Mwandishi Wetu, Dodoma
Naibu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Msafiri Mbibo amefanya ziara ya kikazi katika ofisi za TRA zilizopo Wilaya ya Chamwino na Kongwa jijini Dodoma ambapo amewataka watumishi wa ofisi hizo kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha wanavuka malengo ya ukusanyaji kodi waliyopangiwa katika wilaya zao.
Ziara hiyo ameifanya baada ya kumaliza ufunguzi wa mafunzo ya siku tatu kwa makatibu wa kamati za kudhibiti uadilifu ndani ya mamlaka hiyo.
Alisema kuwa katika utekelezaji wa majukumu yao ya kazi wanatakiwa kuhakikisha wanatenda mambo mema hata kama kuna changamoto wanazokutana nazo bila kusahau kufanya kazi kwa bidii, ubunifu na heshima kwa watu wote.
“Hata kama mnakutana na changamoto mnatakiwa kuhakikisha mnatenda mambo mema bila kusahau kufanya kazi kwa bidii, heshima na ubunifu,” alisema Mbibo.
Katika ziara hiyo alikutana na Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Suleiman Serera ofisini kwake ambapo pamoja na mambo mengine, walijadiliana mipango mbalimbali ya kuongeza mapato wilayani humo.
Naibu Kamishna Mkuu huyo anaendelea na ziara yake katika maeneo mbalimbali mkoani hapa ikiwa na dhumuni la kutembelea ofisi za TRA na kuzungumza na watumishi kwa ajili ya kuwapa hamasa ya kuendelea kufanya kazi kwa bidii na weledi katika majukumu yao ya kila siku.