26.9 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

TRA yaweka mikakati ya kuimarisha uadilifu kazini

Mwandishi wetu, Dodoma

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imejiwekea mikakati mbalimbali itakayowezesha kuimarisha uadilifu katika utendaji wake wa kazi.

Moja ya mkakati huo ni pamoja na uundaji wa kamati za kudhibiti uadilifu ndani ya mamlaka hiyo kwa ajili ya kuongeza mapato ya Serikali hapa nchini.

Hayo yamesemwa na Naibu Kamishna Mkuu wa TRA, Msafiri Mbibo jijini Dodoma wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kwa makatibu wa kamati hizo za kudhibiti uadilifu ndani ya mamlaka hiyo.

“Kama mnavyofahamu Tanzania imeingia katika uchumi wa kati, hivyo kama tunataka kuhakikisha tunadumu katika uchumi huu wa kati au tunaenda zaidi ya tulipo ni lazima jamii yetu iendeshe mambo yake kwa uadilifu mkubwa na taasisi kama TRA ambayo ni nyeti ni lazima tuboreshe eneo la maadili ili kuwa na nidhamu katika suala zima la ukusanyaji kodi,” alisema Mbibo.

Alisema TRA ina jukumu la kukusanya kodi kwa niaba ya Serikali na jukumu hilo haliwezi kutekelezwa kwa ufanisi bila kuwa na watumishi waadilifu ikiwa ni pamoja na uwepo wa mfumo imara unaosimamia uadilifu.

“Jukumu la TRA ni kukusanya kodi ambazo zinahusisha fedha, na sisi sote tunajua kwamba, fedha zina ushawishi mkubwa lakini hata wateja wetu ambao ni walipakodi wanaweza kuwashawishi watumishi wetu ili wasilipe kodi kulingana na uhalisia wa kodi zao na hivyo kupunguza fedha za Serikali, tukumbuke kwamba tukiimarisha uadilifu tutaongeza mwamko wa wananchi kulipa kodi kwa hiari,” alisema Mbibo.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Mambo ya Ndani ya mamlaka hiyo, Amiram Lekey alisema kuwa lengo la mkakati huo ni kupunguza rushwa kwa kutumia mbinu za kuzuia na kupambana na rushwa hasa katika sekta zenye vishawishi vya rushwa ikiwemo Mamlaka ya Mapato.

“TRA imeunda kamati hizi katika ngazi mbalimbali kuanzia ngazi ya taasisi, mkoa, wilaya na vituo vya kodi ikiwa ni sehemu ya kutekeleza mpango mkakati wa mamlaka wa Kupambana na Rushwa wa awamu ya tano ulioanza mwaka 2017 hadi 2022,” alisema Lekey.

Alisema mafunzo hayo ya kuwajengea uwezo makatibu wa kamati hizo za kudhibiti uadilifu ndani ya mamlaka yanashirikisha makatibu wa kamati zah kudhibiti uadilifu za idara zilizopo ndani ya TRA, Chuo cha Kodi (ITA), TRA Zanzibar, vituo vya kodi na mikoa yote hapa nchini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles