitihada kubwa zinaanza kwenda kwenye Stigler’s, umeme wa maji, mimi sina matatizo nayo yawezekana huo ndiyo uamuzi lakini Stigler’s kwenye ilani haimo,” amesema.
Nape amesema Ilani imezungumzia gesi, nishati ya gesi kwa sehemu kubwa na hii ndiyo ilikuwa imani ya wana Lindi na Mtwara kwa Serikali ya awamu ya tano.
Amesema zilikuwapo jitihada zilizofanywa na Mzee Mwinyi (Rais wa Awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi) ikapatikana Songosongo na pia Mzee Mkapa (Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa), awamu ya nne ikaja na jitihada za uchumi ambao walikuwa na matumaini nao.
“Wakati jitihada zinafanyika watu watakumbuka, kuna watu walipoteza maisha pale Lindi na Mtwara, kuna watu walipata majeraha na vilema Lindi na Mtwara lakini tukaamini kuna neema kesho.
Amesema kwa hotuba ya Waziri Mkuu na kwa bahati mbaya wamemkabidi Magufuli wakaamini lipo salama, alipowapa Majaliwa (Waziri Mkuu Kassim Majaliwa) wakaamini wako salama zaidi kwa sababu Waziri Mkuu anatoka kwetu.
“Sasa ni bahati mbaya sana kwamba humu ndani hakuna kabisa kabisa, maana yake ni kwamba hili jambo pengine limenza kuachwa sasa tuende kwenye Stiglers lakini aje, hatusaliti ilani ya Uchaguzi ya CCM?
“Lakini je hatuwasaliti wana Lindi na Mtwara ambao walitupa kura na kutuamini kwamba gesi yao na uchumi wao uko salama,” amesema Nape.